#TANO ZA JUMA #24 2019; Kanuni Za Zamani Hazifanyi Kazi, Tabia Sita Zitakazokufikisha Kwenye Mafanikio Makubwa, Sifa Nne Za Kazi Yenye Maana Kwako, Kusema Ndiyo Na Kusema Hapana Na Mwanzo Wa Safari Ya Kuelekea Kwenye Ukuu.

Rafiki yangu mpendwa,

Juma namba 24 la mwaka huu 2019 siyo letu tena, tumekuwa na siku saba, sawa na masaa 168 ambayo tumeyatumia kama tulivyoyatumia. Muda huo uliopita hautarudi tena, bali tutanufaika na zile hatua tulizochukua pamoja na yale tuliyojifunza.

Nachukua nafasi hii kukukaribisha kwenye TANO ZA JUMA, ambapo ninakukusanyia maeneo matano muhimu ya kujifunza kutoka kwenye kitabu nilichokisoma na kukichambua kwa kina. Hapa unajifunza, kuhamasika na kuondoka na hatua za kwenda kuchukua ili kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Kama hakuna kikubwa ulichofanya kwa juma hili, basi angalau soma hapa na uondoke na mambo utakayokwenda kufanya na kubadili sana maisha yako kwa siku zijazo.

Juma hili tunakwenda kujifunza kuhusu tabia zinazowawezesha watu waliofanikiwa kufanikiwa zaidi. Kuna watu ambao wanafanikiwa kidogo halafu wanaishia hapo. Lakini wapo wanaofanikiwa, na wanazidi kufanikiwa zaidi. Kumbe kuna kitu kinachowatofautisha wanaofanikiwa mara moja na wanaofanikiwa zaidi na zaidi. Na kitu hicho ni tabia ambazo watu wanakuwa wamejijengea.

Katika kujifunza tabia hizi, tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa High Performance Habits: How Extraordinary People Become That Way ambacho kimeandikwa na kocha wa mafanikio Brendon Burchard. Kwenye kitabu hiki, Brendon ametushirikisha hatua sita za kujijengea kama tunataka kufanikiwa zaidi. Pia ametutahadharisha na tabia tatu zinazoharibu kabisa mafanikio yetu na tabia moja kuu inayobeba tabia zote za mafanikio.

high performance 1

Karibu kwenye tano za juma, uzijue tabia hizo muhimu za kukuwezesha kufanikiwa zaidi na zaidi.

#1 NENO LA JUMA; KANUNI ZA ZAMANI HAZIFANYI KAZI.

Kanuni za zamani za mafanikio kwa sasa zimekuwa hazifanyi tena kazi kama zamani. Na hili limekuwa linafanya wengi kuwa katika hali ya kuvurugwa.

Watu wanajifunza kanuni hizo za mafanikio, ambazo zote zimejengwa kwenye msingi wa fanya kazi kwa juhudi, penda sana unachofanya, jitume kuliko wengine, kuwa na shukrani na kuweka mkazo kwenye ubora wako na siyo madhaifu yako.

Kanuni hizo hazifanyi kazi siyo kwa sababu siyo sahihi, ni sahihi sana, na unapokuwa unaanza, kanuni hizo zinakuwezesha kujijengea msingi sahihi.

Lakini kuna hatua unafika, kanuni hizo hazifanyi kazi tena. Hapo ndipo wengi wanapokuwa wamekwama. Kwa sababu wanajua kanuni iliyowafikisha pale walipofika, lakini kadiri wanavyoifanyia kazi haileti tena yale matokeo waliyotegemea kupata.

Mfano wakati mtu anaanza kazi au biashara, kadiri anavyoweka kazi zaidi ndivyo anapata matokeo mazuri zaidi, na hayo yanamwezesha kukua zaidi. Lakini anafika hatua fulani ya mafanikio ambayo kadiri anavyoweka kazi zaidi haileti tena matokeo makubwa zaidi.

Hapo ndipo mtu anahitaji vitu vingine ili apige hatua zaidi. Na kinachohitajika katika hatua hii ni tabia ambazo mtu anakuwa nazo.

Watu wengi wamekuwa wanaiishi misingi ya mafanikio, lakini hawajali sana kuhusu tabia zao binafsi. Wasichojua ni kwamba, kadiri unavyofanikiwa, ndivyo tabia zako binafsi zinavyokuwa na athari kwenye mafanikio yako.

Hivyo kama umefika hatua ya maisha yako, ambapo umekazana kuiishi misingi ya mafanikio, na mwanzo ilikusaidia ila kwa sasa unaona haikusaidii tena, suluhisho siyo kuacha misingi hiyo, bali suluhisho ni kujijengea tabia bora zaidi.

Unapoiishi misingi ya mafanikio, halafu ukajijengea tabia bora, utaweza kufanikiwa sana. Hatua unazochukua zinaleta matokeo makubwa sana pale ambapo unakuwa na tabia sahihi zinazobeba misingi hiyo.

Kwenye kitabu cha juma hili, tunakwenda kujifunza tabia sita unazopaswa kuziishi kama unataka kufanikiwa zaidi. Tabia tatu ni za kwako binafsi zinazohusiana na wewe na tabia tatu ni za kijamii, ambazo zinagusa maisha ya wengine pia.

Jipe muda wa kujifunza tabia hizo sita na hatua za kuchukua kwa kila tabia ili uweze kufanikiwa zaidi. Kumbuka, kikwazo pekee kwa mafanikio yako ni wewe mwenyewe. Ukiweza kujijengea tabia bora, utaacha kuwa kikwazo kwako mwenyewe.

#2 KITABU CHA JUMA; TABIA SITA ZITAKAZOKUFIKISHA KWENYE MAFANIKIO MAKUBWA.

Rafiki, kama nilivyokushirikisha kwenye NENO LA JUMA misingi inakuanzisha kwenye safari ya mafanikio, lakini tabia ndiyo zinazokufikisha kwenye kilele cha mafanikio. Misingi inatupa mafanikio binafsi kwenye maeneo machache ya maisha yetu, lakini tabia zinatupa mafanikio makubwa na yanayowahusisha wengine pia.

Kwenye kitabu chake cha High Performance Habits: How Extraordinary People Become That Way, Brendon Burchard anatushirikisha tabia sita zitakazotuwezesha kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yetu.

high performance 2

Brendon anatushirikisha tabia hizi kutokana na uzoefu wake binafsi, baada ya kuwakochi watu wenye mafanikio makubwa. Lakini pia ameingia kwenye tafiti nyingi za kisayansi na kijamii na kuweza kuona mchango wa tabia hizo kwenye mafanikio. Kupitia uzoefu huo binafsi na matokeo ya tafiti, Brendon anatudhibitishia kwamba tukiweza kuziishi tabia hizi sita, tutaweza kuwa na mafanikio makubwa sana.

Brendon anatushirikisha tabia hizo sita, pamoja na hatua tatu za kuchukua kwenye kila hatua ili ziweze kuwa na manufaa kwenye maisha yetu. Tabia hizi sita amezigawa kwenye makundi mawili, kundi la kwanza ni tabia binafsi na kundi la pili ni tabia za kijamii.

Karibu kwenye uchambuzi huu wa kina wa kitabu cha High Performance Habits, ujifunze tabia sita za mafanikio makubwa na hatua za kuchukua ili maisha yako yawe bora zaidi.

TABIA BINAFSI.

Kundi la kwanza la tabia sita za mafanikio ni tabia binafsi, ambazo zinamhusisha mtu peke yake. Hapo chini kuna tabia tatu zilizopo kwenye kundi hili.

TABIA YA KWANZA; TAFUTA UWAZI.

Tabia ya kwanza na muhimu sana kwenye mafanikio yako ni kutafuta uwazi.

Unatafuta uwazi kwa kujijua wewe mwenyewe vizuri, yaani misingi unayosimamia, uimara wako na hata madhaifu yako.

Pia unakuwa na uwazi pale unapojua nini hasa unataka kwenye maisha yako, maono yako makubwa pamoja na malengo uliyonayo kwenye maisha yako.

Lakini pia uwazi unahusisha kujua jinsi ambavyo utafikia maono na malengo yako, yaani mipango unayofanyia kazi ili kufika kule unakotaka kufika.

Kama hujijui wewe mwenyewe, hujui unakokwenda na hujui unafikaje, haijalishi unachukua hatua kubwa kiasi gani, huwezi kufikia mafanikio makubwa.

Hatua tatu za kuchukua kwenye tabia ya kwanza;

Moja; tengeneza maono yako kwenye maeneo manne muhimu ya maisha yako.

Eneo la kwanza ni maisha binafsi, hapa unapaswa kuwa na maono yako binafsi, unataka kuwa nani. Jione kama tayari umeshafika kule unakotaka kufika na endesha maisha yako kama tayari umeshafanikiwa.

Eneo la pili ni maisha ya kijamii, hapa unahitaji kuwa na maono ya jinsi unavyogusa maisha ya wengine kwenye jamii. Unajiona jinsi unavyohusiana na wengine na kuendesha maisha yako kwa maono hayo.

Eneo la tatu ni ujuzi unaohitaji kuwa nao ili kufanikiwa. Kwa kile unachotaka kufikia kwenye maisha, jua ni ujuzi gani unaopaswa kuwa nao ili kukifikia, kisha jijengee ujuzi huo.

Eneo la nne ni huduma unayotoa kwa wengine, hapa unajiona jinsi ambavyo unatoa huduma yako kwa wengine na wananufaika sana na huduma hiyo. Kila hatua unayochukua leo inakuwa na lengo la kukuwezesha kutoa huduma bora zaidi siku zijazo.

Mbili; amua hisia unazotaka kuwa nazo.

Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia, huwa tunasukumwa kuchukua hatua kulingana na hisia tunazokuwa nazo.

Ili kupata uwazi kwenye maisha yako, lazima uamue ni hisia za aina gani unataka kuwa nazo. Kwa sababu usipoamua hisia unazotaka na kuzitengeneza, dunia itakupa hisia ambazo zitakuwa kikwazo kwako kufanikiwa.

Chagua kuwa na hisia za upendo, hisia za furaha, hisia za utulivu na amani na epuka kuwa na hisia za hofu, chuki na wivu.

Tatu; jua kile chenye maana kwako.

Uwazi kwenye maisha unakuja pale unapojua kile chenye maana kwenye maisha yako na kuzingatia hicho.

Kila unachofanya kwenye kazi au biashara kinapaswa kuendana na maana unayotaka kutengeneza kwenye maisha yako.

Katika kutengeneza maana, unapaswa kuangalia sifa hizi nne, HAMASA, MAHUSIANO, KURIDHIKA na UMUHIMU. Zisome sifa hizi kwa kina kwenye makala ya juma hapo chini.

TABIA YA PILI; TENGENEZA NGUVU.

Mafanikio yako ni matokeo ya nguvu ulizonazo. Huwezi kufanikiwa kama huna nguvu, kwa sababu safari ya mafanikio siyo rahisi kama wengi wanavyofikiri.

Kitu ambacho wengi hawajui ni kwamba nguvu hazitokei tu kwenye maisha yako, bali zinatengenezwa. Jinsi unavyoendesha maisha yako, kuanzia kulala kwako, ulaji wako na hata matumizi yako ya muda wa siku yana athari kubwa sana kwenye nguvu zako.

Pia tunapozungumzia nguvu, wengi hufikiria nguvu za mwili pekee, lakini nguvu zinahusisha pia akili na hisia pia. Unaweza kuwa na nguvu nyingi za mwili, lakini akili ikawa haina nguvu na usiweze kuchukua hatua. Au mwili na akili vikawa na nguvu huna hamasa kabisa kwa sababu nguvu za kihisia unakuwa huna.

Ili ufanikiwe sana, unahitaji kuwa na kiwango kikubwa cha nguvu kimwili, kiakili na kiroho (hisia). Na nguvu hizi zinatengenezwa kwa jinsi unavyoyaendesha maisha yako.

Hatua tatu za kuchukua ili kutengeneza nguvu zaidi kwenye maisha yako.

Moja; achia msongo weka nia.

Msongo wa mawazo ni sumu kubwa sana kwenye nguvu yako, ni kitu kinachoua kabisa nguvu yoyote uliyonayo ndani yako.

Na msongo wa mawazo umekuwa hautokei tu, bali tumekuwa tunauzalisha kwa jinsi tunavyoyaendesha maisha yetu. Na tunatengeneza sana msongo pale tunapotoka kwenye kufanya kitu kimoja kwenda kufanya kitu kingine.

Ili kuepuka kupoteza nguvu, tunapaswa kuchukua hatua ya kuachia msongo na kuweka nia kila tunapobadili kile tunachofanya.

Pale unapotoka kufanya kitu kimoja na kwenda kufanya kitu kingine, usiingie tu moja kwa moja kwenye kufanya. Badala yake funga macho yako kwa dakika moja au mbili, jiambie maneno ‘naachia msongo’ kwa kurudia rudia huku ukiuweka mwili wako kwa namna ya kuachia kilichopo. Unaposikia msongo umetoka kwenye mwili wako, weka nia ya kile unachokwenda kufanyia kazi. Fikiria ni hisia gani unataka kuwa nazo kwenye kufanya kitu hicho na matokeo unayotegemea kupata.

Kwa kufanya zoezi hili litakalokuchukua dakika 2 mpaka 5 utapata nguvu kubwa ya kuingia kwenye kitu kipya huku ukiachana na msongo wa kile ulichomaliza kufanya.

Mbili; tengeneza furaha.

Furaha ni kitu ambacho tunakitengeneza au kukipoteza sisi wenyewe, siyo kitu ambacho kinatokea au kutafutwa. Kutengeneza furaha yako mwenyewe ni moja ya njia za kutengeneza nguvu zaidi kwenye maisha yako. Kwani unapokuwa na furaha unakuwa na hamasa zaidi ya kuchukua hatua na kupiga hatua.

Unatengeneza furaha kwa kuwa na hisia chanya kwenye maisha yako. Kupenda kile unachofanya, kuwapenda wengine, kuwa mtu wa shukrani ni hisia chanya ambazo zinakuletea furaha zaidi.

Pia unatengeneza furaha kwa kutawala akili yako na fikra chanya za yale mazuri unayotaka na kutengeneza taswira ya matokeo unayotaka kupata na kujikumbusha taswira hiyo mara kwa mara.

Tatu; boresha afya yako.

Afya ni eneo muhimu sana la nguvu zako. Bila ya afya imara huwezi kuwa na nguvu. Ili kuboresha afya yako unahitaji kuweka mkazo kwenye maeneo haya matatu muhimu sana.

Eneo la kwanza ni ulaji, kula kwa afya, kula kiasi na kula vyakula ambavyo siyo sumu kwako. Epuka kabisa sukari, ni kitu ambacho kinakuondolea nguvu kwa haraka sana. kula kiwango kidogo cha wanga, kula mafuta, protini na mboga mboga kwa wingi.

Eneo la pili ni ufanyaji wa mazoezi. Kazi za wengi kwa sasa zinahusisha kukaa kwa muda mrefu, kama hufanyi mazoezi, ukaaji wako unapoteza nguvu. Hivyo kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi angalau kwa nusu saa kila siku. Unapofanya mazoezi, mwili unatumia vyakula ilivyohifadhi kuzalisha nguvu zaidi.

Eneo la tatu ni kulala. Usingizi ni kiungo muhimu sana cha nguvu zako. Kama hupati usingizi wa kutosha huwezi kuwa na nguvu, kila wakati utajiona umechoka kimwili na kiakili. Tafiti zinaonesha mtu anahitaji masaa 7 mpaka 8 ya kulala ili kuweza kupumzika vizuri. Hivyo pata usingizi wa kutosha ili kuwa na nguvu.

TABIA YA TATU; KUZA UMUHIMU.

Sisi binadamu huwa tunasukumwa kufanya kitu pale ambapo kinakuwa na umuhimu mkubwa. Bila ya kuwepo kwa umuhimu, hatupati msukumo wa kuchukua hatua. Mfano mzuri ni pale tunapokuwa na muda mrefu wa kufanya kitu, huwa hatupati msukumo wa kufanya, lakini muda unapofika ukomo, tunapata msukumo mkubwa wa kuchukua hatua.

Ili uweze kufanikiwa, unahitaji kuwa na msukumo mkubwa sana wa kuchukua hatua, inabidi uwe na shauku kubwa ya kupata kile unachotaka, ambayo itakusukuma kuchukua hatua bila ya kuchoka.

Utaweza kuwa na shauku hii kubwa iwapo utaweza kukuza umuhimu wa mafanikio unayofanyia kazi. Kile unachotaka kwenye maisha, kinapaswa kuwa ni muhimu kuliko vitu vingine vyote, hivyo utasukumwa kukifanya muda wote.

Umuhimu pia unakuwezesha kuvuka vikwazo na changamoto zilizopo kwenye safari ya mafanikio. Hakuna mafanikio rahisi, safari ya mafanikio ina vikwazo na magumu ya kila aina, kama kitu siyo muhimu zaidi kwako, kama hujajitoa kufa na kupona kukipata, hutaweza kukipata, maana mambo yatakuwa magumu sana kwako.

Katika kukuza umuhimu kwenye safari yako ya mafanikio, kuna hatua tatu muhimu za kuchukua.

Moja; jua nani anahitaji ubora wako wa hali ya juu.

Sisi binadamu huwa tunawajali sana wengine kuliko sisi wenyewe. Hivyo tunapojua kwamba kuna watu wanatutegemea, huwa tunajituma zaidi kuliko tunapokuwa hatuna wanaotutegemea.

Kupata umuhimu mkubwa wa wewe kuchukua hatua, tafuta mtu au watu ambao upo tayari kuwapigania, kwamba ukishindwa siyo tu umeshindwa wewe mwenyewe, bali pia umewaangusha na wengine pia.

Watu hao wanaweza kuwa familia yako na wale wanaokutegemea wewe, hawa wanakusukuma kujituma zaidi kwa sababu ukishindwa basi umewaangusha na wao pia.

Pia watu hao wanaweza kuwa wale wanaotegemea unachofanya, labda wateja wa huduma au bidhaa unayotengeneza, hawa wanakusukuma ufanye kwa ubora zaidi.

Muhimu ni uweze kuona kwamba hufanyi kwa ajili yako tu, bali wapo wanaotegemea sana wewe ufanye na hapo unapata msukumo mkubwa.

Mbili; jua KWA NINI yako.

Kila mtu ana sababu KWA NINI anafanya kile anachofanya, lakini wengi huwa hawajikumbushi KWA NINI yao na hivyo hamasa yao inashuka.

Kila wakati unapaswa kujikumbusha kwa nini yako, sababu kubwa ya wewe kufanya unachofanya na kwa nini ni muhimu upate matokeo unayofanyia kazi.

Weka wazi sababu zako za kutaka kufanikiwa, na hizo zitakusukuma zaidi. Kila siku yaandike maono na malengo makubwa unayofanyia kazi. Jiambie kwa maneno kile unachotaka na hilo linakufanya ujisukume zaidi.

Tatu; kuza kikosi chako.

Upo usemi kwamba wewe ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka, kwamba wale wanaokuzunguka wana mchango sana wa pale ulipo sasa. Kwa kujua nguvu ya wale wanaokuzunguka kwenye maisha yako, hakikisha unazungukwa na watu waliofanikiwa au wanapambana kufanikiwa.

Unapozungukwa na wale waliofanikiwa au wanaopambana kufanikiwa, unapata msukumo mkubwa wa wewe kufanikiwa pia.

Kila wakati kagua wale wanaokuzunguka, wale unaojihusisha nao kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla. Wanapaswa kuwa watu wenye mtazamo chanya na wanaopambana ili kufanikiwa.

Pia unapaswa kuwa na menta au kocha ambaye anakusukuma kufanikiwa zaidi. Mara nyingi mtu unapokuwa mwenyewe ni rahisi kuridhika na mafanikio madogo unayopata. Lakini unapokuwa na mtu mwingine anayekuangalia, ni rahisi kuona wapi unalegalega na kukusukuma zaidi.

TABIA ZA KIJAMII.

Kundi la pili kwenye tabia sita za mafanikio ni tabia za kijamii, tabia ambazo zinawahusisha watu wengine pia. Na hapo chini kuna tabia tatu za kundi hili.

TABIA YA NNE; ONGEZA UZALISHAJI (TIJA)

Watu wengi wamekuwa wanafikiri kwamba ili kufanikiwa unatakiwa kuwa ‘bize’ muda wote. Kuwa na mambo mengi ya kufanya. Lakini hili siyo kweli, kuwa ‘bize’ siyo kuzalisha au kuwa na tija.

Ili ufanikiwe unahitaji kuwa ‘bize’ kwa yale yenye umuhimu mkubwa kwako. Unahitaji kuwa na uzalishaji mzuri, kuleta tija kwenye maisha yako.

Msingi mkuu wa kuwa na tija ni kuwa na malengo na kuwa na nguvu na umakini wa kufanyia kazi malengo hayo. Kama huna malengo, huna umakini na huna nguvu, huna unapokwenda. Hatua zozote unachochukua ni kujichosha tu.

Kila hatua unayochukua lazima iwe ina lengo fulani, lazima kila unachofanya kiwe na matokeo ambayo yanakusogeza karibu na malengo yako. Kadiri unavyokuwa na malengo makubwa, yanayoeleweka na yanayopimika, ndivyo unavyosukumwa kuwa na tija zaidi.

Kitu muhimu zaidi kwenye uzalishaji na tija ni umakini wako. Tunaishi zama za kelele, zama ambazo kuna mambo mengi ya kufanya na muda ni mchache. Unapaswa kuyapangilia vizuri majukumu yako na siku yako kulingana na vipaumbele vyako ili usipoteze muda na nguvu kwa vitu visivyo muhimu.

Moja ya vitu ambavyo vimekuwa vinapunguza uzalishaji na tija kwa wengi ni jinsi wanavyofanya kazi zao. Mfano kufanya kazi mfululizo bila ya mapumziko ni kitu kinachochosha sana na kupunguza ufanisi. Ili kuondokana na hali hii, pangilia majukumu yako kwa namna ambayo utakuwa na mapumziko kila baada ya muda. Mpangilio mzuri ni kufanya kazi kwa dakika 50 kwa umakini mkubwa kisha kupumzika kwa dakika kumi, kisha kurudia tena hivyo. Unapopumzika unaondoka pale ulipo kaa, kujinyoosha na kufanya kitu cha tofauti. Lakini usiingie kwenye mitandao ya kijamii wakati wa mapumziko hayo.

Hatua tatu muhimu za kuchukua ili kuongeza tija kwenye maisha yako.

Moja; weka vipaumbele vyako vizuri.

Kila mtu ana vitu vingi sana vya kufanya kwenye siku yake. Lakini vitu vyote havina uzito sawa. Hivyo unapaswa kuweka vizuri vipaumbele vyako.

Katika kuweka vipaumbele kwanza anza na matokeo unayotaka kuzalisha kwenye maisha yako. Ukishajua matokeo unayotaka kuzalisha, jua ni majukumu yapi muhimu kwako kufanya ili kupata matokeo hayo, na majukumu hayo ndiyo yanakuwa kipaumbele chako.

Hufanyi kitu chochote ambacho hakikupeleki kwenye matokeo unayotaka, hata kama ni kizuri kiasi gani.

Safari yako ya mafanikio makubwa inaanza pale unapochagua machache ambayo yatachukua umakini na nguvu zako zote na kupuuza mengine yote, hata kama yanaonekana ni mazuri kiasi gani.

Mbili; chati hatua tano za kupata matokeo unayotaka.

Katika kupata matokeo unayotaka kwenye maisha yako, kuna mengi unahitaji kufanya. Ili kuwa na uzalishaji bora na tija, unahitaji kuchati hatua tano kubwa za kuchukua ili kufika kwenye matokeo unayotaka kupata.

Chukua lengo kubwa ulilonalo kisha jiulize swali hili, kama kuna hatua tano pekee za kuchukua ili kufikia lengo hili, zitakuwa hatua zipi?

Ukishajua hatua hizo tano muhimu, zipangie muda na weka kwenye kalenda na orodha yako ya mambo unayofanyia kazi. Kisha anza kuchukua hatua moja baada ya nyingine mpaka zikamilike hatua zote tano.

Umuhimu wa kugawa lengo kubwa kwenye hatua tano ni kulifanya lengo kubwa kuwa kwenye hatua ndogo ndogo unazoweza kufanyia kazi na pia kuweka vizuri vipaumbele vyako ili usipotelee kwenye usumbufu.

Tatu; kuwa vizuri kwenye ujuzi wa msingi.

Kile unachofanya, kuna ujuzi wa msingi ambao unapaswa kuwa nao. Sasa uzalishaji wako unategemea sana ubora na ustadi wako kwenye ujuzi huo.

Hivyo unapaswa kuweka kazi kuhakikisha unabobea kwenye ule ujuzi wa msingi wa kile unachofanyia kazi.

Kumbuka hakuna aliyezaliwa akiwa anajua chochote, kila kitu ambacho unaona wengine wanakijua jua wamejifunza. Hivyo na wewe pia unaweza kujifunza na kubobea kwenye ujuzi wowote unaohitaji.

Ukishajua unachotaka kwenye maisha yako, jua ujuzi unaohitaji ili kukifikia kisha kazana kuwa bora sana kwenye ujuzi huo.

Unaweza kubobea ujuzi wowote kama utakuwa tayari kujifunza, kuwa na kocha wa kukuongoza, kuwa na wengine unaoshindana nao na kuwa tayari kuwafundisha wengine.

TABIA YA TANO; TENGENEZA USHAWISHI.

Mafanikio yako ni matokeo ya ushawishi wako kwa wengine. Kadiri unavyokuwa na ushawishi kwa wengi ndivyo unavyoweza kufanikiwa zaidi.

Wale wenye ushawishi kwenye kazi ndiyo wanaopata nafasi za kupanda juu zaidi. Wenye ushawishi kwenye biashara ndiyo wanaopata wateja wengi zaidi. Na wenye ushawishi kwenye maisha ndiyo wanaokuwa na mahusiano bora zaidi.

Njia pekee ya kukuza ushawishi wako kwa wengine ni kuwafanya waone wewe uko upande wao na pia kuwafanya waweze kuwa bora zaidi ya walivyo sasa.

Hatua ya kwanza na muhimu kabisa kwenye kujenga ushawishi wako kwa wengine ambayo wengi hawaitumii ni kuwaomba watu hao wakusaidie kitu. Watu wengi hufikiri ushawishi unatokana na wewe kuwa mwongeaji sana, lakini ukweli ni kwamba ushawishi unatokana na watu kukufikiria wewe mara nyingi. Hivyo unapowaomba watu wakusaidie kitu hata kama ni kidogo, wanakufikiria na hivyo unakuwa na ushawishi kwao.

Ushawishi pia unatengenezwa kwa kutoa, pale unapowapa watu kitu bila ya kutegemea kupata chochote, unakuwa na ushawishi mkubwa kwa watu hao. Mtu anapopokea kitu kwako, tena kwa wakati ambao hakutegemea na bila ya kudaiwa kulipa chochote, anamfikiria sana yule aliyempa kitu hicho, na hivyo anakuwa ameshawishiwa.

Kuwajali wengine pia kunaongeza ushawishi wako kwao.

Zifuatazo ni hatua tatu muhimu katika kutengeneza ushawishi wako kwa wengine.

Moja; wafundishe watu jinsi ya kufikiri.

Kama utawafundisha watu jinsi ya kufikiri, yaani ukiathiri ufikiri wao, unakuwa na ushawishi kwao.

Kuna vitu vitatu ambavyo unapaswa kuwafundisha watu jinsi ya kufikiri, kuhusu wao wenyewe, kuhusu watu wengine na kuhusu dunia kwa ujumla.

Kupitia kazi unazofanya, hakikisha unawafundisha wengine jinsi ya kufikiri kwa usahihi.

Mbili; wape watu changamoto ya kukua zaidi.

Unapaswa kuwapa watu changamoto ya kukua zaidi, kutoka pale walipo sasa na kupiga hatua zaidi. Usiwe mtu wa kuwabembeleza watu na kutaka wajione wako vizuri, badala yake kuwa mtu wa kuwaonesha watu ukweli, kwamba wanaweza kuwa bora zaidi ya walivyo sasa.

Katika kuwasukuma watu wawe bora zaidi, kuna wengi hawatakuelewa. Wapo ambao watakuona wewe ni mkatishaji tamaa, na wapo wengine wataona ni mtu usiyeridhika. Lakini simamia kuwafanya watu kuwa bora na wale watakaokuwa bora hawatakusahau kamwe.

Yapo maeneo matatu muhimu ya kuwasukuma watu kuwa bora zaidi.

Eneo la kwanza ni kuwasukuma watu kuwa na tabia bora zaidi, kuwafanya wawe waaminifu, wenye uadilifu, wanaojituma na wavumilivu.

Eneo la pili ni kuwasukuma watu ni kwenye mahusiano yao na wengine, kuwafanya waweze kuboresha zaidi mahusiano yao na wengine.

Eneo la tatu ni kuwasukuma watu kwenye mchango wanaotoa kwa wengine, kuwasukuma watoe thamani kubwa zaidi kwa wengine.

Tatu; kuwa mfano wa vile unavyotaka watu wawe.

Unaweza kutumia nguvu nyingi sana kuwaambia watu wanapaswa kuwaje, lakini isizae matunda. Lakini wewe unapokuwa kama unavyotaka watu wawe, ujumbe unafika haraka na watu wanakuwa. Kwa mfano unaweza kuwasisitiza sana watu umuhimu wa kuwahi kazini na usieleweke. Lakini unapoanza kuwa mtu wa kwanza kufika kazini, wale walio chini yako watalazimika kuwahi.

Kile ambacho unataka watu wawe, anza kuwa wewe kwanza na utakuwa mfano mzuri kwao. Watu wanashawishika zaidi kwa kukuangalia kuliko kukusikiliza.

TABIA YA SITA; ONESHA UJASIRI.

Safari ya mafanikio siyo safari rahisi, ina magumu na vikwazo vingi. Kuna kila hatari ya kushindwa kwenye safari hii. Na hatari hizi zimewazuia wengi kuendelea na safari hii ya mafanikio.

Njia pekee ya wewe kuweza kuendelea na safari hii na kufanikiwa ni kwa kuonesha ujasiri. Unahitaji ujasiri ili kuweza kufanikiwa zaidi.

Na ujasiri haimaanishi kwamba huna hofu kabisa, badala yake ni kuwa tayari kuchukua hatua licha ya kuwa na hofu. Wale wanaoonekana jasiri na mashujaa siyo kwamba hawana hofu, wanakuwa nazo, ila hawaruhusu hofu hizo ziwe kikwazo kwao.

Pia ujasiri unaambukizwa, kadiri unavyochukua hatua za kijasiri kwenye eneo moja la maisha yako, ndivyo unavyoweza kutumia kwenye maeneo mengine pia. Hivyo kama huna ujasiri, unaweza kuanza na vitu vidogo na kupata ujasiri wa kufanya vitu vikubwa pia.

Ujasiri haupo tu kwenye kuchukua hatua za kishujaa, lakini pia ujasiri ni kuwa tayari kutokuchukua hatua fulani ambayo ingekuwa kikwazo kwako. Mfano mtu amekuudhi na hasira zikakujia, lakini ukajizuia usichukue hatua yoyote ukiwa na hasira hizi, hilo pia ni ujasiri.

Katika kujijengea ujasiri, zipo hatua tatu za kuchukua.

Moja; heshimu mapambano.

Tambua kwamba safari ya mafanikio ni mapambano. Jua kwamba utakutana na magumu na changamoto. Hivyo usikimbie wala kutafuta njia rahisi, badala yake heshimu mapambano na yapokee vizuri.

Kufikia mafanikio makubwa inahitaji kuweka kazi sana, kuwa na nidhamu ya hali ya juu, kujifunza kila wakati na kupambana na vikwazo vinavyoibuka kila wakati. Yote haya yanahitaji ujasiri.

Tunaishi kwenye jamii ambayo inayaremba mafanikio, inawadanganya watu kwamba kuna njia za mkato za kufanikiwa bila ya kuumia na bila ya kazi. Huo ni uongo na usijisumbue nao.

Kuwa tayari kuumia, kuwa tayari kuteseka na kuwa jasiri kupambana na hayo yote na mwisho wa siku utafanikiwa sana.

Mbili; washirikishe wengine malengo yako makubwa.

Malengo makubwa uliyonayo kwenye maisha yako, usiyafanye kuwa siri. Badala yake waeleze watu wazi kuhusu malengo hayo.

Kwa kufanya hivi wataibuka watu wa kukupinga na kukushangaa. Wapo watakaokuambia umechanganyikiwa, wapo watakaokuambia huwezi kabisa kufikia malengo hayo makubwa. Lakini usiwasikilize hao, badala yake endelea kusimamia malengo yako.

Paza sauti kueleza malengo makubwa ya maisha yako na unayoyafanyia kazi. Wengi watakupinga na kukucheka, lakini wapo watakaoweza kukusaidia na kuja kwako kuhakikisha unafikia malengo hayo.

Unahitaji ujasiri wa hali ya juu kuweza kuyaweka wazi malengo yako makubwa, lakini kwa kufanya hivyo kunakuongezea ujasiri zaidi.

Pia pale mambo yanapokuwa magumu kwenye safari yako, ndiyo wakati wa kuiishi misingi yako kwa sababu hapo ndipo unapikwa kwa ajili ya mafanikio yako makubwa.

Tatu; tafuta mtu wa kumpigania.

Unapopewa jukumu la kumlinda mtu mwingine, unajitoa zaidi kuliko kujilinda mwenyewe. Mtu mwingine anapokuwa hatarini na wewe ni jukumu lako kumuokoa unapata ujasiri wa kuchukua hatua ambazo wewe mwenyewe usingeweza kuzichukua.

Hivyo angalia ni mtu au watu gani upo tayari kuwapigania, upo tayari kufa kwa ajili yao. Watu hao watakupa wewe ujasiri wa kuchukua hatua ambazo wewe mwenyewe usingeweza kuchukua.

Kumbuka unafanya zaidi pale wengine wanapohusika kuliko unapokuwa mwenyewe.

Rafiki, hizo ndiyo tabia sita ambazo unapaswa kujijengea ili uweze kufanikiwa zaidi. Tabia hizo kila mtu anaweza kujijengea bila ya kujali elimu, haiba, rangi, kabila au uwezo. Kazi ni kwako kuzijenga tabia hizo kwa kuchukua hatua tulizojifunza na maisha yako yataweza kuwa bora zaidi.

Kwenye #MAKINIKIA tutajifunza mitego mitatu ya kuepuka ambayo imewaangusha wengi na tabia moja muhimu inayokuwezesha kunufaika na tabia hizi sita tulizojifunza.

#3 MAKALA YA JUMA; SIFA NNE ZA KAZI YENYE MAANA KWAKO.

Watu wengi wanapokuwa wanaanzia chini kabisa, kigezo pekee cha kuchagua kazi au biashara ya kufanya huwa ni kipato. Na wengi husema wazi, niko tayari kufanya kazi au biashara yoyote itakayoniingizia kipato.

Kweli wengi wanapata kazi au biashara ambayo inawapa kipato. Wanaweka juhudi sana na hilo linawawezesha kufanikiwa. Wakati wanaanza kazi hiyo wanakuwa hawaipendi wala haiwahamasishi sana. Lakini kwa sababu inawaingizia kipato, basi wanajiambia wakiweka juhudi kubwa na kipato kikawa kikubwa, wataipenda tu.

Wanaweka juhudi kweli, na kipato kinaongezeka kweli, lakini ndani yao bado kunakuwa na utupu fulani. Walichofikiri kwamba wakipata fedha zaidi watapenda kazi au biashara hiyo hakitokei.

Sasa maisha yao yanakuwa kama kufukuza kipepeo, wanakazana kufanya kazi zaidi ili wapate furaha na hivyo hawaipati.

Kitu ambacho watu hawa wanakuwa hawajui ni kwamba furaha kwenye kazi haitokani na kipato unachoingiza, bali maana ambayo kazi hiyo inaleta kwenye maisha yako.

Kwenye makala ya juma hili, nimekushirikisha sifa nne za kuangalia kwenye kazi au biashara ili iwe na maana kwako.

Hii ni makala ambayo kila mtu anapaswa kuisoma na kuifanyia kazi, kwa sababu kazi na biashara tunazofanya zinagusa eneo kubwa sana la maisha yetu.

Kama hukusoma makala hiyo, basi isome sasa hapa; Sifa Nne Za Kuangalia Wakati Wa Kuchagua Kazi Au Biashara Ili Iwe Na Maana Kwako Na Uweze Kufikia Mafanikio Makubwa.

Rafiki, kama hupokei makala ninazotuma kwenye email kila siku basi unakosa maarifa mazuri sana. Nakusihi ujiunge na mfumo wetu wa kupokea email ambao ni bure kabisa, na kila siku nitakuamsha na makala fupi ya DAKIKA MOJA, yenye mafunzo muhimu sana kwa mafanikio yako. Kujiunga na mfumo huu wa email fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

#4 TUONGEE PESA; KUSEMA NDIYO NA KUSEMA HAPANA.

Rafiki, mafanikio yako kwenye maisha yanategemea sana uwezo wako wa kutumia maneno haya mawili; NDIYO na HAPANA.

Unapokuwa unaanzia chini kabisa, unahitaji kusema NDIYO mara nyingi uwezavyo.

Iwe ni kwenye kazi au biashara, chochote ambacho mwajiri au mteja anakuambia sema ndiyo. Hata kama huwezi au hujui, sema ndiyo kisha nenda kajifunze jinsi ya kukifanyia kazi.

Unahitaji kusema ndiyo unapokuwa unaanza kwa sababu fursa nyingi unazozipata mwanzoni zinakusukuma wewe kukua zaidi. Zinakufanya ujijue wewe mwenyewe na ujue ni maeneo gani uko vizuri na yapi hauko vizuri.

Unapokuwa unaanza unahitaji kufanya mambo mengi na tofauti, haya yanakuwezesha kukua zaidi.

Kusema kwako ndiyo kwa wingi mwanzoni kutaanza kukuletea mafanikio kidogo. Na hapo utajifunza kwamba kusema ndiyo kuna manufaa makubwa kwako.

Sasa mafanikio haya kidogo unayokuwa umepata, usipokuwa makini yanakuwa kikwazo kwako kufanikiwa zaidi.

Kwa sababu unapopata mafanikio kidogo, kila mtu anakuja kwako na matakwa yake zaidi. Mwajiri anakupa majukumu zaidi na mengine yako nje kabisa ya wajibu wako. Wateja wanakuja kwako na mahitaji makubwa zaidi, mengine yako kabisa nje ya uwezo wako.

Kwa sababu umeshajifunza kusema ndiyo kuna manufaa, unasema ndiyo kwa kila kitu. Hili linapelekea kuwa na ndiyo nyingi kuliko uwezo wako wa kuzitekeleza, na hapo sasa unajizuia kukua zaidi. Unajikuta unachoka na mahitaji mengi ya wengine, unakosa kabisa muda wa kufanya yale muhimu kwako. Unatawanya nguvu zako maeneo mengi  na kujikuta unafanya kwa kawaida na kwa viwango vya chini.

Hapa sasa ndipo unapopaswa kuanza kutumia neno jingine muhimu sana kwa mafanikio yako. Neno hilo ni HAPANA.

Ndiyo ilikuwezesha kuanza safari ya mafanikio, HAPANA ndiyo itakufikisha kwenye kilele cha mafanikio.

Baada ya kukubali mambo mengi, utakuwa umejifunza ni vitu gani unaweza kuvifanya kwa ubora zaidi, unavyopenda kuvifanya na ambavyo vinakulipa zaidi ukivifanya. Hapo sasa unapaswa kuvifanya hivyo kuwa kipaumbele cha kwanza kwako. Hivyo ndiyo vitu utakavyoendelea kusema ndiyo.

Vitu vingine vyote nje ya hivyo ni HAPANA. Hata kama mtu anahitaji kiasi gani, hata kama yupo tayari kukulipa kiasi gani, kama kitu hakipo kwenye vipaumbele vyako, jibu lako ni HAPANA.

Inahitaji ujasiri kusema HAPANA, maana utakuwa unazikataa fedha. Lakini jua ni neno unalopaswa kulitumia kama kweli unataka kufikia mafanikio makubwa zaidi.

Kama umekuwa unasema ndiyo kwenye kila aina ya fursa, leo kaa chini na fanya zoezi hili. Orodhesha shughuli zote unazofanya ambazo zinakuingizia kipato. Orodhesha pia biashara zote unazofanya zinazokuingizia kipato. Orodha hiyo ipange kwa kuanza na unayopenda zaidi.

Kisha weka kiasi cha kipato unachopata kwenye kila shughuli au biashara na pia. Hapa utagundua kitu kimoja, kwenye orodha ya vitu 10 utakavyokuwa umeweka, vitu 2 vina manufaa makubwa kwako kuliko vitu 8 ukivikusanya kwa pamoja. Kama umeorodhesha vitu 5, basi kimoja kina manufaa kuliko vile vinne ukivikusanya pamoja.

Sasa lengo lako kuu kwenye maisha liweke kufanya vile vyenye manufaa pekee. Vingine vyote achana navyo, ni usumbufu kwako, vinakuzuia usifanikiwe zaidi. Sema HAPANA kwa vitu vingine vyote isivyokuwa vile vichache vyenye manufaa kwako.

Kwa njia hii utakuwa na uhuru zaidi na utaweza kufanya vitu vichache kwa ubora wa juu, utabobea sana na kipato chako kitakuwa kikubwa pia.

Nina imani umeelewa matumizi sahihi ya NDIYO na HAPANA, anza kuyatumia sasa.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; MWANZO WA SAFARI YA KUELEKEA KWENYE UKUU.

“Often, the journey to greatness begins the moment our preferences for comfort and certainty are overruled by a greater purpose that requires challenge and contribution.” ― Brendon Burchard.

Kuna vitu viwili vinatuzuia tusifike kwenye ukuu, tusifanikiwe zaidi. Vitu hivyo ni raha na uhakika. Huwa tunapenda sana raha, tunapenda kufanya vitu ambavyo tunajisikia raha kufanya, vitu ambavyo havitusukumi wala kutuumiza. Lakini pia tunapenda sana uhakika, tunapenda kufanya vitu ambavyo tuna uhakika navyo. Lakini kitu kikishakuwa na uhakika, hakiwezi kukufikisha kwenye mafanikio.

Hatua ya kwanza ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa na ukuu ni kuachana na raha na uhakika na badala yake kuwa tayari kukabiliana na changamoto na kutoa mchango kwa wengine.

Kwa maneno mengine, safari yako ya ukuu inaanza pale unapozikabili changamoto, pale unapofanya vitu ambavyo hujazoea kufanya, ambavyo ni vipya kwako na ukawa tayari kukabiliana na changamoto unazokutana nazo bila ya kuzikimbia. Lakini pia inahitaji kutoa mchango wako kwa wengine. Chochote unachofanya, kazana kutoa thamani kubwa kwa wengine, wafanye wale wanaokutana na kazi yako kuwa bora zaidi kuliko walivyokuwa kabla hawajakutana na kazi zako.

Unafanikiwa na kufikia ukuu pale unapoachana na raha na uhakika na kwenda kuzikabili changamoto na kutoa mchango kwa wengine.

Rafiki yangu mpendwa, hizi ndiyo TANO ZA JUMA hili la 24, ni imani yangu umejifunza kwa kina umuhimu wa tabia kwenye mafanikio yako na pia matumizi ya ndiyo na hapana. Nenda kaziweke tabia hizi kwenye maisha yako na utaweza kufanikiwa zaidi ya hapo ulipofika sasa.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili nitakwenda kukushirikisha TABIA TATU ambazo zimewaangusha wengi waliofikia mafanikio makubwa ili uweze kuzikwepa. Pia nitakushirikisha TABIA MOJA KUU ambayo ukiijumuisha na tabia sita ulizojifunza, hakuna kinachoweza kukuzuia kufanikiwa zaidi. Ukikosa tabia hii moja kuu, tabia sita ulizojifunza hazitakuwa na msaada kwako kufanikiwa.

#MAKINIKIA yanapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM. Kama bado hujajiunga na channel hii basi unakosa madini mengi na mazuri kutoka kwenye vitabu. Jiunge leo na utanufaika sana na mafunzo mengi yanayopatikana kwenye channel hii. Maelekezo ya kujiunga na channel hii yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu