Mtu mmoja amewahi kumuuliza Mjasiriamali na Bilionea Richard Branson ambaye anamiliki makampuni zaidi ya 400 kwamba anawezaje kuwa na mlinganyo wa kazi, maisha na burudani, anatengaje muda wa kazi, muda wa maisha na hata muda wa burudani?
Richard Branson kwa mshangao aliuliza, kwani vitu hivyo vimetenganishwa? Si vinapaswa kuwa kitu kimoja?
Na hili ni funzo kubwa sana ambalo tunajifunza kutoka kwa wale waliofanikiwa sana, ambao tunawaona wakifanya mambo mengi, ambayo tunajiuliza kwa mambo hayo mengi wanayofanya wanapata wapi muda wa maisha.
Kumbe kwao kile wanachofanya ndiyo maisha yenyewe na ndiyo burudani pia. Hivyo hawahitaji kuacha kufanya ili waishi au wapumzike, kukifanya tu kitu hicho ni maisha kwao na ni burudani pia.
Ndiyo maana ni muhimu sana mtu kufanya kile ambacho unapenda kufanya, kile ambacho hata kama hakuna anayekulipa bado utafanya. Maana ukiwa unafanya hiki, hufikirii tena kuhusu maisha na burudani, kile unachofanya kwako kinakuwa ndiyo maisha na burudani pia.
Fanya kile unachopenda sana kufanya kwenye maisha yako, kile ambacho upo tayari kukifanya hata kama hakuna anayekulipa, ila wewe angalia watu gani wanaweza kukulipa na wape thamani kubwa kupitia kile unachopenda kufanya. Hili litafanya maisha yako kuwa na umoja, usiwe na hitaji la kuweka mlinganyo kati ya kazi, maisha na burudani.
Na kama hujafika hatua ya kuweza kufanya kile unachopenda kuwa ndiyo chanzo chako cha kipato, basi penda kile ambacho unafanya sasa. Usikubali kufanya chochote kama vile unapita pekee, usikubali kuchukulia chochote kwa urahisi. Badala yake weka mapenzi yako kwenye hicho unachofanya sasa, ambacho kinachukua sehemu ya maisha yako.
Na wala huhitaji nguvu kubwa kujilazimisha kupenda unachofanya, badala yake peleka mawazo yako kwenye kile unachofanya. Weka akili yako na mawazo yako yote kwenye kile unachofanya na utaona jinsi ulivyo na nafasi ya kufanya kwa ubora zaidi. Na kadiri unavyofanya kwa ubora, ndivyo unavyopenda zaidi kile unachofanya.
Fanya unachopenda au penda unachofanya na utakuwa na maisha kamili, ambayo kazi, maisha na burudani vinakuwa kitu kimoja na mafanikio uhakika.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,