#TANO ZA JUMA #25 2019; Kukosea Ni Ubinadamu, Matumizi Ya Orodha Kupunguza Makosa, Hatua Nane Za Kutengeneza Biashara Unayoweza Kuiuza, Matumizi Ya Orodha Kwenye Uwekezaji Na Kwa Nini Nidhamu Ni Ngumu Kujenga.

Rafiki yangu mpendwa,

Hongera kwa juma namba 25 la mwaka huu 2019 ambalo tunalimaliza. Ni imani yangu limekuwa juma bora sana kwako, juma ambalo umejifunza vitu vipya na kuchukua hatua mpya ili kuweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Nachukua nafasi hii kukukaribisha kwenye TANO ZA JUMA hili, ambapo nimekuandalia maarifa bora sana kwako yatakayokuwezesha kupiga hatua zaidi na kufikia mafanikio ambayo unataka kufikia kwenye maisha yako.

Kwenye juma hili nakwenda kukushirikisha maarifa kutoka vitabu viwili ambavyo nimesoma na kuchambua.

Kitabu cha kwanza kinaitwa Built to Sell: Creating a Business That Can Thrive Without You ambacho kimeandikwa na mwandishi John Warrillow. Kupitia kitabu hiki, John ametushirikisha hatua nane za kutengeneza biashara inayoweza kujiendesha bila ya uwepo wako na pia unayoweza kuiuza na kupata fedha zaidi. Hatua hizi nane nimekushirikisha kwenye makala ya juma hili.

checklist manifesto

Kitabu cha pili kinaitwa The Checklist Manifesto: How to Get Things Right ambacho kimeandikwa na Daktari bingwa wa upasuaji Atul Gawande. Kwenye kitabu hiki, Atul ametuonesha jinsi ambavyo sisi binadamu tunafanya makosa kwenye kazi zetu za kila siku, na njia rahisi ya kupunguza makosa hayo ambayo ni kutumia orodha (checklist). Sehemu kubwa ya TANO hizi za juma itabeba maarifa kutoka kitabu cha Checklist Manifesto.

Karibu tujifunze na kuhamasika ili tuweze kuchukua hatua kubwa na kufanikiwa zaidi.

#1 NENO LA JUMA; KUKOSEA NI UBINADAMU.

Imekuwa ni kawaida ya watu kujiona kwamba hawawezi kukosea, hasa pale wanapokuwa na elimu kubwa au uzoefu mkubwa kwenye kile ambacho wanakifanya. Lakini huu siyo uhalisia, kukosea ni sehemu ya maisha ya binadamu.

Hivyo kama tunataka kuwa na maisha bora, na kama tunataka kufanikiwa zaidi kwenye maisha yetu, basi tunapaswa kukubali kwamba huwa tunakosea.

Wanasema kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua. Hivyo kama unataka kutatua matatizo mengi unayokutana nayo kwenye kazi zako, biashara zako na hata maisha yako kwa ujumla, unahitaji kwanza kukubali kwamba kuna makosa umekuwa unafanya.

Hiki siyo kitu pendwa kwa wengi, yanapotokea matatizo kila mtu huwa anakimbilia kunyoosha vidole kwa wengine kwamba ndiyo waliosababisha matatizo hayo, lakini wao hujitoa kwenye tatizo husika. Hii haitakusaidia kutatua matatizo unayokutana nayo na haitakufikisha kwenye mafanikio.

Kubali kwamba kuna nyakati na maeneo ambapo huwa unakosea. Na hapo sasa unaweza kujifunza makosa unayofanya, kwamba ni wakati gani huwa unafanya makosa zaidi, ukiwa kwenye mazingira gani na hali gani.

Kwa kujifunza kuhusu makosa yako, kuna eneo utaliona ambapo lina udhaifu na linalopelekea makosa mengi kujitokeza. Hapo sasa unaweza kuweka hatua za kukusaidia usirudie makosa hayo kwenye eneo hilo.

Mfano kama umekuwa unafanya makosa kwenye makubaliano ya bei kwenye biashara yako, ukishajua hili ndiyo tatizo lako, unatengeneza njia ya kuzuia tatizo hilo lisijirudie. Hapa unaweza kuweka orodha ya vitu vya kuzingatia wakati wa makubaliano ya bei, na unapokuwa kwenye hali inayohusisha makubaliano, unatumia orodha hiyo.

Chanzo kikubwa cha makosa tunayofanya kwenye maisha ni kwa sababu tunafanya mambo kwa mazoea, na hivyo inakuwa rahisi kuruka baadhi ya hatua muhimu kwenye kufanya kile tunachofanya. Tunapokuwa na orodha ambayo tunaifuata, ni rahisi kuondokana na makosa ambayo tumekuwa tunafanya.

Mfano mdogo kabla sijamaliza hapa, panga siku unaenda sokoni kununua mahitaji, fikiria mahitaji yako yote bila ya kuandika popote, kisha nenda sokoni ukanunue. Utakaporudi utagundua kuna vitu umesahau kununua. Lakini kama utakaa chini kwanza na kuorodhesha mahitaji yote uliyonayo kabla ya kwenda sokoni, kisha ukifika sokoni unanunua na kuweka alama kwenye orodha yako, hutaweza kusahau hata kitu kimoja.

Kwenye kitabu chetu cha juma, tutajifunza mengi kuhusu matumizi ya orodha kupunguza makosa ambayo tunayafanya kila siku.

Kubali kwamba kuna makosa mengi umekuwa unayafanya, na hapo chukua hata ya kukuzuia usirudie tena makosa hayo.

#2 KITABU CHA JUMA; MATUMIZI YA ORODHA KUPUNGUZA MAKOSA.

Atul Gawande ni daktari bingwa wa upasuaji wa nchini Marekani. Lakini pia ni mtafiti wa afya, hasa kwenye eneo la afya ya jamii. Kupitia kazi yake ya upasuaji na utafiti, Atul amekutana na changamoto kubwa sana zinazotokana na makosa yanayofanywa na watu ambao wameaminiwa kufanya kazi zao vizuri.

Mfano mzuri ni katika upasuaji, Atul ameweza kugundua kwamba, changamoto nyingi zinazotokea kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, ni kwa sababu ya makosa yanayofanywa na timu nzima ya upasuaji. Kuanzia kwa daktari mpasuaji mwenyewe, mtu anayetoa dawa ya usingizi na hata manesi wanaosaidia wakati wa upasuaji.

Kwa mfano moja ya changamoto kubwa sana baada ya upasuaji huwa ni maambukizi ya bakteria (bacteria infection), ambayo huwasumbua sana wagonjwa baada ya upasuaji. Tafiti zinaonesha kwamba iwapo mgonjwa atapewa dawa ya kuua bakteria (antibiotic) ndani ya dakika 30 kabla ya upasuaji kuanza, maambukizi yanapungua sana. Lakini kutokana na mambo mengi yanayohusika kwenye upasuaji, kitu kidogo kama hicho kinasahaulika na wagonjwa wanaumia.

Pia changamoto nyingine kama mgonjwa kupoteza damu nyingi na hivyo kufariki wakati wa upasuaji au baada ya upasuaji, unaweza kuzuiwa kama watu watategemea upotevu mwingi wa damu na damu za nyongeza kuandaliwa kwa ajili ya mgonjwa kuongezewa pale anapopoteza damu.

Kwa kuona changamoto hii kubwa kwenye upande wa afya, Atul alichukua muda na kujifunza kwenye taaluma nyingine, kuona wanafanyaje mambo yao ambayo ni magumu na muhimu sana bila ya kusahau.

Na hapo alianzia kwenye taaluma ya urubani, hii ni moja ya taaluma ambayo kosa dogo lina madhara makubwa sana kwa watu wengi. Hivyo aliangalia ni jinsi gani marubani wanafanya kazi zao na hatua wanazochukua pale dharura inapotokea ili kuzia maafa yasitokee.

Aliangalia pia kwenye taaluma ya uhandisi, ambayo ni moja ya taaluma muhimu sana, kwa sababu kosa dogo kwenye uhandisi wa jengo kubwa au mashine linaweza kuleta madhara makubwa mno.

Akaenda pia kwa wanasheria, na kuangalia wanafanyaje kazi zao, kwa sababu kosa moja dogo linaweza kupelekea mtu kupata hukumu asiyostahili, mtu akapewa adhabu ya kunyongwa wakati hakustahili adhabu hiyo.

Na pia alienda kwa wawekezaji wakubwa wa fedha, na kuangalia ni kwa jinsi gani wanapima hatari na kuwekeza kwa usalama.

Katika taaluma zote hizi alizoziangalia, Atul aligundua kitu kimoja, taaluma zote hizo zinatumia orodha katika kutekeleza majukumu yale muhimu. Kwa mfao kwenye urubani, kuna orodha za namna ya kufanya kila kitu, na hata inapotokea dharura, zipo hatua za kuchukua ili kuepusha madhara makubwa.

Baada ya kuona umuhimu huu wa kua na orodha ya mwongozo, Atul kwa kushirikiana na Shirika la Afya duniani waliweza kutengeneza orodha ya kutumiwa kwenye vyumba vya upasuaji, ambayo imeweza kupunguza sana changamoto kubwa za upasuaji kama maambukizi, kupoteza damu, kuzidisha dawa ya usingizi na upasuaji usio sahihi kufanyika.

Ni baada ya mafanikio haya makubwa sana yanayotokana na hatua ndogo na rahisi ya kutumia orodha, ndipo Atul ameuandikia kitabu kinachoitwa The Checklist Manifesto: How to Get Things Right. Haijalishi unafanya kazi au biashara ya aina gani, matumizi ya orodha hasa kwenye yale maamuzi muhimu yatakusaidia sana usifanye makosa. Na haya kwenye maisha yako ya kila siku, kama utayaendesha kwa kuwa na orodha unayoifuata, utaweza kupunguza makosa mengi unayotengeneza sasa.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hiki cha MATUMIZI YA ORODHA  katika kupunguza makosa. Jifunze na chukua hatua ili kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

MOJA; Vyanzo viwili vya makosa tunayofanya.

Makosa tunayofanya kwenye kazi na maisha yetu kwa ujumla yanatokana na vyanzo viwili vikuu.

Chanzo cha kwanza ni ujinga, hapa mtu unakuwa hujui kile ambacho ni sahihi kufanya. Hakuna maarifa ya kutosha kuhusu eneo hilo na hivyo hakuna mwenye kujua kilicho sahihi kufanya. Makosa yanayotokana na ujinga tunaweza kusamehewa na hata kujisamehe kwa sababu hatuna ujuzi nayo.

Chanzo cha pili ni uzembe, hapa mtu anajua kilicho sahihi kufanya, lakini hakifanyi, iwe ni kwa kusahau au kupuuza. Hapa maarifa sahihi ya kile kinachopaswa kufanywa yapo, lakini watu wanashindwa kuyatumia. Haya ndiyo makosa ambayo mtu huwezi kujisamehe au kwa kujua umefanya uzembe na kuleta madhara makubwa kwa wengine.

Lakini makosa haya ya uzembe huwa hatuyafanyi kwa makusudi, bali mara nyingi huwa inatokana na kusahau. Na hasa pale hali inapokua ya dharura, ni rahisi sana kusahau vitu vidogo ambavyo baadaye vinaleta madhara makubwa.

Hivyo njia bora ya kuepukana na makosa haya ya uzembe ni kuwa na orodha ya hatua zote muhimu unazopaswa kuchukua kwenye kile unachofanya. Kwa kuwa na orodha unayoifuata, utazingatia yale muhimu.

MBILI; Elimu na ujuzi pekee havitoshi, uzoefu unahitajika.

Hakuna kipindi ambacho elimu na ujuzi vinapatikana kwa urahisi kama sasa. Lakini pia ndiyo wakati ambao makosa yanayofanyika ni mengi na makubwa.

Tumekuwa tunaona makosa yanatokana na kukosa elimu na ujuzi sahihi, lakini hilo siyo kweli. Wengi wana elimu na ujuzi sahihi lakini bado wanafanya makosa mengi na makubwa.

Unahitaji uzoefu kupitia ufanyaji ili kujua changamoto halisi zinazotokana na ufanyaji. Kwenye kujifunza huwezi kukutana na changamoto, na hata ukikutana nazo siyo hatari. Lakini kwenye ufanyaji, hapo ndipo unapata uhalisia wa changamoto.

Mfano ni rahisi kusoma kuhusu kufanya upasuaji fulani, au kurusha ndege, lakini unapokuwa kwenye upasuaji na damu zikaanza kutoka kwa wingi, au upo angani na injini zote mbili za ndege zikafeli, hapo sasa ndipo unahitaji uzoefu kuweza kukabiliana na hali hiyo.

Uzoefu unapatikana kwa njia mbili, kwa kufanya wewe mwenyewe na kukosea au kwa kujifunza kupitia makosa ya wengine.

Njia bora kwako ni kujifunza kupitia uzoefu na makosa ya wengine, ambapo utaangalia dharura zote zinazoweza kutokea kwenye ufanyaji, kisha kuangalia zinavyoweza kukabiliwa na hapo kuweka mfumo wa hatua za kuchukua iwapo dharura kama hiyo itatokea, na hapa tunarudi kwenye ORODHA.

Orodha ni kitu kitakachokuwezesha kutumia uzoefu sahihi katika nyakati za dharura au hatari.

TATU; Changamoto mbili kubwa tunazokutana nazo kwenye mazingira magumu.

Pale tunapokuwa kwenye mazingira magumu ambayo yanakuhitaji kufanya maamuzi magumu na ya haraka, kuna changamoto mbili ambazo huwa zinatukabili.

Changamoto ya kwanza ni kusahau na kugawanyika kwa umakini wako. Pale ambapo una mambo mengi yanayokuhitaji ufanye kwa haraka, ni rahisi kusahau vitu vidogo na ambavyo ni muhimu. Lakini pia umakini wako unakuwa mdogo na hivyo kushindwa kuweka mkazo kwenye vile muhimu.

Changamoto ya pili ni mazoea, pale unapokuwa kwenye hali ya hatari, ni rahisi kuchukulia vitu kwa mazoea, hasa zile hatua ndogo ndogo na kujiambia hicho lazima kitakuwa kimefanyia. Na mara nyingi vitu hivyo tunavyochukulia kwa mazoea vinakuwa havijafanyika na hivyo kuwa ndiyo chanzo kikuu cha changamoto.

Kuondokana na changamoto hizi mbili, unapaswa kutumia orodha. Kwa sababu orodha inakukumbusha yale maeneo muhimu na hivyo umakini wako kutokugawanyika. Lakini pia inakukumbusha hata yale madogo madogo ambayo ni rahisi kuyachukulia kwa mazoea.

NNE; Hakuna tena mjenzi mkuu, au mtu mmoja anayeweza yote.

Kipindi cha nyuma mtu mmoja alikuwa na mamlaka ya kuendesha kitu kikubwa anachosimamia. Kwenye uhandisi na ujenzi palikuwa na mjenzi au mhandisi mkuu. Kwenye urubani kulikuwa na rubani mkuu na kwenye upasuaji kulikua na bingwa wa upasuaji. Watu hawa walichukuliwa kama ndiyo wenye kujua kilicho sahihi kufanya na hivyo kusimamia zoezi zima.

Lakini kwa sasa hakuna tena nafasi ya mtu mmoja kusimamia zoezi zima, kwenye uhandisi na ujenzi kuna ushirikiano wa wahandisi wengi mpaka ujenzi ukamililike, kwenye urubani kuna timu nzima inayorusha ndege na kwenye upasuaji, timu nzima kuanzia mpasuaji, mtu wa usingizi na manesi wasaidizi ni muhimu.

Kama ambavyo tumeona, kukosea ni ubinadamu, mtu mmoja ni rahisi sana kukosea, lakini panapokuwa na watu wengi na wenye ushiriki sawa kwenye kitu, ni vigumu watu wote kukosea au kusahau kitu.

Hivyo katika kutengeneza orodha, inahitaji kujumuisha watu wote wanaohusika kwenye kitu, ili iwe rahisi kutekeleza na yale muhimu yasirukwe au kupuuzwa.

TANO; Aina tatu za matatizo.

Matatizo tunayokutana nayo kwenye maisha yamegawanyika kwenye aina tatu.

Aina ya kwanza ni matatizo rahisi, haya yana njia iliyo wazi ya kuyatatua, ukishaijua njia hiyo ni kuifuata na tatizo linakuwa limeisha. Mfano kupika mkate, ukishajua mchanganyiko sahihi wa vitu na muda wa kuoka, unaweza kurudia zoezi hilo mara nyingi bila ya tatizo.

Aina ya pili ni matatizo magumu, haya ni matatizo ambayo yanahusisha vipengele vingi na hakuna njia moja ya kuweza kuyatatua. Matatizo haya yanahusisha watu na timu mbalimbali, ujuzi mbalimbali na pia hali za nje zinaathiri matatizo haya. Mfano ni kurusha chombo kwenda angani, hakuna kanuni moja ya kutumia na watu wengi wanahusika. Kadiri watu wengi wanavyohusika kwenye tatizo, ndivyo uwezekano wa kuzalisha matatizo zaidi unakuwa mkubwa.

Aina ya tatu ni matatizo tata, haya ni matatizo ambayo hata baada ya kuyafanya, bado huwezi kurudia na kupata matokeo yale yale. Aina hii ya matatizo inahitaji njia mpya ya kutatua kila yanapotokea. Mfano kwenye matatizo magumu, ukishaweza kutatua mara moja, unaweza kurudia tena kutatua tatizo hilo kwa njia hiyo. Lakini kwenye matatizo tata, hakuna kanuni yoyote, hata kama tatizo litajirudia tena, unaanza kulitatua kama ni jipya. Mfano wa matatizo tata ni malezi ya watoto. Kwenye malezi hakuna uzoefu, hata kama umeshakuwa na watoto wanne, ukipata watano anakuja na changamoto zake ambazo uzoefu wako wa nyuma hauna msaada wowote.

Kwa kutumia orodha ya yale muhimu ya kuzingatia, tunaweza kutatua matatizo tata pale yanapoibuka, hata kama hakuna kanuni ya kuyatatua. Kwa kuwa tunajua maeneo muhimu ni yapi na kuyafanyia kazi, tatizo linatatulika au kuzuia lisiwe na madhara makubwa.

SITA; Orodha inagatua madaraka.

Pale changamoto kubwa kama za majanga zinapotokea, tatizo huwa linakuwa kubwa zaidi pale madaraka yanapokuwa kwa watu wachache wa juu na wa chini kusubiri maelekezo kutoka juu. Hali hizi zimekuwa zinatokea sana wakati wa majanga kama ya moto au mafuriko, ambapo watu waliopo eneo la tukio wanashindwa kujua hatua za kuchukua kwa kusubiria maelekezo ya walio juu ambao hawapo eneo la tukio.

Lakini kunapokuwa na orodha ya hatua za kuchukua wakati wa dharura au majanga, madaraka yanakuwa kwa wale waliopo eneo la tukio na hivyo kuweza kufanya maamuzi sahihi yanayozuia dharura au majanga hayo yasiwe na madhara makubwa.

SABA; Jinsi ya kutengeneza orodha nzuri kwako kutumia.

Tumeshaona faida za kutumia orodha na umuhimu wa kuwa na orodha kwenye mambo yote muhimu ambayo mtu unafanya. Unaweza kuwa na hamasa sana ya kutengeneza orodha kwenye maeneo muhimu ya maisha yako. unapaswa kuua jinsi ya kutengeneza orodha sahihi, kwa sababu orodha isipokuwa sahihi inakuwa kikwazo zaidi kwako.

Orodha nzuri ya kutumia inazingatia vitu vifuatavyo;

Moja, imeandikwa kwa usahihi na kwa kueleweka, kwa lugha ambayo inaeleweka na wote wanaoitumia.

Mbili, imeandaliwa kwa ufanisi kiasi kwamba inaweza kutumika kwenye hali yoyote ngumu.

Tatu, orodha inagusa yale maeneo muhimu, ambayo yakisahaulika yanazalisha matatizo makubwa.

Nne, orodha ina vipengele vichache, vitano mpaka 9 ambavyo ni rahisi kufanyia kazi ndani ya dakika moja.

Tano, orodha inafaa kuweka kwenye vitendo, lengo kuu la kuwa na orodha hii ni kuchukua hatua, hivyo lazima iwe inafaa kuweka kwenye vitendo.

Sita, orodha iendee kwenye ukurasa mmoja tu wa karatasi. Zaidi ya hapo itakuwa vigumu kuifuata.

NANE; Orodha siyo mwongozo wa kufanya.

Watu wengi wanapotengeneza orodha au kupewa orodha ya kutumia, huwa wanafikiri ndiyo mwongozo wa ufanyaji. Lakini hili siyo sahihi.

Orodha siyo mwongozo wa ufanyaji, orodha haitakuambia ufanyeje kile unachopaswa kufanya. Orodha siyo kanuni ya ufanyaji.

Bali orodha ni kitu cha kukuzuia usifanye makosa pale ambapo unakuwa kwenye wakati mgumu au dharura. Orodha inakukumbusha maeneo muhimu ya kufanyia kazi katika wakati ambao unahitaji kuchukua maamuzi ya haraka.

Orodha ni kifaa cha kukusaidia kufanya maamuzi pale unapokuwa kwenye changamoto au wakati mgumu, ambapo ni rahisi kufanya makosa kama huna orodha.

TISA; Watu hawapendi kutumia orodha.

Pamoja na manufaa haya makubwa ya kutumia orodha, hasa nyakati za dharura au kufanya maamuzi magumu, bado watu wengi hawapendi kutumia orodha.

Hasa watu ambao wana ujuzi na uzoefu mkubwa, huwa wanaona kutumia orodha ni kitendo cha dharau, kwa sababu orodha inasisitiza yale maeneo ya msingi kabisa, wengi huona hawawezi kusahau hayo.

Lakini katika nyakati za dharura, wengi wanasahau maeneo madogo na ya muhimu. Hivyo weka ufahari wako pembeni na tengeneza na tumia orodha. Hakuna unachopoteza kwenye kutumia orodha, kama ukiitengeneza vizuri itakuchukua dakika moja tu kuipitia, lakini itakusaidia sana usifanye makosa ambayo yataleta madhara kwako na kwa wengine pia.

KUMI; orodha ya kutengeneza orodha.

Katika kutengeneza orodha yako, fuata orodha hii.

Kwanza kabisa igawe orodha hiyo katika makundi matatu, hivi ndiyo vinakuwa vituo vya kusimama na kupitia orodha kabla ya kuendelea. Moja kabla ya kuchukua hatua, pili wakati wa kuchukua hatua na tatu baada ya kuchukua hatua. Hizi ni nyakati ambazo unasimama na kujiuliza kipi muhimu kufanya na kama kimefanywa. Hapa unajihakikishia kuwa umefanya yale muhimu kabla ya kuendelea mbele.

Katika kuandaa orodha yako, pitia hatua hizi tatu;

Hatua ya kwanza; uandaaji wa orodha.

Katika hatua hii zingatia haya;

 1. Lengo kuu la orodha lijulikane.
 2. Kila hatua kuu ijumuishwe.
 3. Kila hatua ambayo inapaswa kuchukuliwa iwekwe.
 4. Orodha hiyo iweze kusomwa kwa sauti.
 5. Kuwe na vipengele vinavyoimarisha mawasiliano baina ya wahusika, ili wafanye kazi kama timu.

Hatua ya pili; uhariri.

Hapa unazingatia yafuatayo;

 1. Orodha iwe inaelekeza watu kuacha kwa muda kile wanafanya na kupitia orodha kwanza.
 2. Iwe na lugha rahisi na inayoeleweka.
 3. Ienee kwenye ukurasa mmoja.
 4. Isiwe na matumizi ya rangi nyingi.
 5. Herufi ziwe zinazosomeka kwa urahisi na za ukubwa sahihi kusomeka hata kwa mbali.
 6. Kuwa na vipengele chini ya kumi kwenye kila kituo cha kupitia orodha.
 7. Iwe na tarehe ambayo imehaririwa, na iwe inaendelea kuhaririwa kadiri maboresho yanavyofanyika.

Hatua ya tatu; uthibitishaji.

Hapa zingatia yafuatayo;

 1. Orodha ijaribiwe katika mazingira halisi ili kuona ufanisi wake.
 2. Orodha iboreshwe kulingana na matokeo ya majaribio.
 3. Orodha iendane na kazi inayofanyika, iende na mtiririko wa kazi.
 4. Makosa yaweze kutambuliwa na kutatuliwa haraka.
 5. Weka mpango wa marejeo ya orodha hiyo kwa siku zijazo.

Hivyo ndivyo unavyoweza kutengeneza orodha itakayokusaidia katika nyakati za dharura na changamoto zinazohitaji kufanya maamuzi ya haraka.

Kaa chini na utengeneze orodha zitakazokusaidia kufanya maamuzi kwenye kazi au biashara zako ili uepuke kufanya makosa ambayo yanakugharimu.

#3 MAKALA YA JUMA; HATUA NANE ZA KUTENGENEZA BIASHARA UNAYOWEZA KUIUZA.

Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara kwa lengo la kupata uhuru wa kifedha, uhuru wa muda na hata wa maisha pia. Hasa wale ambao wanakuwa wameanzia kwenye ajira, wanakuwa wamejifunza ajira ni kifungo kikubwa, kwa sababu mtu mwingine anaamua ulipwe kiasi gani, anakupangia muda wa kufanya kazi na hata maisha yako binafsi anayapanga yeye, mfano huwezi kuchagua kusafiri pale ambapo una jambo muhimu bila kwanza ya kuomba ruhusa kwa mwajiri wako.

Hivyo biashara imekuwa inaonesha matumaini ya kutoa uhuru wa kipato, kwa sababu wewe ndiyo bosi, inaonesha kukupa uhuru wa muda, kwa sababu hakuna anayekupangia muda wa kazi na pia inaonesha kukupa uhuru wa maisha yako, kwamba unaweza kufanya chochote bila ya kumwomba yeyote ruhusa.

Hizo huwa ni ndoto nzuri zinazowasukuma wengi kuingia kwenye biashara, lakini kwa bahati mbaya sana, zimekuwa zinabaki kama ndoto. Mtu anapoingia kwenye biashara, anagundua hana ule uhuru ambao alifikiri biashara itampa. Anakosa kabisa uhuru wa kipato kwa sababu biashara inamtegemea yeye, hivyo akifanya kazi fedha inaingia, asipofanya fedha haiingii. Pia uhuru wa muda unakosekana, kwa sababu yeye ndiyo kila kitu, na hivyo kulazimika kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi.

Na unaokosekana kabisa ni uhuru wa maisha, kwa kuwa na biashara ambayo inamtegemea mtu moja kwa moja, anakosa kabisa uhuru na maisha yake. Hapa mtu anakosa kabisa mpaka baina ya biashara na maisha, na kujikuta muda wote anajihusisha na biashara. Pia ule uhuru wa kusafiri au kufanya vitu vingine unakosekana kabisa, kwa sababu biashara inamhitaji mtu muda wote.

Hapa ndipo mtu anapohitaji kuchukua hatua za ziada, na hatua hizo ni kuweka mfumo mzuri wa kuendesha biashara yake ambao haumtegemei yeye moja ka moja.

Mwandishi John Warrillow  kupitia kitabu chake kinachoitwa Built to Sell: Creating a Business That Can Thrive Without You ametushirikisha hatua nane za kutengeneza biashara inayoweza kujiendesha yenyewe bila ya wewe kuwepo kabisa. Lakini pia ametufundisha jinsi tunavyoweza kuuza biashara zetu baada ya kuzitengenezea mfumo wa kujiendesha zenyewe na tukanufaika sana baada ya kuuza.

Kwenye makala ya juma hili la 25 nimekushirikisha hatua hizo nane za kutengeneza biashara itakayokupa uhuru mkubwa. Zisome hatua hizo nane hapa; Hatua Nane Za Kutengeneza Biashara Inayokupa Uhuru Mkubwa Na Unayoweza Kuiuza.

MUHIMU; Mwezi Julai 2019 tutakuwa na semina kwenye KISIMA CHA MAARIFA ambayo itahusu kutengeneza mfumo wa kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa. Hii siyo semina ya mtu yeyote makini kukosa. Kwa maelezo zaidi kuhusu semina hii soma hapa; Haya Ndiyo Masomo Kumi (10) Utakayojifunza Kwenye Semina Ya Kutengeneza Mfumo Wa Biashara.

#4 TUONGEE PESA; MATUMIZI YA ORODHA KWENYE UWEKEZAJI.

Rafiki, umewahi kujiuliza kwa nini watu wamekuwa wanatapeliwa? Tena siyo tu watu wa kawaida, bali watu ambao wana mafanikio makubwa na fedha nyingi. Watu hawa wamekuwa wanatapeliwa mara kwa mara. Wale wajanja wanaojua jinsi ya kucheza na akili za watu, wamekuwa wanatengeneza mitego ya kitapeli ambayo mtu usipokuwa makini unanasa na kupoteza fedha zako.

Wanasayansi wa ubongo na mishipa ya fahamu wamegundua kwamba matarajio ya kupata fedha huwa yanasisimua sehemu za ubongo ambazo huwa zinasisimuliwa na madawa ya kulevya kama cocaine. Hii ina maana kwamba unapooneshwa fursa ya kupata fedha, unaacha kufikiria kabisa na tamaa inakutawala. Na hakuna wakati mbaya kwenye maisha yako kufanya maamuzi kama wakati ambapo umetawaliwa na tamaa.

Mara zote tamaa inapokuwa juu, fikra zinakuwa chini na unafanya maamuzi ambayo ni mabovu kwako. Kwa sababu sehemu ya ubongo wako inayosisimuliwa na tamaa huwa ina nguvu sana. Ndiyo maana ulevi na uraibu wa madawa ya kulevya ni mgumu kuvunja, kwa sababu tamaa inapowaka, ni vigumu sana kuizima.

Hivyo wale wanaotaka kukutapeli fedha zako, huwa wanakuja kwako na kitu ambacho kitakupa tamaa ya kupata fedha, kitu ambacho kitasisimua sehemu ya ubongo inayotawaliwa na tamaa. Na ukishaingia kwenye tamaa hiyo, huwezi kufikiri sawasawa na hivyo unafanya maamuzi mabovu na kupoteza fedha zako.

Njia pekee ya kuondokana na hali hii, hasa kwenye fursa na uwekezaji ni kuwa na orodha ya vitu vya kuzingatia kabla hujatoa au kuwekeza fedha zako. Andaa orodha hii wakati ambao akili yako haijaingiwa na tamaa, na orodhesha vitu vyote muhimu ambavyo lazima viwepo ili utoe fedha zako au kuziwekeza.

Sasa unapojikuta kwenye hali ambayo fursa au uwekezaji umeibua tamaa ndani yako, usihangaike kabisa na tamaa hizo. Badala yake chukua orodha yako na anza kujiuliza je vitu vyote muhimu vipo? Kama kinakosekana hata kimoja basi jua hiyo siyo fursa au uwekezaji sahihi kwako na achana nao hata kama tamaa ni kubwa kiasi gani.

Wakati ambao umeshaingia tamaa siyo wakati wa kuamini maamuzi yako, bali ni wakati wa kuamini orodha sahihi uliyoiandaa kuwa mwongozo wako.

Kwa kutumia orodha kwenye kuziendea fursa na uwekezaji, utajiepusha kufanya makosa ambayo wengi huyafanya wanapokuwa na tamaa ya kupata fedha. Pia itakuzuia usitapeliwe na wale mafundi wa kucheza na akili za watu na kujipatia fedha kirahisi.

Usikubali kutoa fedha yako kuweka kwenye fursa au uwekezaji wowote kabla hujapitia orodha yako yenye vitu muhimu kuzingatia kwenye fursa au uwekezaji.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KWA NINI NIDHAMU NI NGUMU KUJENGA.

“Discipline is hard–harder than trustworthiness and skill and perhaps even than selflessness. We are by nature flawed and inconstant creatures. We can’t even keep from snacking between meals. We are not built for discipline. We are built for novelty and excitement, not for careful attention to detail. Discipline is something we have to work at.” ― Atul Gawande

Chochote unachofanya kwenye maisha yako, unapaswa kuzingatia misingi hii minne ili kufanikiwa, UAMINIFU, UJUZI, KUJALI WENGINE na NIDHAMU.

Sasa katika hayo manne, NIDHAMU ndiyo kitu kigumu kuliko vyote vile.

Atul Gawade anatuambia nidhamu ni ngumu sana kujenga kwenye maisha yetu kwa sababu nidhamu haipo kwenye asili yetu. Kwa asili sisi binadamu huwa tunapenda vitu vipya na vinavyosisimua. Hivyo tunapohitajika kurudia kufanya kitu kile kile kwa muda mrefu, tunachoka haraka na kuacha nacho.

Lakini bila ya nidhamu hatuwezi kufanya chochote kikubwa kwenye maisha yetu. Ili tufanikiwe tunapaswa kufanya vitu ambavyo haupendi kuvifanya na kuvifanya kwa muda mrefu na tena kwa kurudia rudia.

Hivyo nidhamu ni kitu ambacho tunapaswa kukijenga kwa nguvu kwenye maisha yetu. Tusitegemee kwamba nidhamu itakuja kirahisi, badala yake tuweke juhudi kwenye kuijenga na kuelewa pale tunaporudi nyuma kwamba ni asili yetu binadamu na hivyo kurudi kwenye nidhamu.

Pia unapokuwa na mtu mwingine anayekuangalia ni rahisi kujijengea nidhamu kuliko unapokuwa unajaribu kujenga nidhamu wewe peke yako. Kazana kujijengea nidhamu, siyo rahisi, lakini matokeo yake ni makubwa sana kwenye maisha yako.

Rafiki, hizi ndiyo TANO ZA JUMA hili la 25, nina imani umeondoka na maarifa sahihi ya kwenda kufanyia kazi, hasa kutengeneza orodha za kufuata kwenye kazi zako na maisha yako kwa ujumla ili upunguze makosa ambayo umekuwa unayafanya na yanakugharimu. Pia kazana kujijengea nidhamu, kwa kuwa na mtu anayekufuatilia kwa karibu kwa nidhamu unayojijengea.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili, nakwenda kukushirikisha MBINU 17 ZA KUKUWEZESHA KUTENGENEZA BIASHARA BORA. Mbinu hizi 17 zinatoka kwenye kitabu cha BUILT TO SELL. Hizi siyo mbinu za kukosa kama upo kwenye biashara au unategemea kuingia kwenye biashara.

Kuyapata #MAKINIKIA, unapaswa kuwa kwenye channel ya TALEGRAM YA TANO ZA JUMA. Maelekezo ya kujiunga na channel hii yako hapo chini. Chukua hatua ya kujiunga leo hii na utaweza kupata chambuzi za vitabu na vitabu kwa mwaka mzima. Wiki ya kwanza ni bure, na baada ya hapo unalipa elfu moja kila wiki.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu