“Joy for human beings lies in proper human work. And proper human work consists in: acts of kindness to other human beings, disdain for the stirrings of the senses, identifying trustworthy impressions, and contemplating the natural order and all that happens in keeping with it.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.26
Ni jambo la kushukuru sana kwa mimi na wewe kuweza kuiona siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Tumeipata siku hii kama zawadi, na hivyo tunapaswa kuitumia kwa uangalifu mkubwa, kwa kuwa na vipaumbele na kuvifanyia kazi.
Tukaiishi siku hii kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA na tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari SEHEMU YA KUIPATA FURAHA…
Watu wamekuwa wakihangaika sana kutafita furaha,
Wengi wamefikiri furaha wataipata kwenye elimu, elimu wakaipata lakini siyo furaha.
Wakafikiri furaha wataipata kwenye kazi, kazi wakapata lakini siyo furaha.
Wakafikiri furaha wataipata kwenye biashara, biashara wakawa nayo lakini siyo furaha.
Wakafikiri furaha wataipata kwenye mahusiano, mahusiano wakawa nayo lakini siyo furaha.
Na pia wakaona wakishakuwa na mali nyingi basi watakuwa na furaha, mali wakawa nazo, lakini siyo furaha.
Maeneo yote hayo, na mengine mengi tunayoyatumia kutafuta furaha siyo sahihi.
Hutaipata furaha yako kwenye vitu, bali utaipata furaha yako kwa namna unavyotumia na kuchukulia vitu hivyo.
Utaipata furaha kwa kuwa mtu, na kufanya yale sahihi kwako kama mtu kufanya.
Na yaliyo sahihi mtu kufanya ni kuwa mwema kwa watu wengine, kudhibiti hisia zako, kufanya yaliyo sahihi na kufuata sheria za asili.
Elimu haitakupa furaha, bali jinsi unavyotumia elimu hiyo ndiyo kutakupa furaha.
Kazi haitakupa furaha, bali jinsi unaifanya kazi hiyo ndiyo kunakupa furaha.
Biashara haitakupa furaha, bali jinsi unavyoifanya biashara hiyo ndiyo kunakupa furaha.
Mahusiano hayatakupa furaha, bali jinsi unavyoyaendesha mahusiano hayo ndiyo kutakupa furaha.
Na mali hazitakupa furaha, bali jinsi unavyozichukulia na kuzitumia mali hizo ndiyo kunakupa furaha.
Utaipata furaha kwa kuwa mtu na kuishi kama mtu.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi kama mtu, kwa kufanya yale sahihi kwa mtu kufanya.
#FurahaNiMatendo, #UsikimbizeFuraha, #IshiKamaMtu
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha