“Your mind will take the shape of what you frequently hold in thought, for the human spirit is colored by such impressions.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 5.16

Ni siku mpya ya mwezi mpya katika mwaka wetu huu mzuri wa mafanikio.
Tushukuru kwa nafasi hii nyingine ya uhai na tukaitendee vyema ili tuweze kufanya makubwa sana siku hii ya leo.
Tukaumiliki vizuri muda wetu na kutumia kwa usahihi nguvu zetu ili tuweze kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari RANGI YA FIKRA ZAKO…
Akili yako, inachukua sura ya mawazo unayoyaruhusu kukutawala kwa muda mrefu. Na maisha yako yatakuwa matokeo ya fikra hizo.

Rangi ya fikra zako inaishia kuwa ndiyo rangi ya maisha yako.
Kuwa na fikra hasi muda wote na maisha yako yatakuwa hasi, kila kinachotokea itakiona kibaya kwako, hata kama kina uzuri ndani yake.
Kuwa na fikra za kushindwa na kwa kila unachojaribu utashindwa.

Akilk yako haiwezi kuelewa tofauti ya fikra zako na uhalisia, inachukulia fikra ulizonazo kwa muda mrefu kama ndiyo uhalisia wako, na hivyo itapambana kuhakikisha unapata kile unachofikiri kwa muda mrefu.

Mtu anaweza kuwa anaendesha gari eneo la wazi kabisa, ambapo kuna nguzo mti mmoja pekee, lakini anaends kugonga mti huo. Ni kwa sababu akili yake imekuwa inafikiria kugonga mti huo, na siku nafasi inapatikana anaugonga.

Hakuna kinachotokea kwenye maisha yako ambacho hujapata taswira yake ndani ya fikra zako.
Kila kinachotokea unakuwa umekifikiria kwanza, na unakuwa umekijengea picha kabisa, matokeo ya nje ni kazi ya ndani.

Hivyo kama unataka kubadili rangi ya maisha yako, kama unataka kubadili matokeo ya nje, anza kwa kubadili fikra zilizopo ndani ya akili yako.
Tawaliwa na fikra za yale mazuri unayotaka na akili itakuletea hayo.
Ila usisahau kuweka kazi, kwa kuwa hakuna kitakachojileta chenyewe kwako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutawaliwa na fikra nzuri na chanya ili kuwa na maisha bora.
#TawalaFikraZako, #FikiriChanya, #OnaUnachotakaNaUtakipata

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha