“Chasing what can’t be done is madness. But the base person is unable to do anything else.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 5.17
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo,
Ni nafasi nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari WEWE NI ZAO LA MAFUNZO YAKO…
Hapo ulipofika sasa, siku kwa ajali wala bahati, bali ni matokeo ya mafunzo ambayo umekuwa unajipa mwenyewe.
Kama umepiga hatua ni kwa sababu umejifunza jinsi ya kupiga hatua na kufanyia kazi.
Na kama umekwama ni kwa sababu umejifunza jinsi ya kukwama na kubaki pale ulipo sasa.
Watu wengi wamekuwa ni wagumu kubadilika kwa sababu hawapp tayari kujifunza vitu vipya, vitu ambavyo hawajawahi kufanya huko nyuma.
Hivyo wanabaki pale walipo na wanaendelea kuwa zao la mafunzo waliyojipa huko nyuma.
Kama unataka kupiga hatua za tofauti na ulizopiga sasa, anza kwa kujifunza vitu tofauti na unavyojua sasa.
Kwa sababu kama ambavyo wanajeshi wanaema, hupandi kufikia matakwa yako, bali unaanguka kufikia kiwango cha mafunzo yako.
Chukua hatua sasa kujifunza upya, kujifunza yale ambayo yatakuwezesha kupiga hatua zaidi.
Jifunze kuwa na nidhamu binafsi, kwa kufanya kila unachopanga kufanya bila ya kuahirisha.
Jifunze kuwa na nidhamu kwenye muda wako, kwa kufanya yale ambayo ni muhimu na kuachana na yasiyo muhimu.
Jifunze kudhibiti na kutawala akili yako, ili uweze kuitumia kwa usahihi na siyo kuruhusu utawaliwe na hisia.
Unachopata ni matokeo ya mafunzo uliyonayo, kupata zaidi jifunze zaidi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujifunza njia mpya za kuwa bora zaidi ya pale ulipo sasa.
#JifunzeKuwaBora, #AchanaNaMazoea, #JaribuVituVipya
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha