Fursa mpya zinazoibuka kila siku zimekuwa kikwazo kwa wengi kufanikiwa.
Tulitegemea uwepo wa fursa nyingi uwe kichocheo cha wengi kufanikiwa, lakini matokeo yamekuwa kinyume.
Kadiri fursa zinavyokuwa nyingi, ndivyo wachache sana wanafanikiwa.
Na sababu kubwa ni kushindwa kuchagua fursa sahihi mtu kufanyia kazi na kusema hapana kwa fursa nyingine zinazoweza kuonekana ni nzuri.
Kwa kuwa kila fursa inaonekana ni nzuri, mtu anajikuta akikimbizana na kila aina ya fursa. Leo anakutana na fursa hii na kuanza kuifanyia kazi. Kabla hajapiga hatua sana anakutana na fursa nyingine inayoonekana ni nzuri zaidi. Anaacha ile anayofanyia kazi na kwenda kwenye fursa mpya. Hapo pia hakai muda mrefu kabla hajakutana na fursa nyingine inayoonekana nzuri zaidi.
Rafiki, lazima ufike mahali na ujifunze kusema hapana kwa fursa ambazo zinaonekana ni nzuri, la sivyo hutaweza kupiga hatua kabisa.
Tena kuwa makini sana na wale wanaokuletea fursa hizi mpya, wengi watakuambia kwa tunavyokujua wewe, fursa hii ni nzuri sana kwako, ukiikosa basi umejikosesha mengi. Na wewe utaona kweli wanamaanisha na kuingia kichwa kichwa kwenye fursa hizo.
Rafiki, leo nakupa kipimo sahihi cha kuchagua fursa mpya ya kufanyia kazi pale ambapo tayari umeshachagua fursa nyingine.
Kipimo hicho ni kuipa fursa miezi sita, kama baada ya miezi sita fursa hiyo itaendelea kuwepo na ukaweza kuifanyia kazi basi ni fursa sahihi kwako. Lakini kama haiwezi kusubiri miezi sita, basi siyo fursa sahihi kwako na wala isikusumbue.
Unapokutana na fursa mpya, ambayo umeshawishika kweli kwamba unapaswa kuifanyia kazi, iweke kwenye kalenda yako kwamba utaanza kuifanyia kazi miezi sita ijayo. Kisha isahau kabisa na endelea na fursa unayofanyia kazi sasa. Kama baada ya miezi sita fursa hiyo haipo tena, basi jua haikuwa fursa sahihi kwako. Kama bado ipo basi ni sahihi kwako na unaweza kufanyia kazi.
Na matumaini ni kwamba kwa miezi sita uliyojipa kabla ya kuingia kwenye fursa hiyo, umeshaweka msingi mzuri kwenye fursa uliyokuwa unafanyia kazi na pia umeshaelewa zaidi kuhusu fursa hiyo mpya.
Lakini najua ambacho utakuwa unafikiria, kwamba fursa nyingi hazisubiri, na wale wanaokuletea fursa mpya wanakuambia ukichelewa kidogo unaikosa. Kama unafikiria hivyo, na kama utawaamini wanaokuambia hivyo, basi wewe bado ni mchanga kwenye safari hii ya mafanikio. Na ushauri wangu ni ufuate kile nimekuambia hapa, subiri miezi sita na usiyumbishwe na chochote kile.
Kwa kuwa na msimamo wa aina hii kutakusaidia sana usiyumbishwe na kila fursa mpya zinazoibuka, kutakuwezesha kuweka kazi kwenye fursa moja na kuweza kubobea na kuzalisha matokeo bora sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,