Sisi binadamu huwa tunapenda sana uhakika kwenye kitu chochote tunachofanya.

Hii ndiyo sababu watu wapo tayari kukaa kwenye kazi inayowalipa kidogo na wasiyoipenda kwa sababu tu kipato ni cha uhakika.

Wakati watu hao hao wangeweza kuingia kwenye biashara ambayo inaweza kuwalipa zaidi, lakini kwa kuwa hakuna uhakika wa kipato kwenye biashara, wengi huhofia.

Hatua ya kwanza ya wewe kufikia mafanikio makubwa ni kuondokana na dhana ya kutaka uhakika kwenye yale unayofanya.

Kubaliana na hali ya kutokuwa na uhakika, kwa kila kitu kipya na kikubwa unachotaka kufanya, kubali kwamba huwezi kuwa na uhakika wa asilimia 100.

Kitu kikishakuwa cha uhakika, kila mtu anakifanya na hakiwezi tena kukupa mafanikio.

Mafanikio makubwa yapo kwenye vitu ambavyo siyo vya uhakika, vitu ambavyo vina hatari fulani ya kushindwa au kukosa.

Wale wanaokuwa na uthubutu wa kufanya vitu hivyo ndiyo wanaopata manufaa makubwa.

Jua udhaifu huu mkubwa uliopo ndani ya kila mmoja wetu, kupenda uhakika, ili kujua jinsi ambavyo kila kitu kitakwenda na mpaka matokeo ya mwisho yatakavyokuwa.

Jua kitu kikishakuwa na uhakika, hakiwezi tena kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Hata akili yako yenyewe, inafanya kazi kwa umakini mkubwa pale ambapo kitu kinakuwa siyo cha uhakika kuliko kitu kinapokuwa cha uhakika. Kitu kinapokuwa cha uhakika, akili inafanya kwa mazoea.

Mfano kama umeajiriwa na kipato ni cha uhakika kila mwezi, utafanya kazi yako kwa mazoea, kwa sababu unajua kipato ni uhakika na hakiathiriwi na jinsi unavyofanya kazi zako za kila siku.

Lakini unapokuwa kwenye biashara yako ambayo kipato siyo cha uhakika, utajisukuma kufanya zaidi, kutafuta wateja wapya, kutoa huduma bora kwa wateja wako ili kuweza kuongeza kipato. Na hatua hizo zitakuwezesha kupiga hatua zaidi na kufanikiwa zaidi.

Ondokana na dhana ya kutaka uhakika, ndiyo inakuchelewesha kufikia mafanikio makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha