Ukiwa huna fedha, kitu muhimu zaidi kwako kinakuwa fedha.
Hivyo haishangazi pale unapoweka juhudi zako zote kwenye kutafuta fedha, maana huna unachoweza kufanya kwenye maisha bila ya kuwa na fedha.
Lakini pia hiki ni kipindi hatari sana kwako, kwa sababu unapopeleka nguvu zako zote kwenye fedha unasahau vitu muhimu kwenye maisha yako.
Na moja ya vitu muhimu sana ambavyo vimekuwa vinasahaulika na wengi ni kusudi la maisha.
Wengi hufikiri kwa sababu wanahitaji fedha, basi wakishazipata maisha yao yatatulia.
Ni mpaka pale wanapozipata fedha ndiyo wanagundua kumbe maisha ni zaidi ya fedha.
Mpaka pale wanapopata fedha za kuwatosha, kiasi kwamba hawana tena wasiwasi juu ya fedha na wanaweza kumudu chochote wanachotaka ndiyo wanagundua kuna kitu kinakosekana ndani yao.
Hapa ndipo wengi hujikuta wakifanya mambo ambayo yanawaharibia kabisa maisha yao, kwa sababu utupu uliopo ndani yao haujazibwa na fedha.
Ujumbe wangu kwako leo ni huu rafiki, tafuta fedha utakavyo, lakini usilisahau kusudi la maisha yako.
Kadiri unavyolijua kusudi hili mapema ndivyo unavyokuwa na maisha tulivu, maisha yenye maana kwako.
Pambana uwezavyo ili kupata fedha, lakini pia endelea kufanyia kazi kusudi la maisha yako.
Kama kazi au biashara yako ndiyo kusudi la maisha yako basi una bahati kubwa, hapo unapata vyote kwa pamoja.
Kama kusudi lako la maisha ni tofauti na kazi au biashara unayofanya, unahitaji kutenga muda kwa ajili ya kufanyia kazi kusudi la maisha yako.
Huwezi kukwepa wala kukimbia hilo. Chukua hatua sasa kabla hujachelewa na kujikuta una kila unachotaka, lakini ndani yako kuna utupu. Lijue kusudi lako mapema na liishi kila siku.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,