Mpendwa rafiki yangu,
Unajua kwa sasa tunaishi kwenye dunia yenye kuvutia sana ukilinganisha na hapo awali. Dunia ya sasa inakila kitu tunachotaka na miaka ya nyuma watu walikuwa wamekulia kwenye mashamba, kulikuwa hakuna teknolojia kubwa kama ya sasa, watu walikuwa wanaisi kwenye jamii ndogo sana na ubinadamu ulikuwa ni mwingi zaidi.
Watu siku hizi wamekuwa hawana tena ule uwezo wa kuhisi yaani kutumia ile milango yao ya fahamu kama mwanzo yaani watu hawakosensible. Tunashuhudia watu wako bize kweli kila kukicha wakitafuta kile wanachokitaka.
Kuna watu siku hizi kwenye mioyo yao wako wapweke, licha ya kuwa na kila kitu bado watu wanaishi lakini kama vile wamechanganyikiwa kwenye maisha yao. Watu wamejikita sana kukusanya mali katika jamii na kusahau vitu vidogo sana ambavyo vinawafanya watu wajisikie vizuri.
Kuna mambo mengi ya kawaida kabisa ambayo tukiyafanya yatawafanya watu wajisikie wa muhimu kwenye hii dunia.
Kwa mfano, kuwa na mazungumzo na jirani yako kwenye mabasi ya umma ni kitu ambacho ni kidogo sana lakini siku hizi hakuna. Mtu akiingia kwenye gari baada ya kupata siti anachukua simu yake anaendelea kuwa bize na mitandao ya kijamii. Hata kujuliana hali kwenye magari imekuwa adimu lakini unapomsalimia hata mtu unayekaa naye kwenye siti moja na kuongea naye mawili matatu utakua umemfanya ajisikie muhimu. Kwani kuna watu wanatoka kwao wakiwa na changamoto zao za asubuhi huenda hata hakupata wa kumsalimia sasa wewe ndiyo unakuwa mtu wake wa kwanza unafikiri atajisikiaje kama ukimsalimia kidogo na kumshika mkono na kumtakia majukumu mema?
Kuna mambo madogo sana ambayo jamii ya sasa imeyasahau ambayo ndiyo yanaleta umuhimu kwa wengine kwa mfano jambo lingine. Kuwathamini watu kwa kile wanachofanya. Kuna watu siyo wa kupongeza, hata kama mtu amefanya kitu kizuri hatupongezi, sisi tunajua kukosoa tu. Mtu amejaribu, amependeza lakini hatuwapongezi kwa yale mazuri waliyofanya. Kuna mambo madogo kama haya ukimfanyia mtu lazima atakushukuru na utakua umemfanya mtu muhimu kwenye hii dunia. Kuna wengine wanakosa hata watu wakuwatia moyo, kuwaambia wamependeza, kusikia tu hata neno nakupenda, kutakiwa majukumu mema. Ni jambo dogo sana lakini kupitia kuwapongeza wengine inachangia sana kuwafanya watu kujisikia ni wa muhimu.
Vitu kama kukaa na familia yako na kula pamoja ni jambo ambalo linawafanya watu wajisikie wa muhimu. Siku hizi ni watu wangapi wanaokaa chini na kula na familia zao? Wazazi wanarudi na kuondoka watoto wakiwa bado wamelala? Watoto wanaona wazazi siku za wikiendi na tena ni salamu tu na siyo kukaa nao na kuongea nao kidogo. Je hapo mtoto atapata wapi baba au mama wa kumsaidia kwenye kazi zake za shule?
Unapowapa muda ndugu, mwenza, rafiki, wafanyakazi mwenzako kwa kuwajulia hali, kuwapigia simu inawafanya wajihisi wao ni muhimu. Kuwapigia simu wateja wako na kuwasalimia kujua wanaendeleaje vipi bidhaa waliyochukua kwako imewasaidiaje ni kitu kinachowafanya watu wajihisi na kujisikia vizuri.
Kuongea vizuri na watu kwa kuwaangalia usoni na kuacha kufanya yale ambayo tulikuwa tunafanya na kumpa uwepo tunayezungumza naye inatufanya tujihisi ni wa muhimu. Dunia ya sasa kuwapata watu wanaosikiliza imekuwa ni changamoto kubwa. Watu wamekuwa bize, unaongea nao huku wakiwa wanafanya mengine na wala hawana muda na wewe tena wanakuwa na ishara ya mwili kama vile ongea haraka unawapotezea muda uondoke.
Hatua ya kuchukua leo; tujaribu kufanya yale mambo madogo ambayo yanawafanya watu wajihisi au kujisikia ni muhimu kwenye hii dunia.
Hivyo basi, pale unapohitaji kusema asante sema, unapohitaji kusema samahani sema, tafadhali, pole na mengine mengi yanayofanana na hayo sema. Kwa namna hiyo utawafanya wengine wajisikie vizuri kwenye maisha yao.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net
Asante sana