“Work nourishes noble minds.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 31.5

Ni furaha iliyoje mimi na wewe rafiki yangu kuiona siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Hatuna cha kusema bali shukrani kwa nafasi hii nyingine ya kipekee sana kwetu.
Siyo kila aliyeweka mipango yake jana kwa ajili ya leo amepata nafasi hii ambayo mimi na wewe tumeipata.
Wapo ambao wangekuwa tayari kutoa mamilioni ya fedha ili tu waweze kuiona siku hii, lakini imeshindikana.
Sasa mimi na wewe rafiki, ambao tumeipata siku hii bure kabisa, itakuwa ni dharau kubwa kama hatutaiishi siku hii vizuri, kwa kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi.

Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KAZI NI TIBA…
Binadamu tumeumbwa kwa ajili ya kazi,
Umbo letu la mwili limekaa kwa namna ya kufanya kazi.
Hivyo ili kukamilika kama binadamu, tunapaswa kufanya kazi.

Matatizo mengi kwenye maisha yanakuja pale ambapo mtu anakuwa hana kazi ya kufanya.
Msongo wa mawazo na hofu hupata nafasi ya kutawala akili ya mtu kama hakuna kazi iliyotawala akili hiyo.
Hisia za wivu, chuki na hata anasa hupata nafasi ya kutawala akili ambayo haisumbuliwi na kazi.
Magonjwa ya mwili kwa sehemu kubwa yanashambulia mwili ambao hauna kazi kubwa.

Ndiyo maana leo nakuambia kazi ni tiba.
Kazi ni tiba ya akili, kwa sababu inailisha akili yako chakula sahihi na kuondoa uchafu wowote ambao ungekupelekea kufanya maamuzi mabovu.
Kazi ni tiba ya mwili, kwa sababu inaulazimisha mwili kutumia virutubisho vilivyohifadhiwa na hivyo kupunguza sumu kwenye mwili.

Unapojikuta njia panda, unapoona changamoto na matatizo yanakuwa mengi kwenye maisha yako, jua una muda mwingi wa kutokufanya kazi.
Anza kutafuta kazi zaidi, kazi zinazohitaji sana akili yako, kazi zinazotumia hasa nguvu zako na haitakuchukua muda utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.
Kwanza fikra hasi na hofu zitapotea kabisa, pili mwili utakuwa changamfu na tatu hutapata muda wa kujihusisha na mambo yasiyo ya msingi.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kuweka kipaumbele kwenye kazi, siku ya kunufaika na tiba ya kazi. Ipende sana kazi, haijawahi kumtupa yeyote. Fanya kazi kila siku ya maisha yako na yatakuwa bora sana.
#KaziNiTiba, #MapenziNaKazi, #IpendeKaziYako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Makirita 3.1,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1