“Where is Good? In our reasoned choices. Where is Evil? In our reasoned choices. Where is that which is neither Good nor Evil? In the things outside of our own reasoned choice.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 2.16.1

Hongera sana rafiki yangu mpendwa kwa nafasi hii nyingine ambayo umeipata leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwako, nafasi ambayo siyo kila mtu ameipata.
Hivyo beba nafasi hii kama zawadi na usipoteze muda wako kwa chochote kisicho muhimu kwako.
Nenda kaiishi siku hii ya leo kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA huku ukiongozwa na AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA na utaweza kuwa na siku bora sana ya leo.

Asubuhi ya leo tutafakari UZURI NA UBAYA UPO KWENYE MAAMUZI YAKO…
Uzuri na ubaya haupo sehemu nyingine yoyote bali kwenye fikra zako na maamuzi unayofanya.
Hakuna mtu anakufanya wewe uwe mzuri au mbaya, bali unakuwa mzuri au mbaya kwa fikra unazokuwa nazo na maamuzi unayofanya.

Hakuna kitu chochote cha nje yako ambacho kina nguvu ya kukufanya mtu mzuri au mbaya.
Bali uzuri na ubaya unaanzia ndani yako, kwa fikra zinazokutawala na maamuzi unayofanya pamoja na hatua unazokwenda kuchukua.

Hivyo sehemu pekee ya kuweka kazi kama unataka kuwa mtu mzuri ni kwenye fikra zako na maamuzi unayofanya.

Hakikisha unadhibiti fikra zako, kwa kuhakikisha ni fikra zako kweli na siyo za kulazimishiwa na watu wengine. Maana zama hizi watu wengi wanayengenezewa fikra na watu wengine kupitia habari na mitandao ya kijamii. Linda sana fikra zako zisichafuliwe na yeyote.

Pia hakikisha unafanya maamuzi sahihi, yanayotokana na fikra zako sahihi na siyo maamuzi ya hisia au kuiga wengine. Hakikisha unayo sababu unayoweza kuielezea kwa nini umeamua kitu fulani. Kama huwezi kuelezea kwa uhakika basi hayo siyo maamuzi yako mwenyewe, umeyafikia kwa hisia tu au umeyaiga kwa wengine.

Ukidhibiti kwa uhakika maeneo hayo mawili, fikra na maamuzi, utaweza kuwa mtu mzuri bila ya kujali wengine wanafanya nini au nini kinaendelea nje yako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kudhibiti fikra zako na kufanya maamuzi sahihi ili uwe mtu mzuri.
#DhibitiFikraZako, #FanyaMaamuziSahihi, #UzuriNaUbayaUpoKwenyeMaamuzi

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha