Dunia ni kubwa na imejaa watu wa kila aina,

Kuna watu wema na watu wabaya, kuna watu waaminifu na wasio waaminifu, kuna watu makini na walio wazembe.

Hiyo ndiyo dunia, imekuwa hivyo kwa muda mrefu na itaendelea kuwa hivyo.

Lakini wewe kwa sababu ambazo hatuzijui, umeamua kujipa jukumu la kuinyoosha dunia, kutaka kila mtu aende kama unavyotaka wewe, kutaka dunia iwe na watu wazuri, waaminifu na walio makini muda wote.

Siyo tu kwamba jukumu hili ni gumu kwako, bali pia siyo jukumu sahihi kwako, unajitesa na kupoteza muda na nguvu zako bure.

Dunia ipo kama ilivyo, inajiendesha yenyewe kwa kanuni za asili, inawalipa watu kulingana na wanachofanya na hakuna anayeweza kuidanganya wala kuiibia dunia.

Dunia inatoa zawadi zake na adhabu zake hapa hapa duniani kwa yale matendo ambayo watu wanayafanya.

Hivyo badala ya wewe kujichagua kuwa kiranja wa dunia, wa kuhakikisha kila mtu ananyooka na kwenda unavyotaka wewe, ningekushauri upeleke muda huo na nguvu hizo katika kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi, hili ndiyo jukumu pekee lililopo ndani ya uwezo wako na ambalo unaweza kuliathiri.

Iache dunia iende inavyoenda, wewe kazana na maisha yako na yale unayofanya.

Jua dunia ina watu wa kila aina, na kadiri unavyokwenda utakutana na wengi wa aina tofauti ambao hata hukutegemea. Lengo lako ni kujifunza kupitia kila unaokutana nao, na kujua ni watu wa aina gani wa kushirikiana nao na watu wa aina gani wa kuwakwepa kwenye maisha yako.

Kwa mfano, inapokuwa kwenye kushirikiana na wengine, badala ya kuchukua mtu yeyote na kisha kujiambia utambadili, chagua kushirikiana na watu ambao tayari wana tabia unazozitaka, ambao hawahitaji kubadilishwa. Siyo jukumu lako kuwabadilisha wengine na kama watu hawataki kubadilika hakuna unachoweza kufanya ukawabadili.

Na unapotegemea watu wakupe au wafanye kitu fulani na wao wakafanya tofauti, usijiumize, jua ndivyo watu walivyo, ndivyo dunia ilivyo na jifunze kuwa na vigezo bora vya kuchagua watu utakaowategemea kwenye shughuli unazofanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha