Kama kazi au biashara unayofanya inakuchosha, ni kwa sababu unaangalia upande ambao siyo sahihi.

Iwapo unaangalia kazi au biashara unayofanya kwa kiasi cha fedha unachopata pekee, itakuwa ngumu sana kwako na hutaweza kukuza zaidi kipato chako.

Lakini unapoangalia kazi au biashara unayofanya kama fursa ya wewe kuwasaidia wengine, unaifurahia, na hapo unaona njia bora za kuwasaidia ambazo zitakuwezesha kuongeza kipato chako zaidi.

Watu wawili wanaweza kuwa kwenye kazi ya aina moja, mmoja akawa hana furaha kabisa huku mwingine akifurahia na kupiga hatua. Tofauti inaanzia kwenye mtazamo ambao watu hao wanao.

Aliyekuwa mhamasishaji na mwandishi Zig Zigler amewahi kusema mama yake alimwambia maneno haya ambayo yalikuwa na nguvu kubwa sana kwake; “mwanangu, kama unafanya kitu kifanye kwa moyo wako wote, kama huwezi kukifanya kwa moyo wako wote basi acha kukifanya, haitakuwa sawa kwako na hata kwa unayemfanyia.”

Kauli hiyo ina nguvu kubwa mno, kama utaweza kuitumia kwenye maisha yako ya kila siku. Chochote unachofanya, weka moyo wako wote kwenye kukifanya, na kama huwezi, basi achana nacho, usiendelee kupoteza muda wako na wa wengine pia.

Kazi au biashara unayoifanya ipende sana, hata kama siyo ulichokuwa unapenda kufanya. Lakini kwa wakati unafanya, ipende. Na njia rahisi kwako kupenda kile unachofanya, ni kuona namna wengine wananufaika na kile unachofanya.

Waangalie wengine kwanza kabla hujajiangalia wewe, tatua matatizo na changamoto za wengine na za kwako zitapotea zenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha