Kila mmoja wetu ana kitu cha tofauti ambacho kipo ndani yake, ambacho hakuna mtu mwingine hapa duniani ambaye anacho.
Kila mmoja wetu ana moto mkubwa unaowaka ndani yake, ambao akiuachilia, utatoa nuru kubwa sana kwa dunia.
Lakini watu wengi wanatumia nguvu kubwa kuzima moto huo au kuuzuia usionekane, kwa sababu hawataki kusumbuka katika kutoa nuru hiyo kwa dunia.
Dunia imefanya kazi kubwa ya kutaka kutufananisha na wengine, taasisi za kijamii zinanufaika sana pale watu wote wanapokuwa wanafikiria sawa, kwa sababu inakuwa rahisi kuwatawala, kuwatumia na hata kuwarubuni.
Tambua nguvu hii kubwa inayokulazimisha uwe kawaida, inayokutana uwe sawa na wengine na usifanye kitu cha tofauti. Nguvu hiyo ndiyo inakufanya ufiche moto uliopo ndani yako, ambao badala ya kuleta nuru kwako na kwa wengine, unakuunguza ndani kwa ndani na hivyo unaumia zaidi.
Kila mmoja wetu anapaswa kuwa nuru kwa wengine hapa duniani, kwa kuachilia moto uliopo ndani yake.
Moto huu unaweza kuwa kwenye kazi unayofanya au biashara, lakini pia unaweza kuwa kwenye kitu cha ziada, nje ya kazi na biashara, ambacho unapenda kufanya na kinakupa hali kubwa ya kuridhika ndani yako.
Muhimu ni kutambua moto wako uko eneo gani na kuuachilia. Kumbuka hata ukiuzuia moto huu ndani yako hautazima, badala yake utakuunguza wewe mwenyewe badala ya kuwa nuru kwa wengine. Achilia moto huo uwe nuru kwa wengi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,