“Kindness is invincible, but only when it’s sincere, with no hypocrisy or faking. For what can even the most malicious person do if you keep showing kindness and, if given the chance, you gently point out where they went wrong—right as they are trying to harm you?”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 11.18.5.9a
Mimi na wewe ni nani mpaka tumeipata nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo?
Wapo wengi waliokuwa na mipango mikubwa kwenye siku hii lakini hawajaiona kabisa, au wameiona lakini hawana nguvu ya kutekeleza kile walichopanga.
Wapo wengi sana ambao wangeipata siku hii moja tunayoipata leo, wasingepoteza hata sekunde moja, wangekamilisha yale muhimu ambayo walishindwa kuyakamilisha walipokuwa na nafasi kama tulizonazo sisi.
Hivyo basi rafiki yangu, hebu tuitendee haki siku hii ya leo, hebu twende kuishi kwa kuzingatia vipaumbele vyetu, tusipoteze hata sekunde moja kwa mambo yasiyo muhimu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari WEMA NI JIBU SAHIHI MARA ZOTE….
Kwenye maisha yetu ya kila siku, tunakutana na watu mbalimbali, ambao wana ajenda zao mbalimbali.
Wapo ambao wanatukosea na hata kutuumiza, wengine kwa makusudi na wengine kwa kutokujua.
Jibu sahihi mara zote, kwa chochote ambacho wengine wanatufanyia, ni kujibu kwa wema.
Iwe watu wametufanyia kitu kizuri au kibaya, jibu sahihi kwetu ni wema.
Mtu anapokufanyia ubaya, anategemea ujibu kwa ubaya, lakini wewe unapojibu kwa wema, anajidharau na anakuheshimu zaidi wewe, kwa sababu unakuwa umekwenda juu yake zaidi, unakuwa mkuu kwake.
Lakini mtu akikufanyia ubaya na wewe ukajibu kwa ubaya, anakudharau kwa sababu ubakuwa umeshuka kwenye viwango vyake vya chini.
Hakuna chochote unachopoteza kwa kujibu watu kwa wema, bila ya kujali walichofanya ni kizuri au kibaya.
Badala yake kujibu kwa wema inakupa wewe nguvu na ukuu kwa wengine.
Na usifanye kwa maigizo au ili kuonekana, badala yake fanya kutoka ndani ya moyo wako kweli.
Usiruhusu mtu yeyote avuruge utulivu wako wa ndani, tenda wema mara zote, jibu kwa wema nyakati zote na maisha yako yatakuwa bora, hutayumbishwa na chochote wanachofanya wengine na utaheshimiwa na kila mtu.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujibu kwa wema hata kwa wale wanaofanya ya kukuudhi na kukuumiza kwa makusudi.
#WemaNiJibuSahihi, #UsilipeUbayaKwaUbaya, UkuuNiKutosumbiliwaNaMamboMadogo
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha