Rafiki yangu mpendwa,

Kila mtu anapenda kufanya makubwa na kufanikiwa sana kwenye maisha yake. Lakini wengi wanapojaribu kufanya makubwa, wanakutana na kikwazo kikubwa ambacho kinawazuia wasiweze kufanya makubwa. Kikwazo hicho ni miili yetu.

Miili yetu haina tofauti na gari, ndani yetu tuna kidhibiti mwendo (speed governor) ambacho kinatuzuia tusiweze kupiga hatua zaidi. Kama ambavyo gari lenye kidhibiti mwendo haliwezi kuvuka kiasi fulani cha mwendo, ndivyo pia miili yetu ina ukomo wa hatua tunazoweza kuchukua.

Hii ni dhana ambayo mwanajeshi mstaafu wa jeshi la Marekani ambaye alikuwa kwenye kikosi maalumu cha anga, ardhi na maji (U.S NAVY SEAL), David Goggins, ameielezea kwenye kitabu chake cha CAN’T HURT ME kama kanuni ya asilimia 40 (40% RULE). Anasema pale unapokuwa unafanya kitu na kujiona umeshachoka au huwezi kuendelea tena, siyo kwamba umefikia mwisho wa uwezo wako, bali umefikia kikomo ambacho mwili wako umejiwekea, ambacho ni asilimia 40 ya uwezo wako. Hivyo kama hutakubaliana na mwili wako na kuendelea, kuna uwezo mkubwa zaidi ambao bado upo ndani yako, na hivyo utaweza kufanya makubwa zaidi.

40%

David ambaye alitokea mazingira magumu sana, kukua katika umasikini na kutokuwa na uwezo mzuri shuleni, aliweza kufikia ngazi za juu za jeshi na hata kuweza kukimbia mashindani ya mbio ndefu, zaidi ya maili mia moja kwa siku moja. Aliweza yote haya siyo kwa sababu alikuwa na kipaji kikubwa au bahati, bali kwa sababu alikuwa tayari kujisukuma hata pale ambapo alikuwa amechoka, kuumia na kukata tamaa kabisa. Kuna wakati ilimbidi aendelee na mbio huku akiwa ameshavunjika mifupa ya miguuni, kitu ambacho kilimpa maumivu makali sana.

Kwenye makala hii ya leo tunakwenda kujifunza jinsi ya kutambua na kuvuka kidhibiti mwendo kilichopo ndani yetu, ambapo tutaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu.

Kidhibiti mwendo kilichopo ndani yetu.

Kama tulivyoanza na mfano wa gari, magari huwa yanawekewa kidhibiti mwendo ambacho kuwa kinazuia uingiaji wa hewa na mafuta kwenye injini ili kuzuia mafuta mengi yasichomwe na kutoa nguvu kubwa kwa gari hilo, hivyo kuwa na ukomo wa mwendokasi.

Kidhibiti mwendo kwenye miili yetu kipo kwenye akili zetu. Kimejichimbia ndani ya utambulisho wetu, kwa jinsi tunavyojijua na kujichukulia. Kwa kudhibiti mwendo hiki cha akili, tunajiambia nini tunaweza kufanya na nini hatuwezi, pia tumejiwekea ukomo ambao tunaona hatuwezi kuuvuka.

Kidhibiti mwendo tulichonacho huwa kinatoa mrejesho kwa njia ya maumivu na uchovu na pia kinatumia hofu na kutokujiamini kama viashiria kwamba mtu umefika mwisho wa uwezo wako. Pale unapofanya kitu unafika hatua ambayo unajiona umechoka na hapo unapata maumivu makali, na unapoendelea kufanya unaanza kupata hofu kwamba utajiumiza na pia kukosa kujiamini kwa kuona ukiendelea zaidi utaharibu. Hapa ni kidhibiti mwendo kinakuzuia usiendelee zaidi, hapo unakuwa umefika kwenye asilimia 40 ya uwezo wako, bado una asilimia 60 hujaigusa kabisa.

Kwa bahati mbaya sana watu wengi wamekuwa wanaishia kwenye asilimia hiyo 40, pale uchovu na maumivu yanapowajia, wanaona wameshafanya kila kilicho ndani ya uwezo wao na hivyo hawawezi kuendelea tena. Lakini ukweli ni kwamba mtu anakuwa hajafika mwisho wa uwezo wake, bado anakuwa na uwezo mkubwa ambao haujaguswa kabisa, kama tu atakuwa tayari kujisukuma zaidi ya alivyozoea.

Jinsi ya kuvuka kidhibiti mwendo kwenye miili yetu.

Ili kuweza kuvuka kidhibiti mwendo kwenye miili yetu na kuweza kufanya makubwa zaidi tunapaswa kubadili kabisa mtazamo wetu na utambulisho wetu. Tunapaswa kufikiri tofauti na tulivyozoea kufikiri na kujiona tofauti na tulivyozoea kujiona.

Achana kabisa na hadithi na mazoea yoyote uliyonayo kuhusu nini unaweza kufanya na nini huwezi na upi mwisho wa uwezo wako. Anza kuamini kwamba unaweza kufanya chochote unachotaka kufanya na unaweza kufanya zaidi ya ulivyozoea kufanya.

Unapofanya kitu na kuanza kupata uchovu na maumivu, huku akili yako ikikuambia umefika mwisho, jua hapo umefika asilimia 40 ya uwezo wako. Hivyo usiishie hapo, badala yake endelea kujisukuma, endelea kuweka juhudi zaidi huku ukiyapuuza maumivu na uchovu. Utashangaa maumivu na uchovu vinapotea vyenyewe na nguvu zaidi inazaliwa ndani yako. Kwa nguvu hii mpya unaweza kwenda mpaka asilimia 60 ya uwezo wako, na ukiendelea kujisukuma zaidi unaweza kufika mpaka asilimia 80. Sasa hebu fikiria kama umezoea kuishia asilimia 40, ukaanza kufikia asilimia 80, hutabaki hapo ulipo sasa, utaweza kufanya mara mbili ya unavyofanya sasa na hivyo kupiga hatua mara mbili ya ulivyopiga sasa.

Kwa kuvuka kidhibiti mwendo cha akili yako unakuwa umeifungua akili yako na kutumia uwezo mkubwa sana ambao upo ndani ya mwili wako na kuweza kufikia viwango vya juu kabisa vya ufanisi kwenye chochote unachofanya.

SOMA; Imani Saba (7) Potofu Zinazokuzuia Usiwe Tajiri Kwenye Maisha Yako Na Jinsi Ya Kuzivuka.

Jinsi ya kutumia kanuni ya asilimia 40 kwenye maeneo mbalimbali ya maisha.

Kanuni hii imekuwa inatumika zaidi kwenye michezo na mazoezi ya viungo, mfano riadha. Pale mtu anapokuwa amechoka na kuona hawezi kuendelea tena, anapopuuza uchovu na maumivu hayo anapata nguvu mpya ya kuendelea na hata kuweza kushinda mbio anazoshiriki. Kila mwanamichezo kuna wakati akiwa mchezoni anafikia asilimia 40 ya uwezo wake na akili yake inamshawishi kuacha, ni wale wanaojisukuma zaidi ndiyo wanaoshinda michezo wanayoshiriki.

Lakini pia unaweza kutumia kanuni hii ya asilimia 40 kwenye kila eneo la maisha yako. Kwa sababu kwenye maisha hakuna kitu kinachokwenda kama tunavyopanga, huwa tunakutana na changamoto na vikwazo vinavyotushawishi kuacha au kukata tamaa. Tunapofika kwenye hali kama hizi tunapaswa kujikumbusha kwamba tumetumia asilimia 40, bado tuna asilimia 60 ya nguvu ndani yetu ambayo tukiitumia tutavuka chochote kinachotuzuia.

Kwa chochote unachofanya, pale unapofikiri umefikia ukomo, pale maumivu na uchovu vinakuambua huwezi kuendelea tena, nenda kwa asilimia 5 zaidi. Usikubali kuachia pale ambapo maumivu yanaanza, badala yake ongeza asilimia 5 zaidi ndiyo uache. Ni kweli maumivu yatakuwa makubwa zaidi, lakini akili yako itakomaa na kuyazoea, wakati mwingine hutaanza kupata maumivu kwa kufikia kiwango kilichokupa maumivu leo, badala yake utaanza kusikia maumivu baada ya kuzidi ile asilimia 5 uliyoongeza. Kwa kuendelea hivi utajikuta unaweza kufanya zaidi na maumivu kutokukusumbua.

Kama unafanya kazi au biashara, usiache pale unapokuwa umepata maumivu au uchovu, badala yake endelea kwa asilimia 5 zaidi ndiyo uache. Hata kama maumivu ni makali kiasi gani, hata kama uchovu ni mkubwa kiasi gani, jiambie utaendelea kwa kiwango kidogo tu kisha utaacha, na hapo akili yako itajifunza kupuuza maumivu na uchovu na kukupa nguvu ya kuendelea zaidi. Hapo unakuwa umeondoa kile kidhibiti mwendo cha kiakili.

Kadhalika kama unasoma au unajisomea, huwa unafika mahali na akili inakuambia huelewi tena, kwamba umechoka na huwezi tena kuendelea. Hapo ndipo unapopaswa kujipa wajibu wa kuendelea kwa asilimia 5 zaidi. Kwa njia hii, akili yako itasahau uchovu na kutokuelewa na itakubali usomaji wako na kuelewa zaidi.

Na katika michezo na ufanyaji mazoezi ndipo kanuni hii inaweza kukusaidia zaidi. Mchezaji mmoja maarufu sana aliwahi kuulizwa katika mazoezi anakimbia mara ngapi? Akajibu hajui, watu wakamshangaa, na akaendelea kusema huwa naanza kuhesabu pale ninaposikia maumivu. Hebu ona jinsi hili lilivyo na nguvu, mtu anachagua kukimbia kwanza bila ya kuhesabu umbali anaokimbia, na anapoanza kupata maumivu na uchovu ndipo anapoanza kuhesabu. Hii ni njia bora sana ya kuvuka kidhibiti mwendo tulichojiwekea kwenye akili zetu.

Anza sasa kuongeza asilimia 5 zaidi kila unapojiona umechoka na huwezi kuendelea tena. Uchovu, maumivu na hata hofu siyo uhalisia, bali ni vitu vimetengenezwa na akili zetu. Miili yetu ina uwezo wa kufanya makubwa zaidi ya mtu ulivyozoea kufanya, laini imewekewa ukomo na akili zetu. Kama mtu utaweza kuondoa ukomo huu uliowekwa na akili, hakuna kitakachoweza kukushinda kwenye maisha yako.

Nenda katumia kanuni hii ya asilimia 40 na kuongeza asilimia 5 kila mara unapofikia uchovu na maumivu, na utaweza kufanikiwa zaidi ya ulivyozoea.

Kitabu cha CAN’T HURT ME ndiyo kitabu nitakachokuchambulia kwa kina juma hili la 13, ndani yake kuna mambo mengi sana ya kujifunza, jinsi ambavyo tunaweza kuzifanya akili zetu kuwa imara na kuweza kukabiliana na ugumu au mateso yoyote. Tutaona jinsi ambavyo, kuumia, uchovu na hofu ni vitu vinavyotengenezwa na akili zetu, na kama tukiweza kuzitawala akili zetu, hakuna chochote kinachoweza kutuumiza.

Hakikisha upo kwenye channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA ili usikose uchambuzi wa kina wa kitabu hiki pamoja na mafunzo ya ziada ya namna unavyoweza kuwa imara zaidi kiakili na kitu chochote kisikuumize au kukuyumbisha kwenye maisha. Kujiunga na channel hii tuma ujumbe TANO ZA JUMA kwa kutumia app ya TELEGRAM MESSENGER kwenda namba 0717396253 na utaunganishwa kwenye channe. Karibu sana.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge