Hitaji kuu la kila mtu ni furaha, hili ni hitaji la ndani kabisa la kila binadamu.
Kila tunachofanya tunasukumwa na vitu viwili, kupata kile tunachotaka, ambacho ni furaha au kuepuka tusichotaka ambacho ni maumivu.
Hakuna mtu mwenye akili timamu, anayefanya jambo la kumuumiza yeye mwenyewe kwa makusudi. Hata pale watu wanapofanya mambo ambayo tukiangalia kwa nje tunaona kabisa kwamba wamekosea, ndani yao wana sababu nzuri sana za kufanya hivyo, ambapo wanaamini watakuwa vizuri zaidi kuliko kutokufanya.
Sasa hili unalitumiaje katika kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako?
Unalitumia kwa kuhakikisha kazi yoyote unayofanya, bidhaa au huduma yoyote unayouza, inachangia kumfanya mtu kuwa na furaha. Na hilo lioneshe wazi kwa wateja unaowahudumia.
Fanya lengo lako kuu kuwa ni kuuza furaha, kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi, kuwapa kile kinachowawezesha kuyafanya maisha yao kuwa bora, kupata wanachotaka au kukwepa wanachoepuka.
Kama unafundisha basi wape watu maarifa ambayo yatawawezesha kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi. Kama unaburudisha basi wape burudani utakayowafanya wazisahau shida zao, japo kwa muda. Kama unatubu basi wape watu matibabu bora yanayowaondolea maumivu waliyonayo.
Chochote unachofanya, utafanikiwa sana kama utapeleka mtazamo wako kwenye kuwafanya wengine kuwa na furaha zaidi kuliko kujiangalia wewe mwenyewe pekee.
Kama hujajua wapi pa kuanzia, anza na wazo linaloleta manufaa kwa wengine wafikie wengi kupitia wazo hilo na wewe utapata manufaa makubwa sana.
Kazi yako kubwa iwe kuwahudumia wengine, na dunia itakuhudumia wewe. Wape watu matumaini, wape watu sababu ya kutabasamu na yafanye maisha yao kuwa bora zaidi. Ni kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako kwa chochote utakachochagua kufanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,