Maisha ni kitu ambacho kila mtu anakipata mara moja, baada ya miaka michache yanayeyuka na hakuna mwenye uhakika nini kinatokea baada ya maisha haya kuwa yameisha. Dini na falsafa zina nadharia tofauti, lakini kwa kuwa hakuna aliyewahi kwenda akarudi, tunabaki gizani kwamba nini kinatokea baada ya kuwa tumeondoka kwenye haya maisha.

Hivyo basi, kwa kuwa hatuna matarajio yoyote ya baada ya maisha haya, basi ni vyema kuyachukulia maisha tuliyonayo kama nafasi yetu pekee ya kuishi. Tunapaswa kuchukulia maisha haya kama kitu chenye thamani kubwa mno, ambacho hatuwezi kumudu kukipoteza. Kwa sababu ndiyo, maisha yako yana thamani kubwa mno kwako.

Lakini hivi sivyo wengi wanavyoishi maisha yao, wengi wanaishi maisha yao hovyo kama vile wana uhakika wa kupata mengine muda wowote. Watu wanapoteza muwa wa thamani wa maisha yao kufuatilia mambo ya kijinga na yasiyo na manufaa yoyote kwao. Watu wanafanya vitu ambavyo ni hatari sana kwa afya zao bila hata kufikiri mara mbili.

Na kibaya zaidi, watu wengi wapo tayari kuuza maisha yao kwa kitu ambacho hakina thamani kubwa. Fikiria watu ambao wamekwama kwenye kazi au biashara wasizopenda, lakini kwa kuwa wanataka kupata fedha, inawabidi wazifanye. Lakini kila siku hawana raha kabisa na maisha yao, wakifikiria kazi zao wanapatwa na simanzi kubwa, lakini wameshayauza maisha yao na hawaoni namna ya kujinasua.

Na hili lipo sana kwenye kazi, ambapo mtu anaingia kwenye ajira, ambayo haipendi, lakini anajiambia ni sehemu ya kuanzia. Lakini anapoingia kwenye ajira hiyo, anayauza maisha yake na kujiweka kwenye gereza kubwa, hasa la mikopo ambalo linamzuia asiweze kutoka kwenye gereza hilo.

Rafiki, ninachotaka kukuambia hapa ni kimoja, maisha yako yana thamani kubwa sana, ndiyo kitu pekee ambacho unakipata mara moja, yatunze, yalinde na yathamini sana. Usiyapoteze kwa kufanya vitu visivyo na msingi, na muhimu zaidi, usiyauze kwa kufanya chochote usichopenda kufanya ila tu unataka kupata fedha.

Rahisisha maisha yako, acha kuiga wengine, acha kutaka kuonekana na wewe upo na chagua kufanya kile unachopenda kufanya na kwa hakika utakuwa na maisha bora yenye furaha na mafanikio makubwa. Ukishakuwa na maisha ya aina hii, hutahofia hata kifo, maana unajua umeishi maisha yako. Wengi wanahofia kifo kwa sababu hawajayaishi maisha yao.

Usiuze maisha yako, ndiyo kitu pekee ambacho huwezi kukipima kwa thamani ya fedha, ishi maisha yako kwa kuzingatia yale muhimu zaidi na kufanya unachopenda kufanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha