“When you let your attention slide for a bit, don’t think you will get back a grip on it whenever you wish—instead, bear in mind that because of today’s mistake everything that follows will be necessarily worse. . . . Is it possible to be free from error? Not by any means, but it is possible to be a person always stretching to avoid error. For we must be content to at least escape a few mistakes by never letting our attention slide.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 4.12.1; 19

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USIPOTEZE UMAKINI WAKO…
Kama kuna kitu kimoja muhimu sana unachomiliki, ambacho kina nguvu ya kukufikisha kule unakotaka kufika basi ni umakini wako. Uwezo wako wa kuweka fikra zako kwenye yale muhimu na kuepuka kelele na kila aina ya usumbufu.

Umakini umekuwa adimu na ghali sana katika zama tunazoishi.
Kila mtu anauwinda umakini wako,
Kuanzia kwenye mitandao ya kijamii, watu wanaweka mambo ambayo yanateka umakini wako na kuyafuatilia.
Ukienda kwenye habari ndiyo kabisa, ni kama jeshi limejipanga kuteka umakini wako, wanasema mbwa kumng’ata mtu siyo habari, bali mtu kumng’ata mbwa ni habari ya kusisimua, hivyo wanakuandalia habari za kusisimua ili kuteka umakini wako.
Hapo bado hujaja kwa wale wanaokuzunguka, ambao wanakuletea habari na maneno maneno yanayohusu wengine ili tu kuteka umakini wako.

Kama kuna kitu kimoja unapaswa kukilinda sana kwenye maisha yako basi ni umakini wako.
Kuweza kupeleka fikra zako kwenye yale muhimu na kuachana na usumbufu na kelele zinazoletwa kwako kila sekunde.

Na ubaya ni kwamba, ukiruhusu umakini wako upotee hata kwa sekunde moja tu, huwezi kuurudisha tena.
Mara ngapi umejiambia unatembelea mtandao au kufuatilia habari kwa muda mfupi tu, unakuja kustuka muda umeenda na bado umenasa kwenye mtandao au habari unazofuatilia?
Kila ukitaka kutoka unaona kitu kingine kizuri zaidi, ukijiambia naangalia hii ya mwisho inakuja nyingine ya kusisimua zaidi. Unajikuta unazidi kuchimba na kuchimba, na mwisho wa siku unaondoka na nini?

Linda sana umakini wako, usiupoteze hata kwa sekunde moja, kama kitu siyo muhimu usijiulize hata mara mbili, usikipe hata sekunde moja. Weka fikra zako kwenye yale yaliyo muhimu pekee na utakuwa mtu wa kipekee sana kwenye zama hizi ambazo karibu kila mtu amevurugwa na kelele na usumbufu.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kulinda umakini wako na kutokuruhusu yasiyo muhimu kupata nafasi kwenye fikra zako.
#LindaUmakiniWako, #TawalaFikraZako, #HangaikaNaYaliyoMuhimu

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha