“Whenever you find yourself blaming providence, turn it around in your mind and you will see that what has happened is in keeping with reason.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 3.17.1
Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumepata nafasi nyingine bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUNA SIKU UTAELEWA…
Udhaifu wetu binadamu uko hapa; tunaweka mipango, halafu tunataka kila kitu kiende kama tulivyopanga.
Inapotokea kitu kikaenda tofauti na tulivyopanga tunachukia na kukata tamaa, tunaona maisha hayana maana au hatuna bahati.
Lakini ukweli ni kwamba, kila kinachotokea ni kwa sababu fulani, na ni kwa manufaa bora zaidi kwako japokuwa kimekuja nje ya mipango yako.
Hivyo kama utapokea kila kinachotokea kwa mikono miwili, na kuamua kukitumia vizuri, kuna siku utakuja kuelewa maana yake. Kuna siku utakuja kuona faida yake kubwa, japo kitu hicho kilikuja na maumivu kwako.
Ndiyo maana wapo watu wanaofukuzwa au kukosa kazi waliyoitegemea sana, lakini wakaja kupata kazi nyingine bora kuliko ile ya awali. Wakati wanakosa kazi ya awali waliumia na kuona hawana bahati, lakini wanapokuja kupata kazi nyingine bora, wanashukuru kwa kukosa ile kazi ya awali.
Kadhalika watu wanafukuzwa au kukosa kazi ambazo walitegemea sana, na hilo linawasukuma kujiajiri na wanafanikiwa sana. Huenda wasingekuwa na uthubutu wa kuacha kazi wenyewe na kujiajiri, lakini kwa kufukuzwa, wanakuwa hawana namna, na hilo ndiyo linawaletea ukombozi wao.
Hata kwenye mahusiano mbalimbali, kuna wakati mahusiano yanafikia ukingo, hayawezi kuendelea tena. Mtu unaumia sana katika hatua hiyo, lakini baada ya mahusiano hayo kuvunjika, unapata nafasi ya kutengeneza mahusiano bora zaidi na mtu mwingine. Mpaka unajiuliza nini kilikuwa kinanichelewesha kwenye mahusiano ya mwanzo.
Rafiki, kumbuka kila kinachotokea, hata kama kinavuruga kabisa mipango yako, hakijatokea kwa bahati mbaya. Kina zawadi kubwa sana kwako ndani yake. Siyo rahisi kuiona kwa haraka kwa sababu unakuwa umetawaliwa na hisia za kupoteza ulichotegemea.
Lakini ipo siku utakuja kuelewa maana ya kile ulichopitia na kuona jinsi kimekuwa na manufaa kwako.
Hivyo haijalishi unakutana na magumu kiasi gani, jua hayo ni maandalizi ya wewe kufikia ukuu.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kupokea kila usilotegemea, ukijua ni mpango mkubwa na bora zaidi kwako.
#KunaSikuUtaelewa, #KisichokuuaKinakuimarisha, #KilaKituKinatokeaKwaSababu
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha