“Show me that the good life doesn’t consist in its length, but in its use, and that it is possible—no, entirely too common—for a person who has had a long life to have lived too little.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 49.10b

Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UZURI WA MAISHA HAUPIMWI KWA WINGI WA MIAKA…
Watu wengi wamekuwa wanapenda kuishi miaka mingi, lakini hakuna chochote kikubwa wanachofanya kwenye miaka hiyo.
Wanayaendesha maisha yao kwa mazoea na hakuna alama yoyote wanayoacha hapa duniani.

Uzuri wa maisha haupimwi kwa wingi wa miaka ambayo mtu anaishi, bali jinsi ambavyo mtu ameishi miaka hiyo.
Uzuri wa maisha unapimwa kwa yale mambo ambayo mtu anafanya kwenye maisha yake, jinsi anavyogusa maisha ya wengine.

Wapo watu ambao wameishi miaka michache lakini wameweza kutoa mchango mkubwa sana kwa wengine.
Na wapo ambao wameishi miaka mingi lakini hakuna kikubwa wamefanya kwao wenyewe na hata kwa wengine.

Hivyo acha kuhesabu miaka yako ya kuishi, badala yake hesabu unafanya nini kwenye miaka hiyo.
Kila mwaka unaoongeza kwenye maisha yako, jiulize nini umefanya kwenye mwaka ulioisha na nini unakwenda kufanya kwenye mwaka ulioongeza.

Ishi maisha yako kwa namna ambayo yakikatika muda wowote kuna alama umeacha hapa duniani.
Iwe ni kwa kazi unayofanya, biashara unayofanya, uongozi uliopata au hata malezi uliyotoa kwa watoto wako.

Usifurahie tu kuongeza miaka na kusherekea kupata mwakwa mwingine kwenye maisha yako. Badala yake tafakari ni nini unaweka kwenye miaka hiyo, ni alama gani unaiacha hapa duniani.
Na jikumbushe tu, kuna siku utakuja kudaiwa vile ulivyopewa halafu hukuvitumia.
Hebu vitumie wasa wakati una maisha na una nguvu.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuyaishi maisha yako kwa kufanya vitu vinavyowagusa wengine na siyo tu kubesabu miaka.
#UboraWaMaishaSiyoWingiWaMiaka, #PimaMaishaKwaMchangoUnaotoa, #AchaAlamaHapaDuniani

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha