Watu wengi wamekuwa wanafikiria lengo kubwa la maisha ni kutafuta usalama.

Ndiyo maana wengi wanashindwa kuondoka kwenye ajira, kwa sababu wanaamini ni salama zaidi kwa upande wa kipato kuwa kwenye ajira kuliko kuwa nje ya ajira.

Mambo mengi watu wanafanya kwa lengo la kuwa salama zaidi kwenye maisha yao.

Lakini kupata usalama kamili kwenye maisha ni kitu kigumu sana, hakuna chochote chenye uhakika kwenye maisha. Chochote tunachotegemea kwenye maisha, kinaweza kwenda kinyume na matarajio yetu na likawa tatizo kubwa kwetu.

Hivyo badala ya kuweka nguvu zetu kwenye kitafuta usalama ambao hauna uhakika, ni vyema kuelekeza nguvu hizo eneo sahihi.

Na eneo sahihi ni kutafuta uwezo, kazana kujijengea uwezo ambao utakuwezesha kukabiliana na chochote kitakachotokea kwenye maisha yako. Kadiri unavyokuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na chochote kinachotokea, ndivyo unavyokuwa huru na maisha yako.

Kama kwa chochote kinachotokea una uwezo wa kupambana nacho au uwezo wa kukipokea na maisha yakasonga mbele, kama hakuna kitu kimoja kinachoweza kuyakwamisha maisha yako, basi una uhuru mkubwa.

Na kama ukijijengea uwezo wako, hasa kwa upande wa fikra, utagundua hakuna kinachoweza kukushinda au kuwa kikwazo kwenye maisha yako kama tu upo hai. Kwamba chochote unachokutana nacho kwenye maisha, hata kama ni kigumu kiasi gani, kitakuwa na majibu au kama hakina basi utaweza kuishi nacho.

Kazana kujenga uwezo wako ili uwe na uhuru na maisha yako, badala ya kukazana kujenga usalama ambao hauwezi kudumu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha