“Tantalus: The highest power is—
Thyestes: No power, if you desire nothing.”
—SENECA, THYESTES, 440

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari MAHITAJI YAKO NDIYO YANAKUFANYA KUWA MTUMWA…
Zama tunazoishi sasa ni zama ambazo utumwa wa kulazimishwa umeshaondolewa kabisa.
Ila umebaki utumwa wa kujitakia mwenyewe.
Na utumwa huu unatokana na mahitaji ambayo mtu unayo.
Unakaa kwenye kazi ambayo huipendi na kulazimika kuwa chininya bosi ambaye hakujali kwa sababu tu unataka fedha.
Unaingia kwenye madeni, ili kununua kitu fulani kwa kuwa wengine wanacho au wanategemea uwe nacho.
Unalazimika kufanya vitu ambavyo ndani yako hutaki kufanya, ila unafanya ili wengine wakukubali.

Kama kuna chochote ambacho unafanya kwenye maisha yako, ambacho ndani yako hakuna msukumo wa kukifanya, basi jua umeshachagua kuwa mtumwa.
Kama mahitaji yako yanakupeleka kufanya vitu ambavyo usingependa kabisa kufanya au hufurahii kufanya, basi umeshapoteza uhuru wako.

Hakuna mtu yeyote anayeweza kuwa juu yako na kukutawala kama utakuwa huhitaji chochote kutoka kwake. Tunalazimika kuwa watumwa wa wengine kwa sababu ya mahitaji yetu.
Hivyo ili kuwa na uhuru wa maisha yako, punguza kabisa mahitaji yako na usitegemee mahitaji yako kutoka kwa mtu mmoja.
Mfano ili kuwa huru kifedha, usitegemee kipato chako kutoka kwenye chanzo kimoja kama ajira pekee.

Chagua kuwa huru, chagua kuwa nw mahitaji machache sana na ya msingi kwako, ambayo yapo ndani yako.
Na epuka kabisa kutaka kuiga maisha ya wengine au kutaka kuonekana au kukubalika na wengine.
Uhuru kamili ni kuchagua kuyaishi maisha yako na kuwaacha wengine waishi maisha yao.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuondokana na utumwa kwa kuondokana na mahitaji yasiyo ya lazima.
#MahitajiNiUtumwa, #UhuruNiKuchagua, #PunguzaMahitajiYako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha