“Don’t act grudgingly, selfishly, without due diligence, or to be a contrarian. Don’t overdress your thought in fine language. Don’t be a person of too many words and too many deeds. . . . Be cheerful, not wanting outside help or the relief others might bring. A person needs to stand on their own, not be propped up.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 3.5
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KIDOGO INATOSHA…
Tumekuwa tunafikiri ili maisha yetu yakamilike na kuwa bora basi tunahitaji vitu vingi sana.
Lakini huo siyo ukweli, maisha bora na yaliyokamilika ni yale ambayo yanategemea vitu vichache.
Kwa kuwa mahitaji yetu ya msingi ni machache na yapo ndani ya uwezo wa kila mmoja wetu.
Lakini tunapokazana na kupata zaidi, ndipo tunapoyafanya maisha yetu kuwa magumu.
Usiwe mtu wa maneno mengi, ongea pale tu ambapo ni muhimu kufanya hivyo, na kama neno haliongezi thamani yoyote usilotoe.
Usiwe mtu wa mambo mengi, fanya yale tu ambayo ni muhimu sana na yenye maana kwako na kwa wengine.
Kama kila mmoja wetu angeelewa hili, kama kila mtu angeacha kukimbiza zaidi na zaidi, dunia ingekuwa sehemu bora sana kwa maisha ya kila mtu.
Lakini hatuwezi kutulia, hatujui nini hasa tunataka na maisha yetu, hivyo tukiona mwingine ana kitu, na sisi tunakitaka pia. Na hili ndiyo linapelekea kuhangaika na mambo mengi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuhangaika na machacje sana, yenye maana na yaliyo muhimu, na mengine kuachana nayo.
#KidogoNiZaidi, #JuaUnachotaka, #WekaVipaumbele
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha