#TANO ZA JUMA #13 2019; Kuumia Ni Kuchagua, Jinsi Ya Kutawala Akili Yako Ili Usiumizwe, Kanuni Ya Asilimia 40 Ya Kujisukuma Zaidi, Usitake Fedha Kabla Hujakomaa Kiakili Na Cha Kubobea Ili Ufanikiwe.

Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye tano za juma la 13 la mwaka huu 2019.

Hapa nimekuandalia mambo matano makubwa ya kujifunza na kuchukua hatua ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi kutoka kwenye kitabu nilichosoma kwa kina.

Juma hili la 13 tunakwenda kujifunza kutoka kitabu kinachoitwa Can’t Hurt Me: Master Your Mind and Defy the Odds ambacho kimeandikwa na Mwanajeshi mstaafu David Goggins.

cant hurt me

David Goggins amepitia maisha magumu sana tangu utoto wake mpaka utu uzima. Kwanza kabisa utoto wake ulikuwa wa mateso sana kutokana na kuwa na baba ambaye alikuwa akiwanyanyasa watoto na mke pamoja na kuwatumikisha kwenye biashara zake. Baada ya wazazi wake kuachana na yeye kuondoka na mama yake, maisha yalikuwa magumu zaidi kwa kuwa mama hakuwa na kazi wala elimu. Kitu kingine kilichomletea mateso zaidi kwenye maisha ni kwamba ni Mmarekani mweusi ambaye alikuwa akibaguliwa sana kila alipoenda. Kuanzia shuleni mpaka jeshini, kote alikuwa mtu mweusi peke yake, kitu kilichomfanya akutane na ubaguzi mara nyingi.

Lakini licha ya magumu yote aliyopitia, licha ya mateso makali aliyokutana nayo kwenye maisha, David alielewa kitu kimoja, kuumia ni kuchagua, na hivyo aliamua kutokuumia, na kugeuza mateso kuwa sehemu ya yeye kukua zaidi.

Kuchagua kwake mateso kuwa sehemu ya kukua kulimwezesha kuwa Komandoo kwenye jeshi la Marekani, kushiriki zaidi ya marathoni 60 na kuvunja rekodi ya dunia kwenye mazoezi ya kuvuta mwili kwa mikono. David ameyaweza haya kwa kuchagua ugumu na mateso na kutokukubali kuumia. Katika tano za juma hili tunakwenda kujifunza jinsi tunavyoweza kuwa bora zaidi kwa kupitia ugumu na mateso na kutokukubali kuumia.

Karibu ujifunze na kuchukua hatua ili kuwa bora zaidi.

#1 NENO LA JUMA; KUUMIA NI KUCHAGUA.

Rafiki, maumivu yamekuwa kikwazo cha wengi kufanikiwa kwenye maisha yao.

Jaribu kujiangalia wewe mwenyewe, angalia kila ambacho umewahi kushindwa na ukakata tamaa, ni kitu gani kilikufanya ukubali kushindwa? Ukiangalia kwa umakini unakuta jibu ni moja, ulishindwa au kukata tamaa kwa sababu hukutaka kuumia zaidi. Ulikuwa umefikia ugumu na mateso ambao ulijiambia huwezi kuendelea tena.

Lakini pia angalia kitu chochote ambacho umewahi kukitaka kweli kwenye maisha yako, kitu ambacho hukuweza kuwa tayari kuendelea na maisha bila ya kuwa nacho. Kitu ambacho kilikuwa kigumu sana kwako kupata, lakini ulikomaa mpaka ukakipata. Je katika wakati huu uliyasikia maumivu? Na je maumivu hayo yaliondoa ile shauku kubwa iliyokuwa ndani yako ya kupata unachotaka? Jibu ni hapana, kwa kile ulichotaka hasa, hukuruhusu kitu chochote kikuzuie kupata.

Mifano hii miwili, kutoka kwenye maisha yako mwenyewe inapaswa inakufundisha kitu kimoja, kuumia ni kuchagua. Japokuwa wote tunakutana na ugumu na mateso, lakini kuumia kiasi cha kusema siendelei tena ni kuchagua mwenyewe. Kama umejitoa kweli na unataka kweli, utayapata maumivu lakini utayapuuza, kwa sababu unachotaka ni muhimu kuliko maumivu hayo.

Na hilo ndilo linalohitajika ili ufanikiwe kweli, hutaweza kufanikiwa kweli kama huwezi kuendelea kufanya licha ya kuwa na maumivu. Lazima uwe tayari kuyapuuza maumivu, lazima uwe tayari kujisukuma zaidi hata pale unapokuwa unaona umefika ukomo, na hapo ndipo unapata kile ambacho wachache wanapata.

Sababu pekee kwa nini wachache ndiyo wanaofanikiwa na wakifanikiwa inakuwa ni kwa kiwango kikubwa kuliko wanaoshindwa ni kwamba wengi wanarudishwa nyuma na maumivu, na hivyo kileleni kunakuwa na nafasi kubwa ila wanaofika ni wachache. Hivyo wale wanaoweza kuyavuka maumivu na kuendelea, wanapofika kileleni wanayafurahia mafanikio tele.

Chagua kutokuumia na hakuna chochote kitakachokuzuia kufanikiwa.

#2 KITABU CHA JUMA; JINSI YA KUTAWALA AKILI YAKO ILI USIUMIZWE.

Kama ulivyoona kwenye utangulizi, juma hili tunakwenda kujifunza kutoka kitabu kinachoitwa Can’t Hurt Me: Master Your Mind and Defy the Odds ambacho kimeandikwa na Mwanajeshi mstaafu David Goggins.

Kwa kuwa kitabu hiki kimeandikwa na mwanajeshi, na mfumo wa mafunzo uliotolewa humu umekaa kijeshi, basi katika uchambuzi huu tutaongozwa na misheni ya kuyakomboa maisha yetu kutoka kwa adui anayetuzuia ambaye ni sisi wenyewe.

Kupitia kitabu hiki, tunakwenda kwenye vita dhidi yetu wenyewe, yaani tunakwenda kupambana na sisi wenyewe, ili tuache kujihujumu na kujirudisha nyuma, tufungue uwezo wetu mkubwa na kuutumia kufanikiwa zaidi.

Hivyo Kamanda David Goggins anatupa tangazo la vita, vita ambayo tunapaswa kupigana ili kuwa na maisha ya mafanikio.

TANGAZO LA VITA;

MUDA; 24/7, masaa 24 kwa siku, siku 7 za wiki.

WAHUSIKA; Wewe mwenyewe.

HALI ILIVYO; Maisha yako yapo hatarini kwa kuishi kwa mazoea na umekuwa laini sana kiasi kwamba utakufa bila ya kujua uwezo mkubwa uliopo ndani yako.

MISHENI; kufungua pingu za akili yako, kutupa sababu zako, kuyamiliki maisha yako kwa ukamilifu na kujenga msingi usiovunjika.

UTEKELEZAJI; moja; soma kitabu na pokea changamoto kumi zilizopo kwenye kitabu hiki na kuzielewa. Rudia tena ili kuimarisha zaidi akili yako.

Mbili; fanyia kazi kila changamoto kwenye maisha yako, ukifanya kwa ubora utapata maumivu. Lakini kumbuka lengo la misheni hii siyo kujisikia vizuri, bali kuwa na maisha bora.

Tatu; usiache kufanya pale unapochoka, bali acha kufanya pale unapokuwa umemaliza kile ulichopanga kufanya.

AINISHO; Hii ni hadithi halisi ya shujaa. Shujaa huyo ni wewe.

Baada ya tangazo hili la vita, sasa tunakwenda moja kwa moja kwenye vita yenyewe, na katika vita hii, kuna changamoto kumi za kufanyia kazi ili kupata ushindi ambao ni maisha ya mafanikio. Tutakwenda kujifunza kila changamoto na hatua za kuchukua ili kuwa bora zaidi.

CHANGAMOTO YA KWANZA; TAMBUA SABABU ZINAZOKUZUIA

Kila mtu kuna magumu na changamoto ambazo anazipitia kwenye maisha yake. Hakuna ambaye anapata kila anachopaswa kupata kwenye maisha. Watu wengi wamekuwa wanatumia magumu waliyopitia kama sababu kwa nini hawawezi kufanya makubwa kwenye maisha yao. David alikuwa na kila sababu kwa nini asingeweza kufanikiwa kwenye maisha yake, alipata malezi mabaya utotoni, hakuwa akiweza kusoma vizuri na maisha yalikuwa magumu. Lakini aliziweka sababu zote pembeni na kuweka juhudi hadi akafanikiwa.

Jiulize ni magumu gani ambayo umewahi kupitia kwenye maisha yako ambayo unajiambia yamekuzuia usifanikiwe. Je ulinyanyaswa utotoni? Je umetokea familia masikini? Je hukuwa unafanya vizuri shuleni na ukaambiwa hutakuwa na maisha mazuri? Tambua hizo zote kama hadithi ambazo zinakuzuia wewe kupiga hatua.

Pia angalia magumu yoyote unayopitia sasa ambayo yanakuzuia usifanikiwe. Kwenye kazi, biashara na hata maisha, ni vitu gani vimekuwa kikwazo kikubwa kwako ambavyo unajiambia kama visingekuwepo basi maisha yangekwenda vizuri?

HATUA YA KUCHUKUA; Chukua kitabu chako cha kuandika mambo yako muhimu kisha andika sababu zote unazojipa kwa nini huwezi kupiga hatua na kufanikiwa. Kisha geuza sababu hizi kuwa msukumo wa wewe kufanikiwa. Kile kinachokuzuia kufanikiwa kifanye kiwe sababu ya wewe kufanikiwa.

Kuwa na orodha hii ya sababu zote unazofikiri zinakuzuia kufanikiwa kisha zigeuze kuwa hamasa ya wewe kufanikiwa. Kama kuna kitu ulishindwa huko nyuma, au watu walikunyanyasa, fanya hayo kuwa msukumo wa kufanikiwa ili usishindwe tena au usiwape tena watu nafasi ya kukunyanyasa.

CHANGAMOTO YA PILI; KIOO CHA UWAJIBIKAJI

Kikwazo kikubwa cha mafanikio yako ni wewe mwenyewe, kwa sababu umekuwa unajidanganya sana. Pale mambo yanapokuwa magumu, badala ya kuyakabili wewe unatafuta njia ya mkato. Huwezi kufanikiwa kwa kukimbia magumu na kutafuta njia ya mkato. Badala yake unakuwa unatengeneza matatizo zaidi. David alipokuwa na changamoto ya kushindwa kusoma shuleni, badala ya kulikabili hilo, yeye aliamua kuwa anaiga kazi za wenzake. Alifaulu lakini alizidi kwenda madarasa ya juu akiwa hajui kusoma.

Ni wakati wako sasa wa kuja uso kwa uso na nafsi yako, kuuangalia ukweli kama ulivyo na kujiambia ni wapi ulipo, ukilinganisha na kule unakokwenda. Unapaswa kuwa na kioo cha uwajibikaji, eneo ambalo unaweza kubandika malengo yako na kuyaona kila siku. Inaweza kuwa chumbani kwako, au ofisini kwako, lakini liwe eneo ambalo unaweza kubandika kitu na kukiona kila siku.

Andika malengo yako makubwa uliyonayo na maono yote uliyonayo kisha bandika kwenye eneo hilo. Kisha kwenye kila lengo andika hatua unayopaswa kuchukua ili kufika pale. Jifanyie tathmini ya pale ulipo sasa na kule unakotaka kufika kisha jiambie kwa ukweli na bila ya kujibembeleza ni hatua zipi unapaswa kuchukua.

Kama lengo lako ni kuongeza kipato, jiambie ukweli pale ulipo sasa, kama upo kwenye madeni au umefulia kabisa. Kama lengo ni kuboresha afya jiambe pale ulipo sasa, kama uzito umepitiliza au maradhi yanakuandama. Usijidanganye kwa namna yoyote ile, ukabili ukweli kama ulivyo.

Kila siku tembelea eneo lako la kuyaona malengo, na kila hatua unayopiga nenda hatua ya juu zaidi.

David alipogundua kwamba hajui kusoma vizuri na hilo ni kikwazo kwake kujiunga na jeshi, alijiwekea lengo la kujifunza kusoma kwa usahihi na alilifanyia kazi lengo hilo usiku na mchana, kitu ambacho kilimwezesha kusoma na kujiunga na jeshi. Kadhalika alipokuwa na uzito uliopitiliza na hilo kuwa kikwazo kwake kupokelewa jeshini, alijiwekea lengo la kupunguza uzito na ndani ya miezi mitatu alitoka uzito wa paundi 297 mpaka paundi 190, aliweza kupunguza paundi zaidi ya 100 ( kg) ndani ya miezi mitatu, kitu ambacho wengi walimwambia hakiwezekani.

Kwa lengo lolote ulilonalo, unapaswa kujiweka kwenye mpango wa uwajibikiaji kwa hatua ndogo ndogo za kukuwezesha kulifikia. Mafanikio yanahitaji kujitoa na nidhamu ya hali ya juu, hayatakuwa rahisi, lakini inawezekana.

CHANGAMOTO YA TATU; NENDA NJE YA MAZOEA.

Hatua ya kwanza ya kukomaza akili yako ili uweze kufanikiwa ni kwenda nje ya mazoea. Maisha unayoishi ni ya mazoea, umekuwa unafanya kile ambacho umezoea kufanya na hupendi kujaribu vitu vipya, kwa sababu huna uhakika na matokeo ya vitu hivyo vipya. Kwa njia hii umekuwa unajizuia mwenyewe kupiga hatua, kwa sababu kama unafanya ulichozoea kufanya, utapata matokeo ambayo umekuwa unayapata. Matokeo makubwa, mafanikio na hata ukuaji upo nje ya mazoea yako, ni kwa kufanya vitu ambavyo hujazoea kufanya ndiyo utaweza kujisukuma zaidi.

David alijifunza kwamba maisha ya mazoea yasingemwezesha kufikia malengo yake makubwa kwenye maisha. Mfano alipoenda jeshini, aligundua ni kujisukuma zaidi ya mazoea ndiyo kitu kitakachomwezesha kufanikiwa katika jeshi.

Chukua kitabu chako na andika mambo yote ambayo umezoea kufanya. Andika pia yale mambo ambayo umekuwa hupendi kuyafanya, mambo ambayo ukifikiria kuyafanya unajisikia vibaya na kuogopa kwamba utashindwa. Haya ndiyo mambo ambayo yatakuwezesha kufanikiwa zaidi.

Katika yale ambayo umeorodhesha kama hupendi kuyafanya au ni magumu kwako kufanya, kila siku chukua hatua ya kufanya kitu katika orodha hiyo kila siku fanya kitu ambacho hupendi kufanya, fanya kitu ambacho kitakusukuma zaidi ya ulivyozoea.  Kwa kufanya hivi kila siku utaikomaza akili yako na kuwa bora zaidi. Utajiamini kwamba unaweza na hakuna chochote kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa.

CHANGAMOTO YA NNE; TEKA MIOYO.

Maisha huwa yanatuweka kwenye mazingira ya mashindano, kitu ambacho wengi wamekuwa wanakihofia kwa sababu wakishindwa wanajiona hawafai. Kila mtu kuna watu ambao inabidi awashinde kwenye maisha yake ili kupiga hatua zaidi. Inaweza kuwa ni mfanyakazi au mfanyabiashara mwendako, inaweza kuwa ni mwalimu au kocha wako, inaweza kuwa ni bosi au mwajiri wako na pia inaweza kuwa ni mteja wako. Hawa wanakuwa ni watu ambao unahitaji kufanya vizuri sana ili kuwaridhisha au kwenda nao vizuri. Na njia pekee ya kuweza kufikia hilo ni kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana, kufanya kwa namna ambayo wao wenyewe hawawezi kufanya au hawajawahi kuona ikifanywa.

David anaita hilo kuteka mioyo, anasema mtu yeyote ambaye unataka akuheshimu, basi fanya kitu ambacho yeye mwenyewe hawezi kukifanya. Na kama mtu anakunyanyasa au kukuumiza kwa makusudi, kuwa imara na onesha kwamba anachofanya hakina maumivu yoyote ndani yako. Wale wanaokusumbua huwa wanafurahi wakiona unaumia, lakini kama wewe huumii na upo imara, wanakuheshimu sana. David aliliona hilo kwenye mazoezi ya kijeshi, pale walimu wao walipokuwa wakiwapa mazoezi makali ya kuwaumiza, yeye aliyafanya bila ya kuruhusu kuumia, kitu ambacho kilipelekea yeye achukuliwe wa tofauti kabisa na wengine.

Kwa yeyote unayemfanyia kazi sasa au anayekusimamia, njia pekee ya kuteka moyo wake na kumfanya akuheshimu sana ni kufanya kazi yako kwa ubora wa hali ya juu, ambao wao wenyewe hawawezi kufanya na hawajawahi kuona mtu mwingine akifanya. Na hilo lipo ndani ya uwezo wako kama utajisukuma na kutoka nje ya mazoea.

Hata katika hali ya ushindani wa kawaida, kama kuna mtu anataka kukuzidi kwenye kile unachofanya, wewe fanya kwa viwango vya juu sana, ambavyo yeye mwenyewe hajawahi kufikiria kama vinawezekana. Na kwa viwango hivyo, siyo tu ataishia kukuheshimu, bali wengine watakuogopa kabisa.

CHANGAMOTO YA TANO; TASWIRA YA MAFANIKIO.

Mtu wa kawaida huwa anafikiria mawazo elfu mbili mpaka elfu tatu kwa saa moja, na sehemu kubwa ya mawazo hayo ni mambo hasi na yasiyo na faida yoyote kwa mtu. Sasa huo ni upotevu wa muda na nguvu zako. Unahitaji kutumia mawazo yako hayo kutengeneza taswira ya mafanikio yako. Baada ya kuwa umeweka malengo yako, pata picha ukiwa umeshayakamilisha na jione jinsi unavyokuwa umepiga hatua baada ya kuyafikia malengo hayo. Kisha mara kwa mara ona taswira hii kwenye mawazo yako. Muda wote mawazo yako yatawaliwe na malengo ambayo umejiwekea.

David amekuwa anatumia njia hii kupiga hatua zaidi, kwenye kila jukumu kubwa analoingia, anaingia kama tayari ameshashinda. Kwenye mbio ndefu alizokuwa anashiriki, anakwenda kushiriki kama tayari ni mshindi. Muda wote akili yake imekuwa inaangalia kwenye ushindi na hili siyo tu lilimsukuma zaidi kufanikiwa, bali pia lilimzuia asikate tamaa na kuishia njiani. Huwezi kukata tamaa kama tayari umeshajiona ni mshindi.

Kwa malengo uliyojiwekea, kila wakati pata picha kama tayari umeshayafikia malengo hayo, pata picha upo kwenye kilele cha mafanikio, ona jinsi inavyokuwa ufahari kwako kupata mafanikio hayo, na hilo litakusukuma zaidi. Pia pata picha ya changamoto unazoweza kukutana nazo katika safari yako ya mafanikio na jione ukiwa unazivuka changamoto hizo na kuelekea kwenye ushindi.

Kumbuka kujipa taswira siyo mbadala wa kuweka kazi, kazi lazima uweke sana, kujipa taswira ni kumiliki akili yako ili isiwe kikwazo kwako. Kwa sababu kama hutajipa mawazo ya mafanikio yako, basi mawazo ya kushindwa yatatawala akili yako.

CHANGAMOTO YA SITA; KOPO LA BISKUTI.

Kila mtu kwenye maisha ana mambo ambayo amewahi kuyapitia, ambayo yalikuwa magumu kwake lakini akayavuka. Kila mtu kuna malengo ambayo aliwahi kujiwekea na akayafikia. Na kila mtu kuna mambo amewahi kushindwa, lakini hakukata tamaa na baadaye akafanikiwa. David anaita mambo haya KOPO LA BISKUTI, yaani ni kama zawadi ambayo unaweza kuitumia kupiga hatua zaidi.

Pale unapokuwa umejiwekea malengo na katika kuyafanyia kazi ukakutana na ugumu, jikumbushe jinsi ambavyo umewahi kuvuka ugumu huko nyuma, jikumbushe malengo uliyowahi kujiwekea na ukayafikia na pia jikumbushe mambo uliyowahi kushindwa, lakini ukapambana mpaka ukafanikiwa. Kwa kujikumbusha haya ya nyuma, utapata nguvu ya kuendelea zaidi na hivyo kufanikiwa zaidi.

David alikuwa akitumia mafanikio na kushindwa kwake kwa nyuma kujisukuma kufanikiwa zaidi. Kila alipokutana na ugumu alijikumbusha jinsia amewahi kuvuka ugumu mwingine huko nyuma.

Andaa mifano yako binafsi ya jinsi ambavyo umewahi kufanikiwa huko nyuma na jikumbushe mifano hii kila unapokutana na ugumu katika kufanyia kazi malengo ya sasa. Kwa kutumia mifano yako mwenyewe utapata hamasa kubwa ya kupiga hatua zaidi.

CHANGAMOTO YA SABA; ONDOA KIDHIBITI MWENDO.

Kila mmoja wetu ana kidhibiti mwendo ambacho kipo kwenye akili yake, inawezekana amejiwekea mwenyewe au amewekewa na jamii kwa kuambiwa nini anaweza kufanya na nini hawezi kufanya. David anaita hili KANUNI YA ASILIMIA 40, kwamba uwezo unautumia sasa ni asilimia 40 tu ya uwezo ambao unao.

Jiulize ni uwezo kiasi gani umekuwa unatumia sasa, angalia ni ukubwa wa kazi kiasi gani umekuwa unafanya, ni ugumu kiasi gani umekuwa unaweza kuukabili na tambua kwamba mwisho wako umekuwa ni asilimia 40 tu ya uwezo wako. Yaani pale unapokuwa unajiona umechoka sana na huwezi kuendelea tena, basi hapo jua hujafika mwisho wako, bali umefika asilimia 40 ya uwezo wako. Ila akili yako inakudanganya kwamba umefika mwisho.

Njia ya kuondokana na hili ni kuongeza asilimia 5 zaidi kila unapokuwa umefika mwisho na kuona huwezi kuendelea tena. Kama umezoea kukimbia kilometa 10 na kuona ndiyo mwisho wako, kimbia zaidi ya hapo kwa asilimia 5. Hata kwenye kazi zako, pale unapoona umefika mwisho, jisukume kwa asilimia 5 zaidi.

Kujisukuma zaidi ndiyo njia pekee ya kufikia uwezo mkubwa uliopo ndani yako na kukomaza akili na mwili wako. Usiache kufanya pale unapokuwa umechoka, bali nenda zaidi ya ulivyozoea kwenda. Kumbuka hii ni vita yako dhidi yako mwenyewe, hivyo lazima ujisukume zaidi ya ulivyozoea ili kuweza kushinda vita hii. Unashindana na wewe wa jana, hivyo fanya leo kitu ambacho hukufanya jana.

CHANGAMOTO YA NANE; PANGILIA SIKU YAKO.

Kila mtu anasema hana muda, lakini ukiangalia siku ya kila mtu, kuna muda mwingi ambao anaupoteza kwa kutofanya lolote, au mbaya zaidi kufanya mambo ambayo hayana faida yoyote kwake. Wengi wanafanya mambo mengi kwa wakati mmoja na hili linapunguza ufanisi wao. Kwa mfano mtu anafanya kazi huku anawasiliana na simu, ni wazi ubora wa kazi anayofanya hautakuwa mkubwa.

David anatushirikisha zoezi la kufanya kwa wiki tatu ili kuweza kushika umiliki wa muda wetu na kupangilia siku yetu kwa namna ambayo tunaweza kufanya makubwa zaidi.

Wiki ya kwanza ishi kama ambavyo umekuwa unaishi sasa, lakini andika kila unachofanya kwenye kila muda wa siku yako. kila baada ya robo saa au nusu saa andika unafanya nini. Fanya hivi kwa wiki nzima bila ya kuacha chochote. Picha utakayoipata kwa wiki hii ya kwanza ndivyo ambavyo umekuwa unaendesha maisha yako, na hapo ndipo mabadiliko yanapaswa kuanzia.

Wiki ya pili anza kuishi tofauti, kwenye yale mambo uliyoorodhesha umekuwa unafanya kwa wiki ya kwanza, chagua yapi ni muhimu na yanayokufikisha kwenye malengo yako. Hayo ndiyo ya kuyapa kipaumbele na mengine yote achana nayo. Kwa wiki yako ya pili, tengeneza ratiba yako mpya ya siku ambapo unaweka vipaumbele vyako tu. Pangilia siku yako nzima kwa kila robo saa mpaka nusu saa. Unapoanza kutekeleza jukumu ulilolipangia muda, unafanya hilo tu kwa muda uliopanga, usijihusishe hata na simu yako. Bora kuweka muda mfupi kwenye jambo moja kwa umakini, kuliko muda mrefu kwa kukosa umakini. Pia kwenye ratiba yako weka muda wa kupumzika na unapofika muda huo pumzika kweli, usijihusishe na chochote, hata simu.

Wakati unafanyia kazi ratiba yako ya wiki ya pili, andika yale unayojifunza na maboresho zaidi ya kufanya, lakini usibadili chochote. Kama kuna kitu umekipa muda mrefu kuliko kinavyostahili andika hilo, kama mapumziko ni mafupi au marefu andika.

Katika wiki ya tatu, boresha ratiba yako ya wiki ya pili kwa kupitia yale ambayo umeandika. Kufikia wiki hii unapaswa kuwa na ratiba ambayo imeshakamilika, ifuate hiyo na endelea kufanya marekebisho, lengo ni uwe na ufanisi mkubwa na kutumia vizuri muda na nguvu zako.

CHANGAMOTO YA TISA; KUWA WA TOFAUTI KATI YA WA TOFAUTI.

Watu wengi wamekuwa wakifikiri ukishafikia ngazi fulani ya maisha, kwa hadhi, heshima au mafanikio basi umeshamaliza kila kitu. David anasema kwamba haijalishi umefika juu kiasi gani, bado unaweza kwenda juu zaidi. Haialishi umeshakuwa wa tofauti kiasi gani, bado unaweza kuwa wa tofauti zaidi. Na hapa ndipo David alipojipa jukumu la kuwa wa tofauti licha ya kuwa kwenye kundi la watu tofauti. Yeye anaita UNCOMMON AMONGST UNCOMMON.

Mafanikio siyo kitua ambacho ukishapata mara moja basi utabaki nayo milele, mafanikio ni kitu ambacho unapaswa kuendelea kukifanyia kazi kila siku. Muda wowote yanaweza kutokea mambo na yakavuruga kabisa mipango yako, hivyo kujiachia baada ya kufanikiwa ni kujiandaa kuanguka.

Kila wakati kuwa na kitu cha kukusukuma, kila wakati kuwa na malengo makubwa unayofanyia kazi. Unapofikia lengo kubwa ulilojiwekea, weka lengo jingine kubwa zaidi. Unapokuwa wa tofauti kama unavyotaka, kazana kuwa wa tofauti zaidi. Hufanyi hivi kwa sababu hujaridhika, bali unafanya hivi kwa sababu unajua unaweza kufanya zaidi, na popote ulipo sasa hutabaki hapo milele.

Popote ulipo, hata kama watu wanakuambia uko juu kiasi gani na huhitaji kujitesa tena, usiwasikilize, endelea kujisukuma, endelea kujitesa. Wengi wamekuwa wanakuwa laini sana wakishapata mafanikio, kitu ambacho kinawafanya washindwe kirahisi. Ifanye kila siku yako kwenye kazi au biashara kuwa ndiyo siku ya kwanza, amka ukiwa umeyafuta kabisa mafanikio yote ambayo umeshayapata na anza upya. Kwa mtazamo huu kila siku utapiga hatua na utazidi kuwa juu kila siku.

CHANGAMOTO YA KUMI; RIPOTI BAADA YA TUKIO.

Wanajeshi wana kitu wanakiita AFTER ACTION REPORT. Yaani kila baada ya tukio unalokuwa umefanya, unapaswa kukaa chini na kuandika ripoti ya tukio hilo. Na unapaswa kuandika pande zote mbili, nini kilikwenda vizuri na kikaleta matokeo mazuri na pia nini kilikwenda vibaya na kuleta matokeo mabaya.

Kwa kufanya zoezi hili, utaweza kujifunza mengi sana kwako mwenyewe, na utakapochukua hatua wakati mwingine utajua yapi ya kufanya na yapi ya kuepuka ili ufanikiwe zaidi.

Kwa kila hatua unayochukua kufikia malengo yako, unapaswa kuandaa ripoti yako ya baada ya tukio. Andika yale uliyofanya vizuri na yale uliyofanya vibaya. Andika maandalizi uliyokuwa nayo na kama yalitosha au hayakutosha. Kisha unapokwenda kuchukua hatua tena weka maboresho kulingana na ulichojifunza kwenye ripoti yako.

Kuna mambo mengi utafanya na kushindwa kwenye maisha yako, badala ya kuangalia upande wa kushindwa pekee, angalia pia unajifunza nini kwa kila hatua unayochukua. Ukijifunza na wakati mwingine ukafanya kwa ubora zaidi, lazima utafanikiwa.

Rafiki, hizo ndizo changamoto kumi za kufanyia kazi kwenye maisha yako kutoka kwa kamanda David Gogging, kumbuka uko vitani na adui yako ni wewe ambaye umekuwa unaishi kwa mazoea, kumbuka vita hii ni ya masaa 24 kwa siku na siku saba za juma. Hivyo tumia kila fursa unayoipata kuwa bora leo zaidi ya jana, jisukume zaidi ya ulivyozoea, na kwenye kila unalofanya, jifunze na kuwa bora zaidi. Kumbuka hili muhimu sana, usiache pale unapokuwa umechoka, bali acha pale unapokuwa umemaliza.

#3 MAKALA YA JUMA; KANUNI YA ASILIMIA 40 YA KUJISUKUMA ZAIDI.

Kutoka kwenye kitabu cha juma hili, mwandishi ametushirikisha dhana ya asilimia 40, ambapo anasema uwezo wa mwili wako unaotumia sasa ni asilimia 40 tu ya uwezo kamili.

Yaani pale unapokuwa umefanya kitu na kujiona umechoka mpaka mwisho, unaona huwezi kuendelea tena, hapo unakuwa umefika asilimia 40 ya uwezo wako. Unaweza kuendelea zaidi ya hapo na ukafanya makubwa kuliko ulivyozoea. Na hii ndiyo njia pekee ya kufanikiwa zaidi, kwa kwenda zaidi ya ulivyozoea sasa.

Kwenye makala ya juma hili, nimekushirikisha kwa kina kuhusu kanuni hii ya asilimia 40 na jinsi unavyoweza kuitumia kwenye maisha yako na ukaweza kufanya makubwa zaidi.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, isome sasa hivi hapa; Kanuni Ya Asilimia 40; Jinsi Unavyoweza Kuusukuma Mwili Wako Kufanya Makubwa Kuliko Ulivyozoea. (https://amkamtanzania.com/2019/03/29/kanuni-ya-asilimia-40-jinsi-unavyoweza-kuusukuma-mwili-wako-kufanya-makubwa-kuliko-ulivyozoea/)

Kila siku kuna makala nzuri sana za kujifunza na kupiga hatua zinawekwa kwenye mitandao yetu mikuu miwili, AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA, fanya kuwa utaratibu wako kuianza siku yako kwa kusoma makala kwenye mitandao hii, itakusaidia kuianza siku ukiwa na mtazamo sahihi wa mafanikio.

#4 TUONGEE PESA; USITAKE FEDHA KABLA HUJAKOMAA KIAKILI.

Hili halihitaji hata mfano lakini tuutumie tu ili tuelewane vizuri. Kumbuka mara yako ya kwanza kupata kiasi kikubwa cha fedha, ambacho hujawahi kupata huko nyuma wala kutegemea kupata, je ulizitumiaje fedha hizo? Kuwa muwazi na usijidanganye, je fedha hizo zilikusaidia au zilikupoteza zaidi?

Kwa walio wengi, wanapopata kiasi kikubwa cha fedha kuliko walivyotegemea au kuwahi kupata, fedha hizo huwa matatizo makubwa kwao. Wengi huzitumia vibaya, huharibu maisha yao, mahusiano yao na kuvuruga kabisa maisha yao. Wengine huenda mbali na kusema kwamba fedha zimewaharibu akili.

Lakini ukweli ni huu, ukipata fedha kabla hujakomaa kiakili, fedha hizo siyo tu zitakuharibu wewe, bali zitaharibu maisha yako kabisa.

Swali ni je unajikomazaje kiakili ili unapopata fedha nyingi zisigeuke kuwa uharibifu kwako?

Moja; jijengee msingi imara kifedha kwa kujua thamani halisi ya fedha na thamani ambayo upo tayari kuitoa ili kupata fedha.

Mbili; usipende vitu rahisi na njia za mkato za kupata fedha, hata kama wengine wanazitumia na kupata fedha, wewe achana nazo.

Tatu; kuwa tayari kujituma zaidi ili kupata fedha zaidi, kwa kila unachofanya, nenda hatua ya ziada, jisukume zaidi ya ulivyozoea na toa thamani kubwa kuliko wengine wanavyotoa.

Nne; kwa kila kipato unachoingiza, usitumie chote, badala yake sehemu ya kipato hicho ifanye kuwa akiba, na kuza akiba yako. Kadiri unavyoweza kukaa na akiba bila ya kuitumia, ndivyo ukipata fedha nyingi utakuwa na utulivu. Lakini kama ukipata fedha unatumia zote bila kuweka akiba kabisa, ukipata fedha nyingi maisha yako yatakuwa majanga.

Tano; unapokutana na kiasi kikubwa cha fedha kuliko ulivyozoea au ulivyotegemea, kuwa na utulivu mkubwa sana. Kwanza usiruhusu watu wengi kujua kwamba umepata kiasi kikubwa cha fedha, maana hao ndiyo watakufanya ushindwe kutulia, kwa kuja na vitu vingi unavyopaswa kufanya. Ukishakuwa na utulivu kabisa, rudi kwenye mipango uliyokuwa nayo awali na ona unawezaje kupiga hatua zaidi kwa fedha ulizopata. Kosa kubwa kabisa utakalofanya kwenye maisha yako pale unapopata fedha nyingi ni kuanza mipango mipya, ambayo hujawahi kuifikiri kwa kina na huna uzoefu nayo, hapo ndipo unapokwenda kuanguka vibaya.

Komaa kwanza kiakili kabla hujataka kupata fedha nyingi zaidi, maana kinachokusumbua sasa siyo kukosa fedha, bali kukosa ukomavu wa kiakili kwenye eneo la fedha. Maana kama fedha kidogo unayoipata huwezi kuituliza, nyingi itakuwa majanga kwako.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA;  UNACHOPASWA KUBOBEA ILI KUFANIKIWA SANA.

“Only you can master your mind, which is what it takes to live a bold life filled with accomplishments most people consider beyond their capability.” ― David Goggins

Wewe pekee ndiye unayeweza kubobea na kuitawala akili yako, na ndiyo kitu pekee unachohitaji ili kuweza kuishi maisha makubwa yenye mafanikio makubwa ambayo wengine hawajawahi kuyafikiria.

Huwa tunafikiri tunahitaji vitu vya nje ili kufanikiwa sana, lakini ukweli ni kwamba kila kitu tayari kipo ndani yetu, na inaanzia kwenye akili zetu. Akili zetu zina uwezo mkubwa sana, lakini pia ndiyo kikwazo kikubwa kama haijatengenezwa na kukomazwa vizuri.

Mfano pale unapokutana na ugumu na kukata tamaa, au unapojiambia umechoka au haiwezekani, jua kwamba huo siyo uhalisia, bali ni akili yako inakudanganya. Ukiweza kubobea kwenye udhibiti wa akili yako, na ukaiendesha badala ya kuiruhusu ikuendeshe, utaweza kufanya makubwa sana, ambayo wengine wakiangalia wanashangaa na kujiuliza umewezaje.

Tumeona hili kwenye maisha ya David Goggins ambaye ametoka chini kabisa na kuweza kufika mafanikio ya juu kwenye jeshi, bila ya kusaidiwa kwa namna yoyote bali kwa kuikomaza akili yake na kuweza kupuuza maumivu na kukata tamaa.

Tawala akili yako na dunia itakuwa yako, kwa kuwa utaweza kupata kila unachotaka, lakini kumbuka safari haitakuwa rahisi, ila uhakika ni inawezekana.

Rafiki, hizi ndiyo tano za juma hili, umejifunza mambo makubwa na muhimu sana, hivyo kilichobaki ni wewe kuchukua hatua ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi. Kama ungependa kupata kitabu hiki, pamoja na mafunzo mengine mazuri kutoka ndani ya kitabu hiki basi jiunge na CHANNEL YA TANO ZA JUMA, maelekezo ya kujiunga yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu