“This is why we say that nothing happens to the wise person contrary to their expectations.”
—SENECA, ON TRANQUILITY OF MIND, 13.3b
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ambayo tumeiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari WENYE HEKIMA HAWANA MATATIZO…
Matatizo mengi kwenye maisha yetu tumekuwa tunayasababisha sisi wenyewe.
Kwa uzembe wetu wenyewe ambapo tunashindwa kufanya kile kilicho sahihi.
Kwa kufanya kwa mazoea na hivyo kusahau yale muhimu.
Kwa kuongea sana na kujikuta tumeropoka kitu ambacho siyo sahihi,
Kwa kuahidi vitu ambavyo hatuwezi kutekeleza.
Kwa kuwa na matarajio makubwa kwenye kitu ambacho hakipo kwenye udhibiti wetu,
Na kwa kuhangaika na vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wetu kuviathiri.
Ukiangalia vyanzo vyote hivi vya matatizo, dawa yake ni moja, hekima.
Ukiwa na hekima unafikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi na kuyasimamia.
Unasikiliza zaidi ya kuongea, unaahidi kidogo na kutimiza makubwa na unajua kipi kipo ndani ya uwezo wako na kukifanyia kazi na kipi kipo nje ya uwezo wako na kuachana nacho.
Kama kila siku unajikuta kwenye matatizo, basi jua shida kubwa inaanzia kwenye busara na hekima.
Jijengee busara na hekima na utaondokana na matatizo mengi unayokutana nayo kwenye maisha yako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujijengea BUSARA NA HEKIMA ili kuondokana na matatizo mengi ambayo umekuwa unajitengenezea mwenyewe.
#UnatengenezaMatatizoYakoMwenyewe #HekimaNiJawabuLaMatatizoMengi #KukaaKimyaSiyoUjinga
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1