#TANO ZA JUMA #23 2019; Suluhisho Lipo Ndani, Jinsi Ya Kuwa Mtawa Wa Mjini, Njia Sahihi Ya Kukabiliana Na Msongo Wa Mawazo, Maisha Uliyopoteza Na Wewe Ni Kile Unachokula.

Hongera sana rafiki yangu kwa juma hili la 23 ambalo tumekuwa nalo na linaelekea kabisa ukingoni. Imani yangu ni kwamba juma hili limekuwa la kipekee sana kwako, ambapo umeweza kujifunza na kujaribu vitu vipya kwenye kazi zako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Karibu kwenye TANO ZA JUMA ambapo nakushirikisha maeneo matano muhimu ya kujifunza na kupiga hatua kwenye maisha kupitia kitabu chetu cha juma ambacho nakuchambulia kwa kina sana.

Juma hili la 23 tunakwenda kujifunza kutoka kitabu kinachoitwa The Urban Monk: Eastern Wisdom and Modern Hacks to Stop Time and Find Success, Happiness, and Peace  ambacho kimeandikwa na Pedram Shojai. Pedram amekuwa mtawa wa falsafa ya Taoism na pia daktari wa tiba za mashariki. Kupitia uzoefu wake wa utawa na kutibu watu, amegundua kuna changamoto kubwa kumi ambacho tunazipitia binadamu kwa zama tunazoishi. Changamoto hizo ni msongo, muda, nguvu, usingizi, mtindo wa maisha wa kukaa, ulaji, kutengana na asili, upweke, fedha na kukosa kusudi la maisha.

urban monk

Kupitia kitabu chake, Pedream amejadili kila changamoto na kutupa hekima za kuzikabili changamoto hizo kutoka kwenye falsafa za mashariki.

Karibu kwenye tano za juma, ujifunze falsafa bora ya kuendesha maisha yako kwa utulivu, furaha na mafanikio makubwa.

#1 NENO LA JUMA; SULUHISHO LIPO NDANI.

Ni kawaida yetu binadamu pale tunapokutana na changamoto kwenye maisha kukimbilia kutafuta jawabu la changamoto hiyo nje yetu.

Wapo ambao wanakimbilia kueleza changamoto zao kwa wengine, wapo ambao wanatumia vilevi ili kusahau changamoto hizo na wengi wamekuwa wanatafuta chochote cha kuwasumbua ili tu wasipate muda wa kufikiria changamoto hiyo.

Usumbufu ambao wengi wamekuwa wanautumia kukimbia changamoto zao ni kuangalia televisheni, kutembelea mitandao ya kijamii na hata kufuatilia habari mbalimbali.

Lakini njia zote hizi za kukimbia changamoto hazitatui changamoto hiyo, bali zinakufanya uisahau kwa muda, lakini changamoto inaendelea kuwepo na tena inazidi kukua na kuwa sugu zaidi.

Rafiki, jibu la changamoto yoyote unayopitia lipo ndani yako, wewe pekee ndiye unayeweza kutatua changamoto unayopitia, na majibu unayo tayari, lakini hutayaona kwa urahisi kama hujaweka kazi kubwa kuweza kuyaona.

Unapopata tatizo au changamoto kwenye maisha yako, acha kabisa ile hali ya kutafuta suluhisho nje yako, jua kwamba suluhisho lipo ndani yako.

Hivyo unachohitaji ni kupata muda wa kutulia wewe peke yako na kutafakari changamoto unayoipitia kwa kina. Fanya tahajudi na tuliza kabisa mawazo yako. Ione changamoto hiyo kwa undani na fika kwenye kiini cha changamoto hiyo.

Kwa kufanya hivi kwanza utajua chanzo halisi cha changamoto, na utaona kumbe wewe mwenyewe ndiye msababishaji mkuu wa changamoto unayopitia. Utaona kuna kitu ulifanya au hukufanya na kimechangia changamoto hiyo kutokea.

Kwa kujua chanzo halisi cha changamoto, utaweza kuchukua hatua sahihi na kuitatua.

Lakini kama utakimbilia kuangalia nje, utaishia kuwalaumu wengine, changamoto haitatatuliwa na maisha yako yatazidi kuwa magumu.

Jawabu la matatizo na changamoto unazopitia kwenye maisha lipo ndani yako, pata muda wa kutulia na wewe mwenyewe na utaweza kuona njia sahihi kwa kila ugumu unaopitia.

#2 KITABU CHA JUMA; JINSI YA KUWA MTAWA WA MJINI.

Watawa ni watu ambao wamechagua kuachana na maisha ya kawaida na kwenda kuishi maisha rahisi kabisa ambayo jukumu lake kubwa ni kukua kiroho na kumjua zaidi Mungu. Watawa wengi wana maisha ambayo hayana msongo kwa sababu hawana majukumu mengi ya kidunia, wanayaendesha maisha yao kwa urahisi kabisa kwa kuhangaika na yale mahitaji ya msingi pekee ambayo ni chakula, maji, mavazi na moto. Chochote nje ya hapo ni anasa na hakimsumbui mtawa. Kwenye makazi ya watawa, majukumu ni manne tu, kusali/kutahajudi, kuteka maji, kupasua kuni na kuandaa chakula.

Maisha ya utawa yana manufaa makubwa sana. Ni maisha ambayo hayana msongo kwa sababu mtu hasumbuki na mambo ambayo siyo muhimu. Ni maisha ambayo mtu anaishi kwenye wakati uliopo na kufurahia kila kinachokuja mbele yake, na kukitumia ili kupiga hatua zaidi.

Wengi wetu tungeweza kunufaika sana na maisha ya utawa, lakini wazo la kuacha mambo yote ya dunia ili kuingia kwenye maisha ya utawa halingii kwenye akili zetu. Wengi wetu tayari tuna majukumu ambayo hatuwezi kuyakimbia. Tayari tuna familia ambazo zinatutegemea, kazi ambazo tumeshaingia mikataba ya kuzifanya na ahadi mbalimbali ambazo tumeshaweka na wengine kwenye maisha yetu ya kawaida.

Kwa kushindwa kwenda kuishi kama watawa, wengi wamekata tamaa na kuona hakuna namna bali kuishi maisha ya msongo kila siku. Maisha ya kukimbizana na kila kinachopita mbele ya mtu na kusubiri siku ya kifo.

Lakini sivyo Mtawa Pedram Shojai anavyofikiria. Yeye pamoja na kuwa mtawa wa Falsafa ya Tao, lakini pia ni mtu mwenye maisha ya kawaida, ambaye ana familia, ana biashara anazoendesha na ana majukumu mengine mengi ya kijamii.

Pedram anatuambia kila mmoja wetu anaweza kuishi kama mtawa na kuzipata faida za maisha ya utawa bila ya kuacha kabisa maisha yetu ya kawaida.

Kwenye kitabu chake cha The Urban Monk: Eastern Wisdom and Modern Hacks to Stop Time and Find Success, Happiness, and Peace  ambacho kimeandikwa, Pedram Shojai ametushirikisha njia mbalimbali za kitawa za kutatua changamoto kubwa tunazopitia kwenye maisha yetu ya kila siku.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hiki cha THE URBAN MONK, tujifunze jinsi ambavyo tunaweza kuishi kama watawa, tukanufaika na maisha ya utawa bila ya kuacha maisha yetu ya kawaida.

Kwenye uchambuzi huu tutaziangalia changamoto kubwa kumi tunazopitia kwenye maisha na hatua za kuchukua ili kuvuka changamoto hizi na kuwa na maisha bora.

CHANGAMOTO YA 1; MSONGO.

Msongo umekuwa changamoto kubwa kwenye maisha yetu kwa sababu tuna mambo mengi ya kufanya na muda ni mchache. Lakini pia hofu tunazokuwa nazo zinatafsiriwa vibaya na akili na hivyo mwili kuwa kwenye msongo mkubwa kwa kitu ambacho siyo hatari sana kwenye maisha yetu.

Ili kuondokana na hali ya msongo, fanya yafuatayo;

  1. Mara zote kuwa na utulivu wa ndani bila ya kujali nini kinaendelea nje.
  2. Dhibiti tamaa zako, kwa sababu kutamani mambo mengi kunaleta msongo.
  3. Chambua sana taarifa unazoruhusu ziingie kwenye akili yako.
  4. Jikomaze kwa kujitengenezea msongo mdogo mdogo.
  5. Jifunze kusikiliza wengine.
  6. Fanya tahajudi.
  7. Usitumie vilevi.
  8. Fanya mazoezi.

CHANGAMOTO YA 2; MUDA.

Tuna masaa 24 kwa siku, na hakuna mwenye uwezo wa kuongeza hata dakika moja. Lakini mambo ya kufanya kwenye muda huu ambao haubadiliki yamekuwa yanaongezeka kila siku. Kadiri mambo ya kufanya yanavyoongezeka tumekuwa tunakazana kuyakandamiza kwenye muda mfupi tulionao.

Mwishowe tunazalisha msongo, tunashindwa kukamilisha yale majukumu muhimu kwetu na hatimaye maisha yetu yanakuwa hovyo.

Wewe kama mtawa wa mjini unapaswa kuchukua hatua zifuatazo ili kuwa na matumizi mazuri ya muda wako.

  1. Jifunze kusema hapana kwa mambo ambayo hayana umuhimu sana kwako.
  2. Usishindane na muda, bali nenda nao, usilazimishe kufanya vitu kwa muda usiowezekana, bali kazana kutumia muda ulionao vizuri.
  3. Fanya tahajudi ya kukupa utulivu pale unapokuwa na mambo mengi ya kufanya.
  4. Jipe mfungo wa habari na mitandao ya kijamii. Kwa mwezi mmoja acha kabisa kufuatilia habari na mitandao ya kijamii na utaona jinsi ambavyo utakuwa na muda mwingi wa kufanya yale muhimu.
  5. Tenga muda wa kupumzika kwenye siku yako, na muda huo unapofika pumzika kweli. Mfano unaweza kufanya kazi kwa dakika 50 kwa umakini, kisha kupumzika kwa dakika 10, na kurudia hivyo kwa siku nzima. Muda wa kupumzika unapumzika kweli.
  6. Kusanya majukumu madogo madogo na yafanye pamoja. Mfano badala ya kujibu meseji au email kila wakati, tenga muda mmoja ambao utajibu meseji na email zote na fanya hivyo kwa muda huo tu.

CHANGAMOTO YA 3; NGUVU.

Kukosa nguvu ni changamoto kubwa ya zama tunazoishi. Kila mtu amechoka, panda usafiri wa umma jumatatu asubuhi ambayo ndiyo siku ya kwenda kuanza juma na angalia nyuso za watu wamechoka utadhani ndiyo mwisho wa juma. Nenda maeneo ya kazi na utakuta asubuhi na mapema watu wanasinzia.

Uchovu umekuwa juu sana zama hizi kwa sababu maisha yamekuwa hayana tena mipaka. Watu wanaweza kufanya mambo yasiyo ya kazi wakiwa kazini, na wakati ambao ni wa mapumziko hawapumziki kweli, badala yake wanaendelea kujihusisha na mambo yanayowachosha zaidi.

Pia ukosefu wa nguvu umekuwa unachangiwa na aina ya vyakula ambavyo wengi tunatumia zama hizi. Vimekuwa siyo vyakula vya kuupa mwili nguvu, bali vyakula vya kushibisha matumbo yetu.

Ukosefu wa nguvu umekuwa chanzo kikuu cha ufanisi na uzalishaji kushuka maeneo ya kazi, kukosa umakini na hata kushindwa kuyafurahia maisha.

Mtawa wa mjini anachukua hatua zifuatazo ili kuwa na nguvu zaidi kwenye maisha yake.

  1. Usitumie kahawa au vinywaji vya kuongeza nguvu, hapa unakopa nguvu za kesho kutumia leo, kesho utalipa. Kama umechoka pumzika.
  2. Kula chakula halisi na achana na vyakula visivyo halisi. Vyakula halisi vina virutubisho vyote muhimu na madini yanayoupa mwili nguvu.
  3. Epuka sumu ambazo zipo kwenye vyakula visivyo halisi na kwenye vinywaji mbalimbali.
  4. Uwekwe mwili kwenye mwendo, fanya mazoezi na hakikisha chakula unachokula unakitumia, la sivyo kinahifadhiwa kwenye mwili na kufanya afya kuwa hovyo.
  5. Usikilize mwili wako, na pale unapokuambia umechoka basi pumzika.
  6. Usile mpaka ukashiba kabisa, ukishafika nusu ya kula, pumzika kwa dakika 5 mpaka kumi na baada ya hapo utajisikia kushiba kabisa.
  7. Tenga muda wa kuwa peke yako, muda wa kutafakari maisha na kuona ulipotoka, ulipo na unapokwenda. Tafakari za aina hii zinakupa nguvu mpya ya kuendelea kupiga hatua zaidi.

CHANGAMOTO YA 4; USINGIZI.

Usingizi umekuwa unachukuliwa kama anasa au kitu ambacho tunaweza kukipunguza ili kupata muda zaidi. Tunapokuwa na mambo mengi ya kufanya na muda hautoshi, basi huwa tunapunguza muda wa kulala.

Kukosa muda wa kutosha wa kulala imekuwa changamoto kubwa sana zama hizi. Kulala ni hitaji muhimu la mwili, mwili unafanya kazi ya kurekebisha maeneo yenye matatizo wakati mtu umelala. Hivyo kama hupati muda wa kutosha wa kulala, mwili hauwezi kujirekebisha hivyo unachakaa haraka.

Pia kulala ndiyo muda ambao mwili unatengeneza nguvu mpya, unapolala ni sawa na unaweka simu kwenye chaji, kulala ni kuuchaji mwili wako na ukilala muda wa kutosha unaamka ukiwa na nguvu za kwenda kufanya yale muhimu.

Ili kuwa na usingizi bora, mtawa wa mjini anafanya yafuatayo;

  1. Epuka vilevi au kahawa muda wa kulala. Unapaswa kunywa kahawa masaa nane kabla ya kulala. Kama unalala saa nne usiku basi mwisho wa kunywa kahawa ni saa nane mchana.
  2. Epuka vyakula vyenye sukari kwa wingi muda unaokwenda kulala, vyakula hivi vinauchosha mwili zaidi.
  3. Chumba unacholala kinapaswa kuwa tulivu na chenye joto la wastani na pia kiwe na giza.
  4. Chumba unacholala kisiwe na tv, na wala usilale na simu yako.
  5. Jitengenezee utaratibu unaufuata kabla ya kulala, labda kujisomea kitabu cha kawaida, kuandika yale uliyofanya kwenye siku yako na kadhalika.
  6. Andika chochote kinachokupa mawazo na msongo kabla ya kulala, unapoandika kitu unakitoa kwenye mawazo yako na hivyo hukifikirii tena.
  7. Fanya mapenzi kabla ya kulala, tendo hili linaleta usingizi bora zaidi.
  8. Kunwa maji ya kutosha kabla ya kulala, lakini usinywe mengi sana kiasi cha kukufanya uamke kila wakati kwenda kukojoa.

CHANGAMOTO YA 5; MTINDO WA MAISHA YA KUKAA.

Huu ndiyo mfumo wa maisha ya watu wengi zama hizi, unaamka kitandani, unakaa kwenye gari kwenda kazini, ukifika kazini unakaa siku nzima ukifanya kazi, kazi ikiisha unakaa tena kwenye gari kurudi nyumbani na ukifika nyumbani unakaa tena kuangalia tv au kufuatilia habari na mitandao ya kijamii. Tunatumia sehemu kubwa ya muda wetu kukaa.

Lakini hivi sivyo tulivyoumbwa binadamu, hatukuumbwa kukaa, tuliumbwa kutembea na kufanya kazi zinazohusisha mwili mzima. Tangu enzi na enzi watangulizi wetu wamekuwa wakiwinda, wakilima, wakichunga na shughuli nyingine zinazohitaji nguvu kubwa.

Mtindo wa maisha wa kukaa muda mrefu umekuwa chanzo cha magonjwa mengi ambayo yanatusumbua zama hizi.

Mtawa wa mjini anaweza kufanya yafuatayo ili kukabiliana na changamoto hii ya mtindo wa maisha wa kukaa muda mrefu.

  1. Kaa chini badala ya kukaa kwenye kiti. Ukaaji kwenye viti kwa muda mrefu umeleta madhara kwenye viuno na migongo ya wengi. Kukaa chini kuna manufaa kuliko kukaa kwenye viti.
  2. Tenga muda wa kutembea, hili linaufanya mwili kuwa kwenye mwendo.
  3. Tumia meza za kusimama, kama kazi yako inahusisha kukaa muda mwingi, tumia pia meza za kusimama ambapo unaweza kufanya kazi ukiwa umesimama.
  4. Chagua mchezo ambao utakuwa unajihusisha nao kwa kucheza na acha kuwa mshangiliaji wa michezo tu.
  5. Tembea peku kwenye mazingira ya asili. Tumejitenga sana na dunia kwa muda wote kuwa na viatu. Dunia ina nguvu ya kuweza kuweka miili yetu sawa kama tutaruhusu mwili ukutane na dunia. Tunaweza kufanya hivyo kwa kutembea peku kwenye mazingira ya asili.
  6. Fanya tahajudi ya kutembea.
  7. Kama unaweza fanya kazi ambayo haikutaki kukaa kwenye foleni kila siku kwenda na kurudi kazini.
  8. Tumia usafiri mbadala kwenda kwenye kazi zako kama baiskeli badala ya gari.
  9. Kuwa na mapumziko ya kubadili kukaa kwako kila baada ya nusu saa. Usikae kwa muda mrefu bila ya kubadili mkao.
  10. Fanya mkutano wa kutembea, kama kuna mtu una mazungumzo naye, badala ya kukaa, mnaweza kutembea huku mnafanya mazungumzo.

CHANGAMOTO YA 6; ULAJI.

Ulaji ni changamoto kubwa sana zama hizi kwa sababu vitu tunavyoita chakula leo, mtu aliyeishi miaka 100 iliyopita hataweza kuvitambua kama vyakula.

Vyakula tunavyokula siyo vya asili tena, bali vyakula vya kutengenezwa na kuzalishwa viwandani. Vyakula hivi havina virutubisho vya kutosha na hivyo miili yetu haipati nguvu kutoka kwenye vyakula tunavyokula.

Lakini pia vyakula ambavyo tumekuwa tunakula vimekuwa havitumiki kwenye mwili, na hivyo kuhifadhiwa kwa kiasi kikubwa, kitu ambacho kimesababisha uzito wa mwili kuongezeka na magonjwa kama kisukari na presha kuongezeka kwa kasi.

Ili kuondokana na changamoto hii ya ulaji, wewe kama mtawa wa mjini zingatia yafuatayo;

  1. Usile kabisa sukari, ni sumu, ni madawa ya kulevya na haina manufaa makubwa kwenye mwili wako.
  2. Tumia vyakula vya wanga kwa kiasi kidogo sana na kwenye mlo mmoja wa siku, isiwe mlo wa kifungua kinywa.
  3. Epuka kula vyakula vyenye sumu, vyakula ambavyo vimekuzwa kwa madawa au kupekewa madawa ili kuepusha kushambuliwa na wadudu mbalimbali. Madawa haya huwa hayaharibiki na hivyo yanakuwa sumu mwilini.
  4. Kula chakula hai, kama ni mnyama basi amechinjwa siku hiyo na kama ni mboga basi zimechumwa siku hiyo. Usile vyakula vilivyohifadhiwa kwa muda mrefu au vilivyosindikwa viwandani.
  5. Kuwa na utaratibu wa kufunga, angalau siku moja kila siku. Hii inaufanya mwili kujisafisha na kuondoa vyakula vya ziada pamoja na sumu.
  6. Lima chakula chako mwenyewe, vitu kama mbogamboga, kuwa na bustani unayoitunza mwenyewe.
  7. Kula angalau masaa mawili kabla ya muda wako wa kulala.
  8. Kula unapokula, wakati unakula, akili na mawazo yako yote yawe kwenye chakula unachokula.

CHANGAMOTO YA 7; KUTENGANA NA ASILI.

Maendeleo yametutenga sana na asili. Wengi wetu tunaishi kwenye miji mikubwa na muda mwingi tumezungukwa na teknolojia mpya. Hili linatuweka mbali kabisa na vitu vya asili ambavyo vina mchango mkubwa kwenye utulivu wetu na hata kuyajaza maisha yetu.

Kwa kujitenga na asili tunaisahau asili yetu binadamu na tunapatwa na msongo mkubwa.

Ili kuondokana na changamoto hii, fanya yafuatayo;

  1. Tembelea maeneo ya asili ukia huna simu yako wala huna usumbufu wowote.
  2. Fanya tahajudi pembeni ya mto, ziwa au bahari kwa kufuata mawimbi ya maji.
  3. Tengeneza bustani nyumbani kwako ambayo inakukutanisha na asili kila siku.
  4. Jifunze ujuzi wa asili wa kukuwezesha kuishi kama ukipotea msituni. Jifunze kuwasha moto bila kiberiti, kupata maji safi, kupata na kuandaa chakula pamoja na kutengeneza malazi yako mwenyewe. Kwa kuwa na ujuzi wa vitu hivyo vinne utaweza kuishi popote.
  5. Kula vyakula vya asili, hivi vina bakteria wanaosaidia tumbo lako kufanya kazi vizuri.
  6. Tembea peku kwenye asili, matembezi ya taratibu na ya tahajudi.

CHANGAMOTO YA 8; UKWEKE.

Licha ya uwepo wa mitandao ya kijamii inayoweza kutuunganisha na mtu yeyote duniani masaa 24 kwa siku na siku 7 za wiki, upweke ni changamoto kubwa sana zama hizi. Tumezungukwa na watu wengi lakini bado tuna upweke mkubwa.

Sehemu kubwa ya upweke huu umesababishwa na maendeleo ya teknolojia ambayo yanawafanya watu kujitegemea wenyewe zaidi kuliko kuwategemea wengine. Pia vyombo vya habari vimekuwa vinaonesha dunia ni sehemu hatari sana ya kuishi hivyo watu wanaogopana.

Ili kuondokana na hali hii ya upweke, fanya yafuatayo;

  1. Rudi kwenye msingi mkuu ambao ni familia. Tenga muda wa kuwa na familia yako, hawa ni watu muhimu sana kwako.
  2. Fanya vitu kwa pamoja na wengine, kama matembezi, michezo, na shughuli nyingine.
  3. Unapokuwa na watu wengine, usitumie simu wala teknolojia nyingine yeyote. Kwa nyumbani mnapokuwa pamoja tv isiwashwe.
  4. Jua ni vitu gani unavyopenda zaidi kufanya na tenga muda wa kufanya vitu hivyo.
  5. Ishi maisha ya kuwahudumia wengine, chochote unachofanya, kazana kutoa huduma zaidi kwa wengine kuliko unavyonufaika wewe.
  6. Fanya matendo madogo madogo ya upendo, kwa kuwasaidia watu vitu ambavyo hawawezi kukulipa. Mfano kumfungulia mtu mlango hata kabla hajakuomba.
  7. Tafuta ukuaji wa kiroho badala ya kung’ang’ana na dini.
  8. Jiunge na vikundi vya kijamii kwenye maeneo uliyopo.
  9. Punguza muda unaotumia kwenye mitandao na tv na weka muda huo kwa wengine.
  10. Fanya kitu ambacho unaogopa kufanya, mfano kama unahofia kuongea mbele ya watu, basi kila siku tafuta fursa ya kuongea mbele ya wengine, kwa njia hii unaishinda hofu yako na kuimarisha mahusiano yako pia.

CHANGAMOTO YA 9; FEDHA.

Fedha imekuwa changamoto kubwa sana kwenye zama tunazoishi sasa. Tunapoteza muda na maisha yetu kwenye kufanya kazi ngumu, lakini fedha tunazozipata tunazipoteza kwa kununua vitu ambavyo siyo mahitaji ya msingi.

Makampuni makubwa yanatumia mbinu za kisaikolojia kututangazia bidhaa na huduma zao kwa namna ambayo tunajisikia vibaya kama hatuna wanachouza.

Pia taasisi za fedha zimerahisisha sana matumizi yetu, hata kama mtu huna fedha za kununua kitu, basi ni rahisi kukopa fedha ili kununua unachotaka. Na hapo sasa mtu analipa mkopo pamoja na riba kubwa.

Yote haya ni matatizo ya kujitakia, kwa kushindwa kudhibiti tamaa zetu na kujilinganisha na wengine.

Ili kuondokana na changamoto hii ya fedha, fanya yafuatayo;

  1. Jua mahitaji yako ya msingi ambayo utayagharamia na yale ya anasa ambayo utaachana nayo. Mahitaji ya msingi ni manne, maji, chakula, moto na malazi. Mengine yoyote nje ya hapo ni anasa, yanaweza kusubiri.
  2. Kuwa na bajeti ya matumizi yako ya fedha, usitumie tu fedha kwa sababu unazo, bali weka bajeti na ifuate hiyo.
  3. Usikope fedha kwa ajili ya matumizi, ni kuchagua kupoteza fedha.
  4. Kwenye kila kipato unachoingiza, sehemu ya kumi hupaswi kuitumia kabisa, hivyo ni fedha unayojilipa kwa ajili ya uwekezaji wako wa baadaye.
  5. Usishindane na watu wengine wala kujilinganisha na yeyote kwenye mali, mavazi na hata maisha.
  6. Fanya tahajudi rahisi kabla hujanunua kitu. Kabla hujalipia jiulize je unachotaka kulipia ni hitaji la msingi au anasa. Hii itakuepusha kufanya manunuzi yasiyo muhimu.
  7. Fanya mfungo wa matumizi. Kwa mwezi mmoja, usinunue kabisa kitu ambacho siyo cha msingi. Jizuie kabisa kununua chochote ambacho siyo lazima kwa kipindi cha mwezi mzima, kisha ona jinsi maisha yako yatakuwa bora zaidi.
  8. Wekeza akiba yako kwenye maeneo ambayo yanazalisha zaidi baadaye.
  9. Usinunue vitu ambavyo thamani yake inashuka kadiri muda unavyokwenda.
  10. Ongeza kipato chako kwa kuwa bora zaidi kwenye kile unachofanya, toa huduma bora zaidi, wahudumie wengi zaidi na utaweza kuongeza kipato zaidi.

CHANGAMOTO YA 10; KUKOSA KUSUDI LA MAISHA.

Watu wengi wamekuwa wanaenda maisha yao kama misukule. Tangu wanazaliwa mpaka wanakufa hawajawahi kuishi maisha yao bali wanaishi maisha ya wengine.

Wanapozaliwa wazazi wanawaelekeza jinsi ya kuishi wakiwa watoto, na wanafuata maelekezo ya wazazi. Wanapoenda shule walimu wanawaelekeza jinsi ya kuishi na wanafuata maelekezo ya walimu. Wanapoingia kwenye kazi waajiri wanawaelekeza jinsi ya kuishi na wanafuata maelekezo yao. Na hata kwenye jamii, watu wanaelekezwa jinsi ya kuishi kulingana na wengine wanavyoishi kwenye jamii na wanafuata maelekezo hayo.

Kwa hali hii, tangu mtu anazaliwa mpaka anazeeka hajawahi kutafakari na kuchagua kuishi maisha anayotaka yeye, bali amekuwa anafanya kile anachoambiwa au ambacho wengine wanafanya.

Haishangazi kwa nini maisha ya wengi yana msongo. Unakuta watu wana maisha mazuri kwa nje, lakini ndani yao kuna ombwe kubwa ambalo wanajaribu kulijaza kwa kununa vitu mbalimbali vya starehe lakini ombwe hilo halijai.

Ombwe hili linajazwa na mtu kulijua na kuishi kusudi lake kwenye maisha, na kuacha kuishi kama wengine wanavyomwambia aishi.

Ili kujua na kuishi kusudi la maisha yako, zingatia yafuatayo;

  1. Tambua kwamba wewe ni shujaa wa maisha yako, acha kushabikia ushujaa wa wengine na anza kujikubali wewe mwenyewe.
  2. Pata picha kubwa ya maisha yako, wewe ni nani, uko hapa duniani kufanya nini na unaacha alama gani hapa duniani. Unapaswa kujiuliza maswali haya na kujipatia majibu.
  3. Kuwa na utaratibu wa kuandika kuhusu maisha yako kila siku. Kuwa na kijitabu ambapo kila mwisho wa siku unaandika yale uliyokutana nayo kwenye siku hiyo na jinsi ulivyoiishi. Kisha pata muda wa kurudia kusoma yale uliyoandika na utaweza kuona vitu vinavyojirudia zaidi kwenye maisha yako.
  4. Sikiliza sauti yako ya ndani. Kila mmoja wetu ana sauti yake ya ndani, sauti ambayo inajua kilicho sahihi kwa mtu. Wengi wamekuwa wanaipuuza na kuikandamiza sauti hii. Wewe isikilize na itakuongoza vizuri.
  5. Tenga muda wa kuwa na wewe peke yako. Zoezi la kujitambua wewe mwenyewe ni zoezi endelevu. Hujitambui siku moja halafu maisha yako yote ukayaendesha kwa utambuzi ulioupata mara moja, bali kila siku ni nafasi ya wewe kujijua zaidi. Hivyo tenga muda wa kuwa peke yako, ambapo utayatafakari maisha yako na kuweza kuona unakotoka, ulipo na unapokwenda. Ni katika tafakari hizi utaweza kujisikiliza na kujua kilicho sahihi kwako kufanya.

Rafiki, hizo ndiyo changamoto 10 kubwa zinazotukabili kwenye maisha tunayoishi na jinsi ya kuzitatua. Fanyia kazi haya uliyojifunza ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi.

#3 MAKALA YA JUMA; NJIA SAHIHI YA KUKABILIANA NA MSONGO WA MAWAZO.

Msongo wa mawazo ni janga kubwa sana kwenye zama tunazoishi sasa. Mazingira yetu yamekuwa kichocheo kikubwa cha msongo wa mawazo.

Kwanza kabisa mambo tunayotaka kufanya lakini muda tulionao ni mchache. Pili vifaa vyetu vya kielektroniki na mitandao ya kijamii kila wakati vinatupigia kelele.

Kwa njia hii mtu kupata muda tulivu wa kuishi maisha yake imekuwa vigumu na hivyo msongo umekuwa juu.

Msongo usiokuwa na ukomo ni chanzo cha afya kudhoofu na hata kuchochea magonjwa ya akili, kansa, shinikizo la damu na magonjwa mengine sugu.

Kwenye makala ya juma hili, nilikushirikisha njia sahihi za kukabiliana na msongo ili uweze kuwa na maisha tulivu, yenye amani na furaha kubwa.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ya juma, isome sasa hapa kabla msongo haujaendelea kukuathiri. Fungua; Njia Sahihi Za Kukabiliana Na Msongo Wa Mawazo Katika Zama Tunazoishi Sasa, Ambapo Mambo Ni Mengi Na Muda Ni Mchache.

Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku ili upate maarifa sahihi ya kukuwezesha kupiga hatua zaidi kwenye maisha.

#4 TUONGEE PESA; MAISHA ULIYOPOTEZA.

Watu wengi wamekuwa wanakutana na hali hii, akiwa hana fedha anakuwa na mawazo na mipango mizuri sana ya kutekeleza anapopata fedha. Anakuwa mpole na mwenye akili nzuri juu ya matumizi ya fedha. Akiona wengine wanatumia fedha vibaya anajiambia kama mimi ningepata fedha hizo, basi ningefanya mambo mazuri sana.

Lakini mtu huyo huyo anapopata fedha, anajikuta anafanya vitu ambavyo hata hakupanga kufanya. Mtu akishapata fedha zile akili nzuri na mipango aliyokuwa nayo anasahau kabisa. Anajikuta ananunua vitu ambavyo hakupanga kununua, mahitaji muhimu ambayo hayakuwepo awali yanaanza kujitokeza. Ni mpaka fedha hiyo inapoisha ndiyo mtu anarudi kwenye akili zake na kujiuliza zile fedha zimeishaje bila kufanya mambo mazuri.

Kama umewahi kukutana na hali kama hii usijione kama una bahati mbaya, au ni mjinga sana inapokuja kwenye fedha. Jua hiyo ni hali inayowakumba watu wengi kwenye fedha, na inatokana na wengi kutokuielewa vizuri saikolojia ya fedha. Fedha ni nguvu, na nguvu yoyote isipodhibitiwa na kutumiwa vizuri inaleta uharibifu.

Leo nakwenda kukushirikisha dhana itakayokuwezesha kuwa na udhibiti mzuri kwenye fedha zako, dhana itakayokuzuia usitumie hovyo fedha pale unapokuwa nazo.

Dhana hii ni kuhesabu fedha kwa kulinganisha na maisha ambayo umepoteza kupata fedha hizi. Wote tunajua kwamba muda ni fedha, na pia tunajua kwamba muda ni maisha, hivyo basi maisha pia ni fedha.

Sasa chukua kipato chako unachopata kwa mwezi, kisha gawa kwa masaa unayofanya kazi. Mfano kama kipato chako ni milioni moja, halafu unafanya kazi masaa 8 kwa siku, siku 5 au 6 za wiki, kwa mwezi unafanya kazi kwa masaa 160 mpaka 200. Ukigawa milioni moja kwa masaa 200 utapata shilingi elfu 5. Hii ina maana kila saa unayofanya kazi unalipwa shilingi elfu 5.

Sasa kwa sababu muda ni fedha na maisha ni muda hivyo maisha ni fedha, kila elfu 5 unayoipata, unapoteza saa moja ya maisha yako. ukipata elfu 10 umepoteza masaa mawili.

Sasa kila unapotaka kununua kitu, kabla hujafanya maamuzi ya kukinunua jiulize kwanza swali hili, je kitu hiki ninachokwenda kununua, kina thamani sawasawa na maisha niliyopoteza?

Kwa mfano umekutana na nguo ambayo inauzwa shilingi elfu 20, umeipenda kweli na unataka kuinunua. Jiulize kwanza je nguo hii ina thamani sawa na masaa manne ya maisha yangu? Je kama nikiambiwa nichague kupata nguo hii na kupata masaa manne zaidi kwenye maisha yangu nitachagua nini?

Kwa kuchukulia fedha zako kama maisha ambayo unapoteza, utajijengea nidhamu kubwa sana ya fedha na kuacha matumizi ya hovyo, yasiyo na manufaa kwako. Pia utapata muda zaidi wa kufanya yale muhimu kwako, pamoja na kuwekeza fedha zako maeneo ambayo yanazalisha na hivyo kukusaidia usifanye kazi muda mrefu kupata fedha za kupoteza.

Linganisha kila fedha unayotaka kutumia na maisha unayopoteza, na utaona jinsi gani vitu vingi unavyopenda kununua havina thamani unayovipa.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; WEWE NI KILE UNACHOKULA.

You are what you eat, so ingest the best stuff and wake up. This means taking some time to find books, films, shows, magazines, audiobooks, lectures, or whatever else you feel is going to help you grow. Use your valuable time to enhance your human experience and to learn new things. – Pedram Shojai

Ipo kauli maarufu kwamba wewe ni kile unachofikiri, au aliwazalo mtu ndiyo linalomtokea. Huu ni ukweli usiopingika.

Lakini pia wewe ni kile unachokula, kila unachoruhusu kiingie kwenye mwili wako, kinaenda kufanywa kuwa sehemu ya mwili huo.

Chakula unachokula kinaenda kumeng’enywa na kuingia kuwa sehemu ya mwili wako.

Lakini pia taarifa na maarifa unayoruhusu yaingie kwenye akili yako yanaenda kuwa sehemu ya akili na mwili wako.

Kwa kujua ukweli huu, unapaswa kuwa mwangalifu sana kwa vitu unavyoruhusu viingie kwenye mwili na akili yako.

Kula vyakula ambavyo ni safi na salama kiafya. Usile vyakula vyenye sumu au visivyo na virutubisho sahihi. Ukila vyakula vibaya unakuwa mtu mbaya. Ukila vyakula vizuri unakuwa mtu mzuri. Matatizo makubwa ya kiafya ambayo wengi wanayapata sasa ni matokeo ya kula vyakula ambavyo siyo vizuri.

Chuja sana maarifa na taarifa zinazoingia kwenye akili yako. Usiruhusu kila kitu kiingie, linda sana akili yako na uchafu mwingi unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Chagua kufuatilia maarifa na taarifa za kujenga na kutia moyo na siyo za kubomoa na kukata tamaa.

Wewe ni kile unachokula, hakikisha kila kinachoingia kwenye mwili na akili yako umekikagua kwa umakini mkubwa na kutambua ndiyo kitu sahihi kabisa kwa maisha yako.

Rafiki, hizi ndiyo tano za juma, tano ambazo zinatuwezesha kuwa na maisha tulivu, yenye furaha na mafanikio makubwa. Kilichobaki ni sisi kuchukua hatua, kutafuta majibu ndani yetu, kuwa watawa wa mjini, kuondokana na msongo, kupima fedha zetu kwa maisha tunayopoteza na kuchagua sana kila kinachoingia kwenye mwili na akili zetu. Wewe ndiye mwamuzi wa mwisho wa maisha yako, fanya maamuzi sasa ili uwe na maisha bora.

Kwenye #MAKINIKIA nitakwenda kukushirikisha hatua za kuchukua ili kuweza kuwa na maisha bora kabisa kwenye maeneo haya kumi yenye changamoto kwa kila mmoja wetu.

#MAKINIKIA yanapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA telegram, hivyo kama bado hujajiunga fuata maelekezo ambayo yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu