Chochote unachochagua kufanya, hakitakuwa rahisi.
Ugumu utaanzia ndani yako mwenyewe, wengine watakupinga na kukukatisha tamaa na hata mazingira na hali hazitakupa urahisi wa kufanya.
Sasa je unavukaje mambo haya yote na kupata kile unachotaka?
Hapa ndipo unahitaji kitu kimoja muhimu sana kitakachokuvusha, kitu hicho ni kujali sana kuhusu kile unachofanya.
Njia pekee ya kukusukuma wewe kufanya kazi hata pale ambapo hujisikii kufanya, kukusukuma kuendelea hata pale wengine wanapokukatisha tamaa ni kujali sana kile ambacho unafanya.
Kukifanya kitu hicho kuwa kipaumbele cha kwanza kwako na kutofikiria kitu kingine chochote bali hicho. Unapeleka nguvu zako zote na umakini wako kwenye hicho unachofanya.
Kadiri unavyojali kile unachofanya, ndivyo unavyopata nguvu ya kukusukuma kufanya zaidi na nguvu hiyo inakuwezesha kuvuka kila aina ya ugumu.
Kama hakuna kitu kingine unachofikiria, wala kinachonyonya nguvu zako, kile unachofanya kinakuwa namba moja kwako, kinakuwa ndiyo kitu pekee kwako, kinakuwa ndiyo wewe.
Kama huwezi kujali kile unachofanya kwa viwango hivyo vya juu, usijisumbue hata kuanza kufanya, kwa sababu hutafika mbali. Utakata tamaa haraka na kwa urahisi sana.
Jali sana kile unachofanya na hakuna kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,