“Don’t set your mind on things you don’t possess as if they were yours, but count the blessings you actually possess and think how much you would desire them if they weren’t already yours. But watch yourself, that you don’t value these things to the point of being troubled if you should lose them.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 7.27
Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Mimi na wewe rafiki yangu tuna bahati ya kipekee sana kuiona siku hii nyingine mpya, siyo kwa sababu ya akili na ujanja wetu, bali kwa bahati tu.
Hivyo njia pekee ya kulipa bahati hii ni kuiishi siku hii vizuri, kufanya yale kuhimu na kuachana na yasiyo muhimu, kusimamia kwa karibu vipaumbele vyetu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari HESABU BARAKA ZAKO…
Ni rahisi sana kwetu kuangalia yale ambayo tumekosa na kuyalalamikia,
Tunajiambia kama tungekuwa na kitu fulani basi maisha yetu yangekuwa bora sana,
Tunajiambia hatutakuwa na furaha mpaka tupate kitu fulani tunachokohitaji sana.
Lakini hivi ni kuchagua kuyapoteza maisha, kwa sababu hakuna wakati wowote kwenye maisha yako ambapo utapata kila unachotaka.
Hivyo njia bora ya kuyaishi maisha yako ni kuhesabu baraka zako.
Hesabu yale mazuri ambayo unayo na yanaendelea kwenye maisha yako.
Hili siyo tu litakufanya uyafurahie maisha yako, bali pia litakufanya uzione fursa nzuri zaidi kwenye maisha yako.
Maana unapohesabu baraka zako, unapoangalia upande mzuri wa maisha yako, unakaribisha mambo mazuri zaidi.
Hivyo rafiki badala ya kuangalia nini umekosa, angalia nini ulichonacho katika maisha yako.
Angalia kila ulichonacho na jiulize jinsi utakavyokikosa iwapo kitaondolewa kwenye maisha yako.
Huwa hatupati nafasi ya kujiuliza hili mpaka pale tunapokuwa tumepoteza kile ambacho tunachukulia kwa mazoea na baada ya kukipoteza ndiyo tunagundua kumbe kilikuwa muhimu sana.
Chukua kalamu na orodhesha vitu vitatu unavyofurahia kuwa navyo kwenye maisha yako, kwenye kazi na/au biashara yako, mahusiano yako na kwenye jamii yako kwa ujumla.
Fanya zoezi hili kila siku na utashangaa jinsi mtazamo wako utakavyobadilika kwa kila unachojihusisha nacho. Vitu vitakuwa muhimu kwako na utaziona fursa zaidi za hatua nzuri kwako kupiga.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuhesabu baraka zako na kuacha kuangalia nini ulichokosa.
#HesabuBarakaZako, #UnachoKilaUnachohitaji, #UsijilinganisheNaWengine
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha