Unapochagua kuyaishi maisha yako, unapochagua kufanya kile ambacho ni muhimu zaidi kwako na kupuuza vitu vingine, kuna watu ambao utawaumiza. Kama haupo tayari kuona wengine wakiumia kwa maisha uliyochagua, nafasi yako ya kufanikiwa ni ndogo au haipo kabisa.

Kama unataka kila mtu akubaliane na wewe au apende kile unachofanya, huwezi kufanya kitu kilicho bora. Utaishia kufanya kitu cha kawaida, kwa lengo la kueleweka na kila mtu. Lakini hata hivyo bado hutaweza kuwaridhisha watu wote, kuna ambao utawaumiza kwa kuchagua kuwa kawaida badala ya kuwa bora.

Mtu wa kwanza unayepaswa kumsikiliza kwenye maisha yako ni wewe, maana huyo ndiye mtu ambaye huwezi kumwepa kwenye maisha yako, utakaa naye kila siku, ukilala uko naye ukiamka uko naye.

Hivyo maamuzi yote ya maisha yako lazima yaanzie ndani yako, kwamba ni kipi muhimu zaidi kwako, kipi kinakuridhisha wewe, kabla hujaangalia wengine.

Maamuzi yoyote unayofanya kwenye maisha yako yatawaumiza baadhi ya watu, hivyo ni vyema usiwe mmoja wa watakaoumizwa na maamuzi yako.

Chagua ni watu gani unaotaka kuwahudumia kupitia kazi yako au biashara yako, kisha weka juhudi zako kuwahudumia kwa ubora sana. Wengine wote wapuuze na achana nao, wataumia, watakuchukia na watakusema vibaya, lakini hilo siyo tatizo lako, ni matatizo yao binafsi.

Watu wamekuwa wanachukia vitu bila hata ya kuvijua kwa undani, hivyo usiumizwe pale ambapo mtu ambaye hujamchagua kumhudumia anapoumia au kuchukia, ni wajibu wake kuendesha maisha yake kwa vipaumbele vyake na siyo kuilazimisha dunia iwe kama wao wanavyotaka.

Jua wapo wengi utakaowaumiza kwa kuchagua kuyaishi maisha yako, lakini hilo lisikuzuie kuyaishi maisha yako, kwa sababu wewe ni wa muhimu zaidi kuliko mtu mwingine yeyote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha