Siku mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tunayo nafasi hii nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye yale tunayofanya ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUWA TAYARI KUBADILIKA…
Tunapanga mambo yetu kwenye maisha, lakini dunia nayo ina mipango yake.
Mara nyingi mipango yetu na ya dunia haiendani kabisa.
Hivyo huwa tunakosa kile ambacho tumepanga kukipata, kwa namna tuliyotegemea kupata.

Hapa ndipo safari ya wengi huishia, kwa kukubali kwamba hawawezi kupata wanachotaka au kufika wanakotaka.
Lakini wale wanaopiga hatua zaidi siyo kwamba hawakutani na hali hizi, wanakutana nazo sana, ila wanakuwa tayari kubadilika.
Kitu kimoja kinaposhindikana wanajua wanaweza kupata vingine zaidi.
Mlango mmoja unapojifunga wanajua mingine mingi itafunguka.
Ni utayari wao wa kubadilika na kufanya kile kinachowezekana kwa wakati huo ndiyo unawawezesha kufanikiwa.

Hili ndiyo unapaswa kuliweka kwenye maisha yako,
Usikubali kabisa kukwamishwa na chochote, usikubali chochote kiwe sababu ya wewe kusimama.
Kama ulipanga kupita njia fulani kufika sehemu fulani, na ukakuta njia hiyo imefungwa, tafuta njia nyingine.
Na kama umetafuta njia umekosa, tengeneza njia mpya.
Muhimu ni kufika pale unapotaka kufika, hivyo kuwa tayari kubadilika kadiri mazingira yanavyotaka ili ufike.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa tayari kubadilika kadiri hali na mazingira yanavyokutaka ubadilike.
#MipangoSiMatumizi, #MaraZoteIpoNjia, #KuwaTayariKubadilika

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1