“The greatest portion of peace of mind is doing nothing wrong. Those who lack self-control live disoriented and disturbed lives.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 105.7

Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata fursa nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari HATIA NI MBAYA KULIKO GEREZA…
Kama unataka utulivu mkubwa wa akili na roho yako, basi mara zote fanya kilicho sahihi.
Unapofanya kisicho sahihi, hata kama ni mafichoni na hakuna anayekuona, wewe mwenyewe unajua siyo sahihi.
Hatia unayokuwa nayo kwa kufanya kisichokuwa sahihi itakutesa sana kuliko ambavyo aliyefungwa anateseka.

Unapofanya makosa, unaishi nayo, huwezi kuyakwepa, hata kama hakuna mwingine anayejua.
Sasa kuishi na makosa hayo uliyofanya na kuficha ili wengine wasijue, ni mzigo mzito na inachosha mno.

Hii ndiyo sababu wapo watuhumiwa wengi ambao huamua kujisalimisha wenyewe kwenye vyombo husika licha ya kuweza kukimbia na kukwepa.
Ni kwa sababu maisha ya kukimbiakimbia yanakuwa magumu kwao, hali ya wasiwasi kila mara wasijue ni wakati gani wanakamatwa inafanya maisha yawe hovyo sana.

Ni afadhali mtu aliyefungwa jela, ambaye anajua kabisa anatumikia adhabu yake kwa kipindi fulani, kuliko yule anayekimbia ili asikamatwe kwa kosa alilofanya. Hatia itamuumiza sana mtu huyu kuliko kifungo.

Kupata amani ya moyo na utulivu wa nafsi, fanya kilicho sahihi mara zote. Epuka kufanya yasiyo sahihi, na kama imetokea umefanya basi kiri kosa ili uweze kurudisha utulivu wako.
Hakuna maisha magumu kama ya kuficha siri ya makosa uliyofanya, ni maisha ya wasiwasi mara zote.
Mtu ambaye hutaki ajue kosa ulilofanya anaweza tu kuwa anajisikia vibaya hivyo hajachangamka sana, lakini wewe utapata wasiwasi na kujiuliza “au ameshajua?”

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa huru kwa kufanya kilicho sahihi mara zote na pale unapofanya kisicho sahihi basi ukiri kosa ili usibaki na hatia itakayokutesa.

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha