Changamoto ya maisha ni hii, unapokuwa hujafanikiwa, hakuna anayehangaika na wewe, utakutana na changamoto chache sana, maisha yatakuwa yanaenda tu kawaida, hakuna migogoro mingi na wengine.

Lakini unapoanza kufanikiwa, watu wanaanza kukufuatilia zaidi, na lawama nyingi zitakuja kwako kutokana na maisha ambayo mafanikio yako yatakulazimu uyaishi.

Kwa mfano kadiri unavyofanikiwa ndiyo unavyokuwa na muda mchache wa kukaa na watu wengi ambao ulikuwa umezoea kukaa nao hapo awali. Sasa kwa kuwa mafanikio yanakutaka utumie muda wako kwenye shughuli muhimu, watu hao watasema tangu umefanikiwa unawatenga au huwajali tena.

Kwa kuambiwa hivyo, wengi hujisikia vibaya, hivyo kulazimika kutenga muda wa kuwa na kila anayetaka muda wao, na hili linaathiri sana mafanikio yao zaidi.

Kama unataka kufanikiwa zaidi, lazima uwe mbinafsi wa vitu viwili muhimu sana, ambavyo unavyo kwa ukomo.

Vitu hivyo ni muda wako na nguvu zako.

Kwa muda una masaa 24 pekee kwa siku, huna zaidi ya hapo, hivyo kabla hujatumia muda wako lazima ujiulize unachokwenda kufanya kinachangiaje kwenye maisha yako na mafanikio yako. Usitake tu kufanya kitu ili kuwaridhisha wengine, kumbuka muda unaotumia kuwaridhisha wengine ni muda unaojichelewesha kufanikiwa zaidi.

Kwa upande wa nguvu, mwili wako ni kama betri ya simu, unapoamka inakuwa imejaa chaji, kila unachofanya kwenye siku yako kinapunguza chaji hiyo. Sasa jiulize kila unachotaka kufanya kwenye siku yako, ambacho kinatumia nguvu zako zinazoendelea kupungua, kina umuhimu kwako? Je kinachangia wewe kuwa na maisha bora na kufanikiwa zaidi?

Hapana ni neno ambalo litakusaidia sana kwenye kulinda vitu hivi viwili adimu ulivyonayo, usiogope kutumia neno hili kadiri inavyohitajika. Sema hapana kwa vitu au watu wanaotaka muda na nguvu zako, lakini hakuna mchango wowote kwenye maisha yako kuwa bora na hata kufanikiwa zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha