“If you find something very difficult to achieve yourself, don’t imagine it impossible—for anything possible and proper for another person can be achieved as easily by you.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 6.19

Tushukuru kwa nafasi hii nyingine ambayo tumeipata leo.
Siyo wote ambao walipanga kuiona siku hii wameweza kuiona.
Ila kwa baraka sisi tumeiona, tena bila hata ya kulipia chochote.
Lakini siku hii tuliyopewa leo ni deni kwetu, deni la kwenda kuweka juhudi kubwa za kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari HATA WEWE UNAWEZA PIA…
Kama kuna kitu unataka kufanya kwenye maisha yako na ukaona ni kigumu kwako, usikimbilie kukubaliana nacho kwamba ni kigumu.
Badala yake angalia kama kuna mtu mwingine ambaye ameweza kukifanya.
Na kama yupo mtu mwingine ambaye ameweza kukifanya, hata wewe unaweza kukifanya pia.
Na pia kama hakuna ambaye ameweza kukifanya, kwa nini wewe usiwe wa kwanza kukifanya na ukafungua njia kwa wengine?

Unataka kufanya biashara ukiwa kwenye ajira lakini unaona ni vigumu, waangalie wengine wanaofanya hivyo na utaona inawezekana kabisa.
Unataka kuanza biashara kwa mtaji kidogo au bila ya mtaji kabisa, wapo wengi wamefanya hivyo kwa hiyo inawezekana kabisa.
Unataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako licha ya kuanzia chini kabisa, wengi wameweza kufanya hivyo, kwa hiyo inawezekana.

Vitu vingi unavyojiambia ni vigumu na haviwezekani, unaona hivyo kwa sababu umechagua kuona ugumu.
Lakini ukichagua kuona upande mwingine, upande ambao unawezekana, utaona njia bora ya kuweza kufanya kile unachotaka kufanya.

Na pia unapowaona watu ambao wamepiga hatua kuliko wewe, badala ya kuwaonea wivu kwa nini wao wamefanikiwa na wewe hujafanikiwa, furahia mafanikio yao na jiambie kama wao wameweza na mimi nitaweza pia.

Ukawe na siku bora ya leo, siku ya kutumia mafanikio ya wengine kama hamasa ya wewe kupiga hatua zaidi.
#WalichowezaWengineUnawezaPia #FurahiaMafanikioYaWengine #HakunaKinachoshindikana

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1