Ipo kauli kwamba hakuna kipya kinachotokea chini ya jua. Kila tunachokiona sasa kilishatokea tena huko nyuma, kwa sasa kinaweza kutokea kwa njia tofauti au tukakikabili kwa namna tofauti, lakini ni kitu kile kile.
Hivyo changamoto kubwa za dunia ni zile zile, zimekuwa zinajirudia kwenye kila kizazi.
Na hii inazalisha simulizi mbili kwenye hadithi ya maisha ya mwanadamu.
Simulizi ya kwanza ni mapambano.
Maisha ni mapambano, tunakutana na magumu na changamoto, ambayo yanatutaka tupambane ili kuyavuka.
Mapambano haya siyo rahisi, ni magumu na yanaumiza na kutesa.
Wengi huwa hawapendi mapambano haya hivyo wamekuwa wanaishia njiani na wasipate kile wanachotaka.
Simulizi ya pili ni maendeleo.
Baada ya mapambano, kinachofuata ni maendeleo. Wale wanaopambana kweli na wasikate tamaa, ndiyo wanaopiga hatua kuelekea kule wanakotaka kufika.
Maendeleo yanakwenda kwa wale wanaojitoa kweli, wale ambao hawakubali kurudishwa nyuma na chochote kile.
Huwezi kupata maendeleo kama hujapambana, kama hujaumia na kuvuka magumu na changamoto.
Angalia mtu yeyote ambaye amepiga hatua na utaona alipambana sana.
Hivyo usitegemee kwamba mambo yatakuwa tofauti kwako, kama unataka kupiga hatua zaidi, kuwa tayari kupambana zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,