Mbuni anapokutana na tatizo ambalo hawezi kulikabili, huwa anafukia kichwa chake kwenye mchanga. Kama vile asipoliona tatizo basi litaondoka lenyewe.
Japokuwa sisi binadamu tuna uwezo mkubwa kuliko mbuni, lakini inapokuja kwenye matatizo makubwa, hatutofautiani sana na ndege hao.
Watu wengi wanapokutana na matatizo makubwa, huwa wanajaribu kuyakimbia au kujificha, wakiamini kufanya hivyo kutayaondoa matatizo hayo. Lakini kinachotokea ni matatizo hayo yanakuwa makubwa zaidi.
Angalia jinsi watu wengi wanavyogeukia vilevi wape wanapokuwa na matatizo mbalimbali. Tena wengine wanajisifu kabisa bora nilewe nisahau matatizo niliyonayo, lakini ulevi unapoisha, matatizo yanarudi pale pale. Na hapo mtu anahitaji kulewa tena, kitu ambacho kinatengeneza tatizo jipya la ulevi.
Kelele nyingi zinazotuzunguka sasa ni njia ya kujaribu kukimbia matatizo tuliyonayo. Na njia kubwa ni mitandao ya kijamii. Sasa hivi mtu akijisikia vibaya kidogo tu, hachukui hata muda kutafakari nini kinaendelea kwenye maisha yake, badala yake anakimbilia kutumia mitandao ya kijamii, kuangalia maisha ya wengine yakoje. Wengine huishia kuanika matatizo yao kwenye mitandao hiyo na hilo kuzalisha matatizo zaidi badala ya kutatua.
Rafiki, hakuna tatizo lolote linalokukabili litaondoka kwa wewe kujificha, kutoroka au kupuuza. Njia pekee ya kuondokana na matatizo uliyonayo ni kukabiliana nayo, kuyatatua.
Pia unapaswa kujua matatizo ni sehemu ya maisha, ukitatua tatizo moja kuna mengine yanakuja, hivyo kama utajijengea tabia ya kuyakimbia matatizo, hutakuwa na maisha kabisa. Kwa sababu kila wakati kuna kitu utakuwa unakikimbia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,