Unapopata nafasi ya kufanya kitu kwa ajili ya wengine, basi jisukume sana ufanye kitu hicho vizuri, kwa namna ambayo watu hao watanufaika na maisha yao kuwa bora zaidi.
Kila mmoja wetu huwa anapata nafasi ya kufanya kitu kwa ajili ya wengine, lakini wengi wamekuwa wanapoteza nafasi hizi na zisiwe na manufaa makubwa kwao baadaye.
Njia pekee ya sisi kuacha alama hapa duniani, ni jinsi tunavyoyagusa maisha ya wengine. Jinsi tunavyowahudumia kwa namna ambayo inaboresha maisha yao na wao kunufaika sana.
Iwe ni kwenye kazi au biashara na hata kwenye maisha ya kawaida, wahudumie vizuri wale unaokutana nao. Jua hitaji lao kubwa ni lipi kisha watimizie, na kazana kuwatimizia kwa viwango vya juu sana.
Watu hawa wataridhika na huduma unayowapa, na watakuwa tayari kurudi tena na hata kuwaleta wengine pia. Hii ni njia nzuri na ya uhakika ya kukua zaidi kuliko kupiga kelele watu wengi zaidi wakusikie.
Watu wengi wanaopata nafasi za kuwahudumia wengine, wamekuwa wanazichukulia kwa mazoea, kwa kufanya kile walichozoea kufanya na kuona kila anayekuja hastahili sana umakini wake. Hapa ndipo wengi wanapoteza nafasi za wao wenyewe kukua zaidi.
Kwako inaweza kuwa siku ya kawaida ya kazi, lakini kwa yule anayekuja kupata huduma kwako, inaweza kuwa siku mbaya sana kwake na hivyo anakutegemea wewe umsaidie isiwe siku mbaya zaidi. Hivyo weka hisia zako pembeni na kazana na hisia za yule unayemhudumia.
Tumekuwa tunaona pia wachache ambao wanapata nafasi za uongozi na madaraka kuzitumia kwa mabavu, kuona kama wao ndiyo wanastahili zaidi na hakuna anayejua kama wao. Hili pia linaharibu sana huduma ambayo mtu anaitoa. Kama umepata nafasi ya uongozi au madaraka, itumie nafasi hiyo kuwahudumia na kuwatumikia wengine. Ona nafasi uliyoipata kama fursa kwako ya kufanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi, na siyo kuyafanya kuwa magumu zaidi.
Utakuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa, kama utaachana na mengine yote na kuamua kuwahudumia wengine vizuri sana. Anza sasa kuwa mtu wa huduma na utaweza kupiga hatua zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,