“Don’t let your reflection on the whole sweep of life crush you. Don’t fill your mind with all the bad things that might still happen. Stay focused on the present situation and ask yourself why it’s so unbearable and can’t be survived.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.36

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ambayo tumeiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari WEKA UMAKINI WAKO KWENYE WAKATI ULIOPO…
Kila mmoja wetu ana malengo makubwa sana kwenye maisha yake,
Malengo ambayo muda mwingi anajikumbusha ili kuweza kuyafikia.
Japokuwa hili ni zuri, lakini hupaswi kuruhusu malengo makubwa uliyonayo yakuzuie kutumia vizuri muda ulionao sasa.

Katika wakati wowote ule, muda pekee ambao una umiliki nao na unaweza kuutumia vizuri ni muda uliopo.
Muda uliopita hauwezi kuubadili, na muda ujao huwezi kufanya chochote.
Lakini muda ulionao, ndiyo muda ambao unaweza kufanya chochote unachotaka kufanya.

Na ili kunufaika na muda huo, weka umakini wako wote kwenye muda huo,
Weka umakini wako wote kwenye kile unachofanya,
Na hapo utaweza kuona hatua sahihi kwako kuchukua.

Unapoweka umakini wako wote kwenye muds uliopo na kwenye kile unachofanya, huwezi kupata hofu wala msongo.
Kwa sababu hofu huwa inakuja pale unapoangalia siku zijazo na usiwe na uhakika.
Na msongo unakuja unapoangalia siku zilizopita na siku zijazo na kuona mambo yatakuwa magumu zaidi.
Lakini unapoweka umakini wako kwenye wakati uliopo na kufikiria kile tu unachofanya kwa wakati huo, unakifanya kwa umakini na hofu au msongo havipati nafasi kwako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuweka umakini wako wote kwenye wakati uliopo na kile unachofanya kwa wakati huo.
#IshiWakatiUliopo #LeoNiLeo #MudaUlionaoNiSasa

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1