Mafanikio ya kweli kwenye maisha ni pale mtu unapokuwa huru kabisa na maisha yako.
Pale ambapo wewe ndiye mwamuzi mkuu na wa mwisho wa maisha yako.
Pale ambapo hakuna chochote kinachoweza kutokea nje yako na kikavuruga chochote kile ndani yako.
Hayo ndiyo mafanikio ya kweli, yanayotokana na uhuru wa kweli kwenye maisha yako.
Lakini watu wengi wamekuwa hawana uhuru, licha ya kuonekana kwa nje kwamba wamefanikiwa.
Na kinachowanyima uhuru ni kuweka mategemeo yao kwenye vitu vya nje.
Pale ambapo mategemeo yao makubwa ni kwenye vitu vya nje, kuanzia wengine, mali walizonazo na chochote kile ambacho hakipo ndani yao, wanakuwa wamejiondoa kwenye uhuru.
Iko hivi rafiki, kitu chochote ambacho kipo nje yako, basi pia hakipo ndani ya udhibiti wako. Hii ina maana kwamba, chochote kinaweza kutokea na kikavuruga kabisa mategemeo uliyojiwekea. Hapo sasa ndipo unapojikuta kwenye hali ya utegemezi na kuvurugwa sana.
Lakini pale ambapo huna mategemeo makubwa kwenye kitu chochote cha nje, chochote kitakachotokea unakipokea bila ya tatizo, na hakikuvurugi kwa namna yoyote ile. Kwa sababu mategemeo yako hujayaweka kwenye vitu vya nje, badala yake yapo ndani yako.
Weka mategemeo yako makubwa ndani yako, kwenye vitu ambavyo viko ndani ya uwezo wako na unavyoweza kuviathiri.
Kuweka mategemeo yako makubwa kwa wengine au hata mali ulizonazo, ni kujiweka kwenye njia ya kuvurugwa, kwa sababu yapo yanayoweza kutokea yaliyo nje ya uwezo wako na yakakuvuruga sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,