“You have been formed of three parts—body, breath, and mind. Of these, the first two are yours insofar as they are only in your care. The third alone is truly yours.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 12.3

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari AKILI YAKO NDIYO KITU PEKEE UNACHOMILIKI KWA ASILIMIA 100…
Wewe umegawanyika katika maeneo matatu, mwili, pumzi na akili.
Katika maeneo haya, mawili ya kwanza unayamiliki kwa sehemu tu. Lakini eneo la tatu, yaani akili yako, ndiyo kitu pekee unachokimiliki kwa asilimia 100.

Huna umiliki mkubwa kwenye mwili wako, unaweza kupata ajali ambayo hukutegemea na huwezi kuizuia. Unaweza kupatwa na ugonjwa ambao huna namna ya kuuzuia au kuuondoa ukishaingia kwenye mwili wako. Hivyo mwili wako unaumiliki kwa kiasi tu, lakini sehemu kubwa ipo nje ya uwezo wako.

Kadhalika kwenye pumzi, pamoja na umuhimu mkubwa wa pumzi kwenye maisha yako, bado huimiliki kwa asilimia 100. Unaweza kukata pumzi muda wowote bila ya kuwa na cha kufanya. Unaweza kubanwa pumzi na ukateseka sana kupumua. Pia unaweza kuwa na ugonjwa unaohusisha mfumo wa pumzi na ukawa mzigo mkubwa kwako. Una imiliki kiasi tu kwenye pumzi yako.

Lakini kwa akili mambo ni tofauti, una umiliki wa asilimia 100 wa akili yako, hakuna chochote kinachotokea kwenye akili yako ambacho huwezi kukidhibiti au kukizuia.
Kila fikra inayoingia kwenye akili yako, umeitengeneza mwenyewe au kuiruhusu mwenyewe.
Hata kama umefungwa gerezani, bado akili yako ipo huru kufikiri chochote unachotaka.
Tambua uhuru huu mkubwa ulionao kwenye akili yako na utumie kwa usahihi, kwa kuhakikisha unamiliki fikra zako na kuhangaika na yale yenye manufaa pekee.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kumiliki na kutumia vizuri akili yako.
#AkiliNiMali, #DhibitiFikraZako, #HangaikaNaYanayokuhusu

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha