Mafanikio siyo magumu kama wengi wanavyofikiri, mafanikio ni rahisi sana kama utachagua kuyaishi maisha yako.

Mafanikio yanakuwa magumu kwa wengi kwa sababu wanajaribu kuwa watu ambao siyo, kwa kujilinganisha na watu wengine ambao hawawezi kuwa kama wao.

Unapochagua kuwa wewe, unapochagua kuishi maisha yenye maana kwako, mafanikio ni kitu ambacho lazima kitokee kwako.

Swali linakuwa siyo kama utafanikiwa au la, bali swali linakuwa ni muda, kwamba lazima utafanikiwa.

Leo nakushirikisha maeneo matatu ya kuweka nguvu zako ambayo yatakuhakikishia kufanikiwa sana kwenye maisha yako. Na mafanikio haya ni kwa kipimo chako mwenyewe na siyo kipimo cha mtu mwingine yeyote.

Kazi.

Eneo la kwanza la kuweka mkazo ni kazi. Unapaswa kufanya kazi ambayo unapenda kuifanya, ambapo upo tayari kujituma zaidi katika kuifanya na kila wakati unajifunza na kuwa bora kabisa kwenye kuifanya kazi hiyo.

Hakuna mafanikio bila ya kazi, na kama unafanya kazi usiyoipenda, wewe mwenyewe unakuwa kikwazo kwa mafanikio yako. Huwezi kufanikiwa kwa kuchukia kazi unayoifanya.

Huduma.

Kiwango chako cha mafanikio ni sawa sawa na ukubwa wa watu unaowahudumia. Hivyo ili kufanikiwa zaidi unahitaji kutoa huduma bora kwa wengi zaidi. Kuwa mtu wa huduma, yatoe maisha yako kufanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

Kwa chochote unachofanya, jiulize unayafanyaje maisha ya wengine kuwa bora zaidi ya yalivyo sasa. Kazana kuwa wa huduma kwa wengi, kwa kutoa thamani kubwa na kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

Mfanye yeyote anayekutana na wewe au kukutana na kazi zako kuwa bora zaidi kuliko alivyokuwa kabla.

Furaha.

Watu wengi huwa wanafikiri wakishafanikiwa basi watakuwa na furaha sana, na wanakazana kufanikiwa lakini furaha hawaioni. Rafiki, unaanza na furaha ndiyo unafanikiwa. Hivyo kama huna furaha kabla hujafanikiwa, hata ukifanikiwa hutakuwa na furaha. Furaha siyo matokeo ya mafanikio, bali mafanikio ni matokeo ya furaha.

Anza ukiwa na furaha, anza kwa kuyafurahia maisha yako, anza kwa kufurahia kile unachofanya, wafurahie wale wanaokuzunguka na furahia kila hali unayopitia. Kwa kuanza na furaha, unaona fursa nzuri kwenye kila unachogusa na kuweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Unapokuwa kwenye hali ya kutokuwa na furaha jiulize nini kinachangia hilo na jikumbushe vile vitu vinavyokupa furaha kwenye maisha yako. Hali yako ya furaha ni moja ya vitu unavyopaswa kuvisimamia kwa karibu sana kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha