Kama kuna tabia mbaya ambazo unashindwa kuzivunja, kunaweza kuwa na sababu kubwa mbili zinazosababisha ushindwe kuvunja tabia hizo.
Sababu ya kwanza ni msongo wa mawazo, unapokuwa na msongo wa mawazo kuna baadhi ya tabia unaweza kuwa unazitumia kuondokana na msongo huo. Inawezekana ni manunuzi makubwa unayofanya ya vitu usivyohitaji, au utumiaji wa vilevi mbalimbali, yote haya yanaweza kuwa njia ya wewe kuvuka hali ya msongo uliyonayo.
Sababu ya pili ni uchoshi, pale unapokuwa umechoka, akili yako inaweza kukutuma kufanya tabia ambazo zinaondoa uchoshi huo. Tabia kama kuzurura kwenye mitandao ya kijamii, kupiga soga na wengine na hata matumizi ya vilevi, inasukumwa na uhitaji wako wa kuondokana na uchovu.
Unapokuwa na tabia mbaya ambayo unataka kuivunja lakini kila mara unakwama, acha kuangalia tabia hiyo na angalia ni wakati gani unafanya tabia hiyo. Kwa kuangalia kinachokusukuma kufanya tabia hiyo, utaweza kutumia njia sahihi ya kuvuka tabia hizo.
Na kwa kuwa sababu tumeshazijua ni mbili, kila unapokuwa na msongo chagua kufanya vitu vitakavyokuondolea msongo huo lakini havina madhara kwako. Vitu kama kufanya tahajudi, kutafakari kwa kina na hata kuangalia upande chanya wa kila unachopitia, itakusaidia kuona namna bora ya kuvuka unachopitia.
Pia unapokuwa na uchovu, badala ya kukimbilia kufanya vitu ambavyo akili inaona ni rahisi kufanya, tenga muda wa kupumzika, kwa kutokufanya chochote kabisa. Yaani wewe unapumzika. Wala usishike simu yako kuingia mtandaoni, wala usitafute marafiki wa kujipumzisha nao, pumzika mwenyewe kwa utulivu na utaondoa uchovu wako bila ya kujenga tabia itakayokugharimu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,