“There are two things that must be rooted out in human beings—arrogant opinion and mistrust. Arrogant opinion expects that there is nothing further needed, and mistrust assumes that under the torrent of circumstance there can be no happiness.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 3.14.8
Ni siku nyingine mpya na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi hii nzuri sana kwenye maisha yetu, nafasi ambayo siyo kila mtu ameipata.
Hivyo ni bahati ya kipekee kwetu na njia pekee ya kushukuru na kulipa bahati hii ni kwenda kuitumia siku hii vizuri, kwa kufanya yale muhimu na kutokupoteza muda au nguvu kwa yasiyo muhimu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUWA TAYARI KUBADILI MAONI YAKO….
Maoni siyo sheria, bali ni muafaka tunaofikia kutokana na uelewa na uzoefu ambao tunao kwa wakati tunafikia maoni hayo.
Hii ina maana kwamba, kadiri tunavyopata uelewa zaidi, kupitia maarifa na taarifa, na kadiri uzoefu wetu unavyokua kupitia matokeo tunayopata, tunapaswa kuyaboresha maoni yetu zaidi.
Lakini sivyo wengi wanavyoendesha maisha hao,
Wengi wanaendesha maisha kwa maoni waliyofikia miaka mingi iliyopita na hawataki kubadilika tena.
Wengi wanajikwamisha wao wenyewe kwa kutegemea maoni waliyokuwa nayo huko nyuma, japo kwa sasa hayana nafasi tena.
Kuwa tayari kubadili maoni yako kadiri unavyojifunza zaidi na kupata uzoefu zaidi.
Epuka makosa mawili ambayo wengi wanafanya,
Moja, kiburi cha maoni, kwa kuona hakuna kipya mtu anaweza kujifunza na hivyo kuendelea na maoni aliyokuwa nayo huko nyuma.
Mbili, kutokujiamini kwamba unaweza kuwa na maoni bora zaidi kulingana na maarifa na uzoefu unaopata.
Usikubali kuwa kikwazo kwako mwenyewe kwa kung’ang’ana na maoni ya nyuma, unapopata maarifa na uzoefu mpya, badili maoni yako.
Na achana na misimamo ya kijinga, ambayo inawapoteza wengi, misimamo ya kuendelea na maoni ambayo yameshapitwa na wakati.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kubadili maoni kulingana na maarifa na uzoefu mpya unaopata.
#MaoniSiSheria, #KunaMengiUsiyojua, #AchaMisimamoYaKijinga
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha