Hofu imekuwa kikwazo kwa wengi kupiga hatua kwenye maisha yao na kufanikiwa zaidi.

Japo wengi hawatakiri kwamba kinachowazuia ni hofu, lakini kwa hakika hofu ndiyo kikwazo kwa wengi, na hata kwako pia.

Fikiria vitu vyote vikubwa ambavyo umewahi kupanga kufanya na hukufanya, fikiria malengo yote makubwa ambayo umewahi kujiwekea na hukuchukua hatua. Unafikiri ni nini hasa kilikuzuia? Najua utataja sababu zote, lakini hutataja hofu.

Mfano umekuwa na lengo la kuanza biashara lakini huanzi, miaka inaenda biashara huanzi. Unaweza kujipa sababu nyingi utakavyo, kwamba huna mtaji, kwamba ushindani ni mkali, kwamba huna muda, kwamba hujapata wazo bora na sababu nyingine nyingi za kujifurahisha.

Lakini ukweli ni huu, kama umekuwa unapanga kuanza biashara lakini huanzi, kikubwa kinachokuzuia ni hofu. Unahofu ya kuwakabili watu wanaoweza kukupa mtaji wa kuanza. Una hofu kwamba ukianza unaweza kushindwa. Una hofu kwamba ukishindwa wengine watakucheka. Una hofu kwamba ukijitoa zaidi ili kukuza biashara yako basi utapoteza maisha yako ambayo umeshayazoea. Hii ndiyo sababu kuu, hofu, nyingine zote ni za kujiridhisha tu.

Hivyo baada ya kujua sababu kuu ni hofu, hatua ya kwanza katika kuikabili hofu na kutimiza malengo na mipango yetu ni kukiri kwamba tuna hofu na inatuzuia. Rafiki, huwezi kutatua tatizo ambalo hujalikubali. Hivyo ili kuivuka hofu, kwanza lazima ukubali kwamba una hofu. Halafu hapo sasa ndiyo unaweza kuchukua hatua sahihi.

Unapojiambia kinachokuzuia ni hofu, unakuwa na uhuru wa kuchukua hatua licha ya kuwa unakabiliwa na hofu hiyo. Ukishaona wazi kilichosimama kati yako na ndoto yako kubwa ni hofu, utaweza kuikabili na kuchukua hatua zilizo sahihi.

Kila unapokwama, kila unapopanga lakini huchukui hatua, jiulize ni kitu gani nahofia hapa?

Wakati mwingine unaweza kuwa unajizuia kufanikiwa kwa sababu unahofia ukifanikiwa wakati umezungukwa na watu ambao hawajafanikiwa itakuwa hali ngumu kwako. Maana wengine wataona una tamaa au umewadhulumu, na wengine wataona wewe ndiyo tegemeo lao. Kwa hofu hii utajizuia kabisa kufanikiwa. Lakini utakapochimba na kugundua kinachokuzuia kufanikiwa ni hofu hii, unajiweka huru kuwa na maisha yako na kuacha wengine waendeshe maisha yao kwa namna wanavyotaka wao wenyewe.

Rafiki, kama hutaikubali hofu yako hutaweza kuikabili, na kama hutaikabili hofu, hutaweza kupiga hatua yoyote kwenye maisha yako.

Kila mtu ana hofu, wale wanaoonekana jasiri ni kwa sababu wanachukua hatua licha ya kuwa na hofu. Lakini waoga hawatambui hata kinachowazuia ni hofu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha