Najua ni ahadi kubwa sana nimekupa hapo, kwamba kuna kitu ambacho ni jawabu la kila kitu!
Ndiyo, kuna jawabu la kila kitu, ambalo unatembea nalo lakini hulitumii.
Na leo nataka nikuoneshe jawabu hilo na kama utaamua kulitumia basi utaondoka sehemu nyingi ulizokwama sasa.
Jawabu la kila kitu ni KAZI NA UPENDO. Hakuna kingine zaidi ya hapo.
Kama umekwama mahali kwa sasa, angalia vitu hivyo viwili, kuweka kazi zaidi na kuweka upendo zaidi.
Hizi ni nguvu mbili ambazo haziwezi kushindwa na chochote.
Unapokuwa tayari kuweka kazi kubwa, kazi yenye thamani kubwa, dunia haitaacha kukulipa kulingana na kazi unayoweka. Hivyo kama umekwama, jiulize ni kazi gani unahitaji kuweka ili kutoka hapo ulipokwama.
Unapokuwa na upendo wa kweli, upendo unaotoka ndani yako, hakuna chochote kinachoweza kuwa kikwazo kwako. Hutakuwa na chuki, wivu wala hofu, kwa sababu upendo unakupa uhakika wa chochote kwenye maisha.
Unapojipenda wewe mwenyewe, ukapenda kile unachofanya na kuwapenda wengine, kila wakati utafanya kile kilicho sahihi kwako na kwa wengine pia. Hata kama maisha ni magumu, upendo unakupa wewe nguvu ya kuvuka kila aina ya ugumu.
Huwezi kujituma kuweka kazi, huku ukiwa na upendo halafu wakati huo huo ukawa na chuki au wivu, au hofu au kukata tamaa. Ni vitu ambavyo haviwezi kwenda pamoja hata kidogo.
KAZI na UPENDO ndiyo jawabu la kila kitu. Kila unapojikuta umekwama, kila unapojikuta njia panda, jiulize ni jinsi gani KAZI NA UPENDO vinaweza kukutoa hapo ulipokwama sasa na utaona hatua sahihi za kuchukua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,