Hakuna mtu ambaye hakutani na matatizo kwenye maisha yake. Matatizo ni sehemu ya maisha ya kila mmoja wetu.
Lakini wengi wanapoingia kwenye matatizo, huwa wanahamaki na kushindwa kujua wanatokaje kwenye matatizo hayo. Na hata wanapojaribu kuchukua hatua fulani, wanajikuta wakitengeneza matatizo makubwa zaidi.
Hii ni kwa sababu wengi huwa wanakimbilia kutatua tatizo kabla ya kupitia hatua ya kwanza muhimu kwenye kutatua tatizo lolote lile. Wengi hukimbilia kwenye suluhisho kabla ya kupitia hatua hiyo ya kwanza, na suluhisho lolote wanalopata huwa halidumu na huzalisha matatizo makubwa zaidi.
Hatua ya kwanza ya kutatua tatizo lolote unalokutana nalo ni kulielewa kwanza tatizo hilo. Lielewe tatizo hilo kwa undani kabla hata hujaanza kufikiria kulitatua. Elewa nini kimesababisha tatizo hilo, ni jinsi gani hilo limekuwa tatizo na msingi wake hasa uko wapi.
Kwenye kila tatizo, kuna msingi mkuu wa tatizo, hiki ni kiini cha tatizo husika, halafu kuna matokeo ya tatizo, haya ni yale madhara yanayoonekana kwa nje.
Sasa wengi wanapotatua tatizo, huwa wanakimbilia kukabiliana na matokeo ya nje ya tatizo na kusahau kiini cha tatizo husika. Hivyo hatua wanazochukua hazileti matokeo kwa sababu hawajagusa chanzo chenyewe.
Unapolijua tatizo, unakijua chanzo kikuu cha tatizo, na hivyo unapolitatua unakwenda kugusa chanzo kikuu cha tatizo hilo.
Unapojikuta upo kwenye tatizo, au umekwama popote, jizuie kukimbilia kutatua na jipe muda wa kulichunguza na kulielewa tatizo kwa kina. Angalia kila kinachohusika kwenye tatizo hilo na kujihakikishia umefika kwenye chanzo kikuu cha tatizo hilo. Hapo sasa ndiyo unaweza kujua hatua zipi sahihi kuchukua ili kutatua tatizo hilo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,