Kila mtu hana muda, mambo mengi muda mchache ni kauli ambayo kila mtu anakiri inaendana na hali yake.

Lakini katika muda huo huo ambao wote tunao kwa usawa kila siku, kuna ambao wanafanya makubwa na kupiga hatua, wakati wapo ambao wanaona muda ukiyoyoma na wasione wamefanya nini.

Watu wengi huanza siku zao vizuri kwa kuzipangilia, lakini siku inapoisha, wakiangalia kipi kikubwa wamefanya hawakioni.

Siku nzima inakuwa siku ya kuzima moto, kupokea na kujibu jumbe na simu za watu, kufuatilia yanayoendelea na mengine mengi, ambayo mwisho wa siku ukiangalia yameleta mchango gani kwenye maisha yako huoni.

Leo nakwenda kukupa kipimo sahihi cha kuweka vizuri kipaumbele chako ili uweze kudhibiti na kutumia vizuri muda wako.

Kipimo hicho ni kujiuliza je miaka kumi ijayo utakumbuka hicho ambacho unataka kufanya?

Chukua mfano unataka kutembelea mitandao ya kijamii kwa sababu unaona unapitwa, au unataka kufuatilia habari kwa sababu unaona kuna vitu vinakupita, sasa kabla hujataka kutimiza hilo, jiulize je miaka 10 ijayo utakumbuka hicho ulichofanya leo? Utaona matokeo yake kwenye maisha yako?

Na wakati mwingine huhitaji hata kutumia miaka kumi, tumia tu mwezi mmoja. Utagundua vitu vingi unavyosukumwa kufanya leo, mwezi mmoja ujao havitakuwa na maana yoyote kwako.

Na kudhibitisha hili, jiulize tarehe kama ya leo unaposoma hapa mwezi uliopita ulifanya vitu gani? Jikumbushe tu kwa haraka haraka. Je unakumbuka habari zote ulizofuatilia kwa siku hiyo? Unakumbuka yaliyokuwa yanaendelea mtandaoni kwa siku hiyo, ambayo ulikazana sana usiyakose? Je unakumbuka jumbe na simu zote ilizojibu?

Vitu vyote ulivyofanya tarehe ya leo mwezi uliopita, ambavyo leo huvikumbuki kabisa na wala huoni mchango au matokeo yake kwenye maisha yako, ulipoteza muda wako kuvifanya.

Anza kutumia kipimo hiki kwa kila unalotaka kufanya leo na kila siku ya maisha yako, jiulize kabla hujafanya kitu, je hiki kitakuwa na matokeo ambayo nitayakumbuka miaka 10 ijayo? Kama jibu ni hapana usifanye, muda wako ni wa thamani sana kuupoteza kwenye vitu vinavyopita.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha