Ukirusha kitu juu, kitarudi chini. Ukipanda juu ya jengo refu au mti mrefu na ukajiachia, utadondoka chini, na huenda ukaumia sana.

Kinachofanya vitu vianguke chini ni nguvu ya mvutano ambayo ipo ndani ya dunia. Nguvu hii inatuzuia sisi binadamu tusiweze kupaa na hata kufanya vitu vikae karibu na dunia badala ya kuelea angani.

Nguvu hii ya mvutano ya dunia ina vikwazo vingi sana kwetu kama sisi binadamu, lakini hujawahi kusikia watu wakilalamika kwamba nguvu hiyo imewakwamisha kufanikiwa. Ambacho tunafanya ni kutumia nguvu hiyo kwa manufaa. Kwa kuwa sisi binafsi hatuwezi kupaa angani, basi tumetengeneza ndege zinazotuwezesha kupaa. Zote hizi zinafanya kazi kwa kutumia nguvu hii ya mvutano ya dunia.

Kadhalika satelaiti zinazorusha mawimbi mbalimbali, zinaweza kuelea angani kwa kutumia nguvu hii ya mvutano ya dunia.

Ninachotaka kukuambia rafiki yangu ni hiki, kila kitu tunachokutana nacho kwenye maisha, kina pande mbili, kina upande mzuri na upande mbaya, kina manufaa na hasara pia.

Hivyo wajibu wetu siyo kujaribu upande mbaya wa kitu, maana hatuwezi kufanikiwa kwenye hilo. Badala yake wajibu wetu ni kutumia upande mzuri wa kitu, na tutanufaika sana.

Kama ambavyo hatujaribu kuibadili nguvu ya mvutano ya dunia, bali tunaitumia, kadhalika tunapaswa kufanya hivyo kwenye maeneo mengine ya maisha yetu.

Mfano kwenye maisha tunakutana na watu mbalimbali, na kila mtu ana upande wake mzuri na upande wake mbaya. Mahusiano mengi ya watu yanapata changamoto kwa sababu kila mtu anajaribu kubadili upande mbaya wa mtu, badala ya kutumia upande wake mzuri.

Kadhalika kwenye kazi, biashara na kila tunachokutana nacho kwenye maisha, tunapaswa kutumia upande chanya na kuachana na upande hasi. Usipoteze muda na nguvu zako kujaribu kubadili vitu ambavyo vipi nje ya uwezo wako, badala yake angalia uzuri unaoweza kuutumia kwenye kila unachokutana nacho.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha