Watu ambao hawajafanikiwa wana tabia moja.
Tabia hiyo ni kuyafanya mafanikio kuonekana kitu kibaya na wale waliofanikiwa kuonekana watu wabaya.
Wale ambao hawajapata kile wanachotaka, wana tabia ya kuwadharau wale ambao wamepata, kwa kujiwekea mazingira ya kuonesha kwamba wale waliopata wanachotaka hawajapata kwa usahihi.
Kuna wakati wataonesha kwamba wamepata kwa bahati, wakati mwingine wataonesha kwamba wamepata kwa njia zisizo halali. Hata wakati mwingine wataonesha kwamba wale waliopata hawajali ambao hawajapata.
Hapo sasa wao watajionesha kuwa wanastahili zaidi, ni wema sana kuliko wengine na wakati mwingine watajionesha kama watu wenye hatia, watu wanaoonewa na waliofanikiwa.
Unapoona watu uliowazidi kwa mafanikio wanakutengenezea mazingira ya aina hii wala lisikuumize, elewa ni njia yao ya kujifariji kwa kutokufanikiwa. Hayo wanayofanya wale ambao hawajafanikiwa, kwa kuona mafanikio yako yasikufanye ukataka kurudi nyuma.
Usipojua hili na kulisimamia, watu watayatumia mafanikio yako kukuadhibu, watakufanya ujisikie vibaya kwa mafanikio yako.
Kwa mfano labda mna kikao na watu wa karibu, ndugu na jamaa, na wewe kwa sababu fulani ukashindwa kufika au ukachelewa kufika. Kuna baadhi ya watu watasema, huyu anaringa, kwa kuwa ana fedha kuliko sisi anaona yeye hana muda na kikao, au anatufanya sisi tumsubiri mpaka afike. Wakati huo kunaweza kuwa na wengine wamechelewa au hawakufika, lakini hawatachukuliwa kama wewe. Elewa hivyo ndivyo watu walivyo na lisikuumize hata kidogo, wala usijaribu kujieleza, maana kadiri utakavyojieleza ndivyo watakavyozidi kujipa sababu za kuyadharau mafanikio yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,